Penalti ilivyozua gumzo, Adana yagomea mechi ya Galatasaray

Uturuki. Mchezo wa Ligi Kuu Uturuki umevunjika baada ya wachezaji wa Adana Demirspor kugomea mechi wakipinga maamuzi ya mwamuzi aliyetoa penalti tata kwa Galatasaray. 

Mwamuzi wa mchezo huo Oguzhan Cakir alitoa penalti iliyowekwa kimiani katika dakika ya 12 na mshamuliaji Alvaro Morata, aliyejiunga na Galatasaray kwa mkopo akitokea AC Milan.

Aidha, uamuzi huo uliwakasirisha wachezaji wa Adana Demirspor na benchi lao la ufundi, wakidai kuwa penalti hiyo haikuwa halali licha ya VAR kuidhinisha maamuzi ya mwamuzi. 

Penati hiyo ilitolewa baada ya mchezaji wa Galatasaray, Dries Mertens kuangushwa kwenye eneo la hatari licha mgusano mdogo ulikuwepo kati yake na beki wa Adana, Semih Guler.

Baada ya tukio hilo, kocha wa Adana Demirspor, Mustafa Alper Avcı, aliwaelekeza wachezaji wake kuondoka uwanjani kama ishara ya kupinga maamuzi hayo, hatua iliyosababisha mchezo kusimamishwa.

Akizungumzia sakata hilo, rais wa Adana Demirspor, Murat Sancak, amesema uamuzi wa kutoka uwanjani ulikuwa ni msimamo wa klabu kupinga kile alichokiita ‘uonevu wa wazi’ kutoka kwa waamuzi.

Kwa upande mwingine, kocha wa Galatasaray, Okan Buruk, ameeleza kusikitishwa kwake na uamuzi wa wapinzani kugomea mechi, akisema tukio hilo linaharibu taswira ya soka la Uturuki.

Kutokana na mchezo huo kuvunjika, inatarajiwa Shirikisho la Soka la Uturuki litatoa uamuzi rasmi kuhusu hatma ya matokeo ya mchezo huo, huku uwezekano wa Adana Demirspor kupokonywa alama au kupigwa faini ukiwa njiani.

Tukio hili limeongeza mjadala mkali kuhusu viwango vya waamuzi kwenye Ligi Kuu ya Uturuki, huku baadhi ya wachambuzi wakidai kuwa msimu huu umejaa maamuzi tata yanayozua utata mkubwa kwenye soka la Uturuki. 

Galatasaray ndio vinara wa ligi wakiwa na pointi 57 baada ya mechi 21 huku Adana Demirspor ikiburuza mkia ikiwa pointi tano katika mechi 21.