Morogoro. Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Nchini (PDPC) imefanya warsha kwa wahariri wa vyombo vya habari ili kuelimisha kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi za watu, hasa wanapochapisha au kutangaza habari zinazohusiana na maisha ya mtu.
Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk Emanuel Mkilia, akifungua warsha hiyo leo Jumamosi Machi Moshi, 2025, mjini Morogoro, amesema uwepo wa teknolojia umefanya taarifa kusambaa kwa kasi na haraka, hivyo ni muhimu kuzingatia ulinzi wa taarifa binafsi.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dk Emanuel Mkilia akifungua warsha kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyoandaliwa na tume hiyo kwa jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari nchini. Picha Hamida Shariff, Mwananchi
“Zana ya ulinzi wa taarifa binafsi ni muhimu kwa sababu inazungumzia udhibiti wa taarifa binafsi. Kuna kampuni kubwa zimepata hasara kwasababu ya kuvunja sheria ya taarifa binafsi, hivyo kutoeleweka kwa zana hii kunaweza kuleta madhara makubwa kwa mtu binafsi na hata kwa taarifa za nchi.
“Ulinzi wa taarifa binafsi ni muhimu ili kuzuia wizi wa taarifa binafsi. Ni vema tukaelewa zana nzima inayohusu usalama wa taarifa binafsi,” amesema mkurugenzi huyo.
Amesema anafahamu kuwa wahariri wanapotekeleza majukumu yao katika vyombo vya Habari, wanachakata taarifa kabla ya kwenda kwa umma, hivyo ni vema wakalinda taarifa hizo binafsi kwa mujibu wa sheria.
“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunazingatia ulinzi wa taarifa zetu ili kulinda faragha za watu. Hakuna anayependa faragha zake zitolewe hadharani na maisha ni kama mchezo wa kuigiza, maana kuna nyuma ya pazia na katika stage.

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa kwenye warsha kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyoandaliwa na Tume ya ulinzi wa taarifa binafsi PDPC yaliyofanyika leo Machi 1, 2025. Picha Hamida Shariff, Mwananchi
“Hakuna anayependa ujue anayofanya nyuma ya pazia, hivyo unaweza kuona umuhimu wa jambo hili tunalozungumzia,”amesema Dk Mkilia.
Ametoa rai kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya Habari kuhakikishe jamii inaelewa umuhimu wa kulinda faragha za watu, kwa kuwa “kwani tuko katika dunia ya kidigitali. Mnaona siku hizi kituko chochote kikitokea kinasambaa kwa kasi sana, kwa hiyo mnaweza kuona msingi wa ulinzi wa taarifa binafsi.”
Wakati huo huo, Dk Mkilia amesema Tume inatambua kuhusu umuhimu wa hariri katika kufikisha elimu ya uelewa kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi kwa umma kwa sababu wako katikati ya waleta taarifa na walaji. Amesema Wahariri wakiamua kuleta sumu nchi haitakalika.
“Niseme machache katika jambo hili, tume hii imesimama katikati ya teknolojia na maisha ya watu, tumejaribu kuangalia maisha ya watu wanavyoishi, lakini teknolojia haina siri, haina hisia lakini mwisho wa siku tunamuangalia huyu mtu ambaye anatumia teknolojia, kwa hiyo tunalojukumu la kulinda hisia.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akizungumza na wahariri waliohudhuria warsha iliyohusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyoandaliwa na PDPC leo Machi 1, 2025 mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
“Warsha hii inatoa fursa kujifunza na kujengeana ulewa wa kina jinsi ya kulinda faragha za watu katika kazi zenu za habari. Warsha hii ni mwanzo maana jukumu letu kubwa ni taarifa kwa umma. Tutaendelea kutumia jukwaa hili ili kuhakikisha watu ambao tumepanga kuwafikia wajue mambo ya msingi kuhusu taarifa binafsi.
“Na sisi tume sehemu kubwa ya kazi yetu ni elimu kwa umma, hivyo kwa kupitia jukwaa hili la wahariri ndio silaya yetu muhimu ya kuitumia kuifikia jamii inaelewa umuhimu wa kulinda faragha za watu,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deogratius Balile, ameishukuru PDPC kwa kuandaa warsha hiyo na amesema kwa sasa wahariri wa mitandao ya kijamii wanahusishwa na wahariri wa vyombo vingine kama vile magazeti, redio na televisheni katika juhudi za kulinda taarifa binafsi.
Mhariri wa habari na Meneja wa The Guardian Digital, Solome Kitomari akizungumzia warsha hiyo, amesema ni muhimu sana kwa kipindi hiki ambacho mitandao ya kijamii imeshika kasi na taasisi mbalimbali za kifedha pia zinahitaji taarifa binafsi, kama vile namba ya NIDA na namba za simu, wakati wa kutoa mikopo.
Hivyo, Kitomari amesema wahariri wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi wa taarifa binafsi unazingatiwa.