
Dar es Salaam. Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam (RCC), chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila, leo Jumatatu, Machi 24, 2024, imepokea na kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Ilala (DCC) ya kugawa jimbo la Ukonga kuwa majimbo mawili.
Mapendekezo hayo ni kuligawa jimbo hilo na kupatikana jimbo la Ukonga na Kivule.
Mchakato ujao ni kuwasilisha mapendekezo hayo kwa mamlaka husika, ikiwemo Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-Tamisemi) ili kupata ridhaa ya mwisho.
Akizungumza katika mkutano wa RCC jijini Dar es Salaam, RC Chalamila amesema, “Mapendekezo haya yamelenga kuboresha huduma kwa wananchi, kutokana na ukubwa wa jimbo hili na idadi kubwa ya watu. Kamati imepokea mapendekezo haya na sasa yatawasilishwa kwenye ngazi zingine kwa maamuzi zaidi,” amesema Chalamila.
Baada ya kugawanywa, Jimbo jipya la Kivule litakuwa na kata sita ambazo ni Kipunguni, Mzinga, Msongola, Kitunda, Kivule na Majohe, likiwa na eneo la kilomita za mraba 128 na idadi ya watu 431,736. Jimbo la Ukonga litabaki na kata saba: Ukonga, Chanika, Gongo la Mboto, Zingiziwa, Buyuni, na Pugu Station, likiwa na idadi ya watu 490,121.
Katibu Tawala Msaidizi Usimamizi, Ufuatiliaji, na Ukaguzi Mkoa wa Dar es Salaam, Saloni Asheri Nyika amesema, “Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa ilituma wataalamu waliokwenda kujiridhisha na kugundua kuwa jimbo hilo linahitaji kugawanywa, huku vigezo vya idadi ya watu na shughuli za kiuchumi vikizingatiwa.”
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba Gadafi, amesema kugawanya majimbo kunalenga kuboresha huduma kwa wananchi.
Endelea kufuatilia Mwananchi.