
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema kwenye Fox News kwamba rais Donald Trump bado analenga makubaliano ya nyuklia na Iran, licha ya kuongezeka kwa uhasama kati ya Israeli na Tehran.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Tuko katika mkao wa kujihami huko Mashariki ya Kati, kuwa na nguvu, katika kutafuta makubaliano ya amani, na kwa hakika tunatumai kwamba ndivyo kitakachotokea,” Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amesema kwenye Fox News. “Na Rais [Donald] Trump ameweka wazi hilo, liko mezani. Swali ni iwapo Iran itakubali,” ameongeza.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesisitiza hapo jana kwamba kampeni ya Israel dhidi ya Iran “itabadili sura ya Mashariki ya Kati”, wakati nchi hizo mbili zikiendelea kushambuliana vikali kwa siku ya tano.
“Israeli inawaondoa viongozi wa kiusalama wa Iran mmoja baada ya mwingine na kwamba kwa kufanya hivyo wanabadili sura ya Mashariki ya Kati, na hilo litaleta mabadiliko makubwa ndani ya Iran yenyewe”, Netanyahu amesema akizungumza na waandishi wa habari jana jioni.
Hayo yanajiri wakati ubalozi wa China nchini Israel siku ya Jumanne uliwataka raia wake kuondoka nchini humo “haraka iwezekanavyo”, huku Israel na Iran zikiendelea kufanya mashambulizi makali.
“Ujumbe wa China nchini Israel unawakumbusha raia wa China kuondoka nchini haraka iwezekanavyo kupitia vivuko vya mpaka wa nchi kavu, kwa sharti kwamba wanaweza kuwahakikishia usalama wao binafsi,” ubalozi huo ulisema katika taarifa kwenye WeChat.