PAUL PETER…Nyota asiyemsahau kocha Aristica Cioaba

Mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Paul Peter Kasunda ni miongoni mwa nyota wanaofanya vizuri msimu huu katika Ligi Kuu hadi sasa, huku akitaja mambo mbalimbali yanayochangia ubora wake, bila kumsahau aliyekuwa kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba.

Nyota huyo amefunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara, akiwa ni mchezaji mzawa anayefanya vizuri, jambo lililovutia gazeti hili kumtafuta na kufanya naye mahojiano, ili kujua safari yake ya soka na siri iliyojificha juu ya kiwango chake bora.

CIOABA AMPA SHAVU

Paul anasema moja ya kocha ambaye hatokaa akamsahau katika maisha yake yote ni Mromania, Aristica Cioaba, kwani ndiye aliyempa nafasi ya kucheza kuanzia timu ya vijana ya Azam FC chini ya miaka 20, hadi kumpandisha kuchezea ya wakubwa.

“Ni miongoni mwa makocha ambao sitokaa nikawasahau, nakumbuka msimu wa 2017-2018, alinipa nafasi na kuniambia nina uwezo hivyo nipambane kikosini, kiukweli nilionyesha kwa vitendo na anabakia kocha muhimu kuwahi kunifundisha,” anasema Paul.

MAISHA YA AZAM FC

Nyota huyu aliyeitumikia Azam FC kuanzia timu ya vijana hadi ya wakubwa, anasema maisha ndani ya kikosi hicho hayakuwa mazuri wala mabaya sana, ingawa anachojivunia ni jinsi alivyojifunza kupigania nafasi sehemu yenye wachezaji bora zaidi.

“Nilikuwa na miaka mitano bora sana Azam FC, unapotoka timu ya vijana hadi ya wakubwa ni jambo la kujivunia kwa sababu ya ushindani uliopo, baada ya hapo niliondoka nikijiona nimekuwa kiakili ili nikatafute changamoto sehemu nyingine.”

ATAMANI KUACHA SOKA

Paul anasema moja ya jambo ambalo hatokaa akalisahau ni kitendo cha kutaka kuachana na soka na kuamua kufanya kazi ya tofauti, kwa kile anachodai sababu kubwa ni kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi mara kwa mara.

“Mchezaji yoyote huwa anapenda kuona akipata nafasi ya kucheza, kwangu nikiwa Azam FC ilikuwa shinda kidogo kwa sababu ya wachezaji waliopo, nilitamani kuacha na kufanya biashara japo sikukata tamaa niliamini uwezo niliokuwa nao,” anasema.

10 BORA YA WAFUNGAJI

Nyota huyo anasema moja ya jambo analoomba ni kuona mwisho wa msimu huu anakuwa miongoni mwa wachezaji walioingia katika 10 bora ya ufungaji, kwani hatua hiyo itamuongezea motisha ya kupambana zaidi na kutimiza malengo yake aliyojiwekea.

“Ikitokea nikiwa mfungaji bora nitafurahi kwa sababu ni malengo ya kila mshambuliaji, kwa sasa natamani niendeleze hiki ninachokionyesha na nishike chati ya wafungaji 10 bora, ila ikitokea ya kutokea basi nitakubaliana na matokeo yoyote.”

MECHI ASIYOISAHAU

Paul anasema moja ya mechi ambayo hatokaa akaisahau katika maisha yake ni ile ya Ligi Kuu Bara kati ya Singida United dhidi ya Azam FC iliyochezwa msimu wa 2017-2018, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Septemba 30, 2017.

“Sitoisahau katika maisha yangu kwa sababu ndio siku ya kwanza niliyopandishwa timu ya wakubwa ya Azam FC, jambo pia la kipekee zaidi ni kufunga bao moja la kusawazisha lililotupatia pointi moja na mechi hiyo kuisha sare ya kufungana 1-1.

NYOTA ANAYEMVUTIA

Paul anasema mchezaji anayemvutia kwake ni nyota wa timu ya taifa ya Brazil aliyewika na klabu za Paris Saint-Germain (PSG), Barcelona na Al Hilal, Neymar da Silva Santos Junior, kutokana na aina ya uchezaji wake mzuri akiwapo uwanjani.

“Ni miongoni mwa nyota ninaowafuatilia sana na kukubali aina ya uchezaji wao, kiukweli mimi nishabiki yake kama ambavyo walivyokuwa wengine, Neymar ni mchezaji asiyechosha kumuangalia jinsi anavyocheza na kujifunza vitu vingi kutoka kwake.”

FEDHA YAKWAMISHA DILI LA LIBYA

Dirisha dogo la Januari 2025, Paul alipata dili la kwenda Libya kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha Al Dahra Tripoli FC, ingawa ofa hiyo iligonga mwamba, huku akifichua sababu kubwa iliyosababisha ni kutokana na kiasi pia kidogo cha fedha.

“Siwezi kusema ni kiasi gani cha fedha kililetwa, lakini ni kweli ofa hiyo ilikuja mezani ila viongozi wangu wa Dodoma Jiji waliikataa kwa walichoeleza ni kidogo, kwa kifupi hiyo ndio sababu kubwa iliyosababisha nisijiunge nao,” anasema.

BEKI KIKWAZO KWAKE

Anasema miongoni mwa mabeki waliokuwa wakimsumbua kila akikutana naye ni aliyekuwa beki wa Coastal Union, Dodoma Jiji FC na Mtibwa Sugar FC, Amani Kyata ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi na mchambuzi wa video ‘Video Analyst’ wa Kagera Sugar.

“Kyata alikuwa ananisumbua sana kwa sababu alikuwa ananijulia ujanja wangu, kila nikitambua ninaenda kukutana naye huwa najiandaa vya kutosha nikijua leo kazi itakuwepo na kweli inakuwa hivyo, kiukweli jamaa alinisumbua vilivyo,” anasema.

PACHA YAKE NA KIPAGWILE

Anasema anafurahia sana kucheza na winga nyota mwenzake, Iddi Kipagwile kutokana na ushirikiano waliokuwa nao uwanjani, jambo linalosababisha kufanya vizuri msimu huu, huku wakiibeba timu kutokana na idadi ya mabao waliyoyafunga hadi sasa.

“Kipagwile anajua njia zangu na mimi pia namjulia ndio maana tumekuwa tunafanya vizuri msimu huu, mwingine ninayefurahia kucheza naye ni Habibu Kyombo anayecheza Pamba Jiji kwa sasa, kwa sababu wote tunajuana aina ya uchezaji wetu,” anasema.

Jina: Paul Peter Kasunda.

Timu alizopita: Azania FC, Mugabe FC, Azam Academy, Azam FC, KMC FC, TZ Prisons na sasa Dodoma Jiji FC.

Nafasi: Mshambuliaji.

Jezi Namba: 51.

Kuzaliwa: Januari 2, 1999.

Taifa: Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *