Pastor Myamba kutoka uchungaji wa ‘Bongo Movie’ hadi madhabahuni

Dar es Salaam. Si mwingine ni mwigizaji Emmanuel Myamba ‘Pastor Myamba’ ambaye kwa sasa ni mchungaji rasmi akiwa Kiongozi wa Kanisa  la House of Victory Church (HVC) lililopo kwenye maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Mwigizaji huyo ambaye alianza kuigiza mwaka 2002, amesema mtu wa kwanza kumpatia uhusika wa uchungaji alikuwa marehemu Steven Kanumba katika filamu iitwayo ‘Johari’.

                          

“Nilivyocheza kama mchungaji watu wakaanza kuniita mchungaji kwa hiyo nimeitwa sana kabla ya kuwa na kanisa.  Kisha kama miaka 20 baadaye ndiyo nikaja kufungua kanisa,”anasema.

Anasema uhusika wake kama mchungaji kwenye filamu mbalimbali siyo sababu ya yeye kuwa mchungaji na kufungua kanisa, bali ni wito aliokuwa nao tangu zamani.

“Hata kipindi hicho nilikuwa nimeokoka na waigizaji wenzangu walikuwa wananiita mchungaji. Kwa hiyo nilikuwa na wito wa uchungaji, lakini sikujua lini utakomaa ili niwe na kanisa. Mpaka mwaka 2017 ndiyo rasmi nikaanzisha kanisa langu  HVC,”anasema.

                        

Vipo vitu ambavyo watu huvifanya kutokana na fursa

wanazopata hata kama ikiwa siyo kazi za ndoto zao, lakini kwenye uchungaji Myamba anasema ni wito  kutoka kwa Mungu.

“Biblia imeeleza kuwa wapo wachungaji wa mshahara, habari ya uchungaji lazima uwe na wito kwa hiyo ukimwambia mtu afungue tu kanisa kwa sababu ya jina anaweza akafikia kipindi likamshinda lazima awe na kitu Mungu amekiweka,”anasema.

Scene hizi hawezi kucheza kamwe 

Wanasema mkulima hachagui jembe, lakini kwa Myamba ni tofauti kwani anachagua uhusika wa kucheza kwenye filamu hasa akizingatia utu wake na waumini wake anaowaongoza. 

“Kuna baadhi ya scene mimi huwa sizichezi kabisa ni msimamo wangu tangu kipindi hicho mfano, siwezi kucheza nimewekwa kwenye jeneza pia siwezi kucheza nikiwa mtupu.

“Kifua wazi naweza nikacheza inategemeana inataka kuwasilisha  nini  lakini isiwe kifua wazi moja kwa moja.  Kwa sababu nyuma yangu nina watoto wa kiroho kwa hiyo kila kitu ninachokifanya lazima kiwe na mipaka na kiasi,”anasema. 

                       

Anasema kama scene itamtaka aigize anaenda kufanya uzinzi na binti siyo lazima video ioneshe wakiwa wanabusu.  

“Kuna scene mimi naweza nikaigiza nipo na msichana lengo ni kufikisha ujumbe, mchungaji  ameanguka dhambini. Inatosha mimi na huyo msichana kuonekana  tunaingia tu sehemu  lakini siyo mpaka kwenda kwenye deep kiss,”anasema.

Anasema anafanya hivyo kwa lengo la kujilinda yeye na watu wengine  wanaotazama.

“Nataka nitengeneze sinema ambazo  mtu anaweza kuangalia akiwa na baba yake bila shida yoyote. Masuala ya kubusu siyo utamaduni wetu.”

Kufanya sanaa ni dhambi ?

Kwa miaka kadhaa kumekuwa na mitazamo kutoka kwa baadhi ya wasanii kuwa kufanya sanaa ya muziki au maigizo ni dhambi. 

Utakumbuka  mwaka 2016, mwanamuziki wa Taarab Mzee Yusuph alitangaza kuacha muziki na kumrudia Mungu lakini ilipofika 2020 alirudi tena kwenye muziki.

                     

Naye msanii Snura Mushi, Julai 2024, alitangaza kuachana na sanaa na siyo hao tu hata Suma Lee naye ameacha muziki na kumrudia Mungu.

Kutokana na hayo Pastor Myamba amesema dhambi ipo kwenye kila fani, mtu binafsi ndiyo anaweza kuamua kuiepuka.

“Kwenye hii dunia unaweza ukaamua kuishi kwa dhambi au kwa utakatifu  kila pahali kuna watakatifu na wenye dhambi na ndiyo maana kuna nyimbo za Bongo Fleva na gospo  lakini wote ni waimbaji. 

“Mimi nimekaa kwenye  kiwanda cha filamu kwa miaka karibia ishirini lakini sijawahi kutenda dhambi kwa sababu ya usanii. Vitu vingine ni asili ya mtu inaonekana ulivyokuwa kwenye sinema ulikuwa mtenda dhambi  kwa hiyo saa unadhani  wote wanatenda dhambi,”anasema.

                     

Hichi ndicho kilifanya apumzike “Unajua chanzo cha mimi kuacha kuzalisha sinema haikuwa kwa ajili ya kuanzisha kanisa. Mimi nilikuwa msanii lakini pia nilikuwa prodjuza  kwa hiyo unapozalisha kazi unaweka hela na unategemea irudi.

“Soko la filamu lilisimama kwenye upande wa CD  nilipambana sana  kutaka kuliingiza kwenye digitali lakini kipindi hicho ilikuwa  shida sana. 

“Nakumbuka kipindi cha nyuma, kabla Netflix huku haisikiki, 2009 niliwahi kufunga safari hadi Marekani kwenda kuangalia filamu zetu zinaweza zikaingia vipi kwenye platform hiyo,”anasema.

Anasema alifanya hivyo kwa sababu alijua kuwa soko la CD linaelekea kuisha.

                     

“Marekani nilionana na Make-Up artist wa Denzel Washington niliongea naye kwa muda mrefu sana, karibia saa nne, aliyoniambia nikaona mlango kwetu bado mgumu sana,”anasema.  

                        

Licha ya hayo Myamba anasema taifa halikujiandaa kuvuka kutoka kwenye kuuza CD na kuhamia digitali. Hivyo basi ameziomba taasisi  kama COSOTA au Basata kuangalia kwa haraka mabadiliko yanayotokea.

“Mimi kwa sasa nimerudi kwenye gemu kwa sababu naona soko limekuwa mitandaoni watu wanaweza kuweka kazi zao na wakajipatia kipato. Nimerudi na kitu kinatwa Hollymovie ambacho kitakuwa kinahusika na filamu za dini kwa asilimia mia moja,” anasema.