Pesa na siasa zinatupora vipaji

Dar es Salaam. Wazazi wenye mioyo na imani ya kilokole walimpa jina la Estelina. Binti mmoja wa Mzee Sanga, kutoka Nyanda za Juu Kusini kwenye baridi kama lote. 

Jamii kwa upana wake ikamtambua zaidi kwa kifupi cha jina lake la Linnah. Ndege mnana kweli kweli likiwa zao la jumba la vipaji Tanzania THT. 

Unamfahamu vyema huyu? Ni mrembo mfupi, shepu kama chupa ya Belea. Juu mdogo chini kajazia kwa namna inayopelekea mioyo ya kiume kitaa iende kasi kama SGR. 

Anamiliki sauti ya kumtoa nyoka pangoni. Na miguu iliyovimba kama chupa ya chai. Inatimisha ubora wa mwili aliopewa na Mungu Baba Mwenyezi. Achana na Linnah.

                      

Leo sizungumzii sauti yake na wala kukuacha macho yako yakoishia katika kiuno na umbile lake tu. Na yale mavazi yake na mapozi ya kike haswa. Hapana kuna la ziada zaidi toka kwake.

Hebu twende ndani zaidi kwa kile alichofanya kwenye sanaa. Zamani alikuwa mlokole siku hizi katupa kule. Anaongea analotaka na kuvaa kapendacho. Ulokole Bongo bana?

Baada wimbo mmoja kumtoa, kila mtu akataka kuisikia sauti yake tena na tena. Siyo mtunzi mzuri ila hakuna anayebisha sauti na uimbaji wake. Kwenye hilo hata ardhi na nyasi zina ushahidi.

Wapo waliojaribu ila aliwaacha mbali sana. Siyo kwamba hakuna aliyeimba kama yeye. Walikuwepo kina Mwasiti katika wakati wake, ila kwa zama zao hizo hakuna kama yeye. Linah alikuwa wa moto.

                        

Usimtaje yule ‘Mzungu Mswahili’ Vanessa Mdee, huyo kesi yake ni nyingine kabisa. Ana muda wake na lugha yake ya kuongelewa. Ila turudi kwa Linnah. 

Nenda kaisikilize sauti yake, uone namna anavyoteka hisia. Kupitia masikio yako bila hata kujua tabia yake sauti tu, itakufanya uwaze kummiliki milele amina. Hatari!
Mbali na Amini kumtungia baadhi ya nyimbo. pia walikuwa wapenzi na kimo walilingana. Walikuwa kama pacha, wakiimba kama walizaliwa tumbo moja. 

Wengi walidhani watafika mbali. Ila binafsi niliamini ladha ya umaarufu ilikuwa bado kugota kwenye mifupa ya Linnah. Waliachana ghafla kama Mbowe na Uenyekiti Chadema.

Baada ya Amini kumvusha katika shimo. Na kufanya aanze kung’aa kama Linnah badala ya Estelina Sanga. Meza ikapinduliwa kibabe na Lissu na ‘ubosi’ wa Chadema.

Mashairi ya Amini yalipomuweka juu ya sayari nzuri ya muziki. Akili yake ikaruka maili nyingi kuangalia  mwenye hadhi na maana kubwa zaidi ya Amini. Mchezo ukaisha.

Miezi kadhaa baadaye Linnah akafyatuka kuwa hapendi kuolewa na mume mfupi. Amini ana futi ngapi kwani? Pia inataka ngongoti. Kigoda cha kazi gani? Noma sana.

Linnah ghafla akanasa kwa mtu amtakaye kulingana na hisia zake. Na siyo wa kumtumia kama daraja la kuvukia, bila kuangalia moyo unataka nini. Maisha yana ukatili sana.

Mkwara wa kwanza mshikaji akatoa ndinga kujihakikishia lindo lake. Mtoto mzuri kama Linnah anayekutana na kila sampuli ya watu. Unaletaje ubahili wa Himo?

Usifanye mchezo kutoa gari katika utawala wa Ngosha. Amini akakaa kando maisha yakaendelea. Pesa ikaamua Linnah ampende nani na Amini akamtafute nani?

Hatuoni bidii ya Linnah kwenye ‘game’ kama zamani. Aliifanya muziki ili aishi vizuri. Alichotaka kupitia muziki akakipata kwa penzi. Hasira za gemu zikatoweka.

Pesa na siasa kwa kiasi kikubwa huathiri sanaa. Na kwa hili sanaa ya filamu ndiyo mhanga mkubwa.

Nina alitoweka kwenye filamu kwa sababu ya penzi na ndoa.
Mwenye mapenzi ya dhati na sanaa ataona jambo jema siasa kuwekwa kando. Siasa imewaweka kando Jojo, Keysha na Nikki wa Pili. Wapo wengi lakini.