

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sonia Oxley
- Nafasi, BBC
Takribani wana michezo 10,500 kutoka kote ulimwenguni watashiriki katika michezo 32 kwenye michuano ya Olimpiki huko Paris msimu huu wa joto.
BBC Sport inaangazia nyota wakubwa na mafanikio yao katika mashindano ya kimataifa.
Leon Marchand (Ufaransa) – kuogelea

Chanzo cha picha, Getty Images
Bingwa huyo mara tano wa dunia anatazamiwa kushinda medali nyingi za dhahabu kwenye mchezo wa kuogelea.
Marchand mwenye umri wa miaka 22, ni mwanafunzi wa sayansi ya kompyuta katika chuo kikuu nchini Marekani, anajuulikana kwa kuvunja rekodi.
Ikiwemo rekodi ya mitndo mbalimbali ya kuogelea ya mita 400 – ambayo ilikuwa imedumu kwa miaka 15 – mwaka 2023.
Simone Biles (US) – sarakasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Miaka mitatu iliyopita watu wengi walidhani, hawatomuona tena Biles baada ya michezo ya Olimpiki.
Biles alijiondoa katika mashindano kadhaa katika michezo ya Tokyo. Alichukua mapumziko kabla ya kurudi kwenye mashindano Juni 2023.
Biles tangu wakati huo amepata medali tano za ubingwa wa dunia, zikiwemo dhahabu nne. “Nahisi kujiamini sana kiakili na kimwili,” alisema mwaka huu.
Novak Djokovic (Serbia) – tenisi

Chanzo cha picha, Getty Images
Dhahabu ya Olimpiki ndiyo tuzo kubwa ambayo haipo kwenye mkusanyiko wa tuzo zake. Lengo lake mwaka huu katika mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024, ni kupata medali hiyo.
Mwaka huu kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37, haukuwa mwaka bora, hajashinda taji lolote na hayuko tena kileleni mwa viwango vya ulimwengu.
Jeraha lilikatiza michuano yake ya French Open kabla ya robo fainali. Ingawa alifika fainali ya Wimbledon mwezi huu kwa kufungwa goti, lakini alizidiwa kwa kiasi kikubwa na Carlos Alcaraz.
Hata hivyo, ikiwa yuko fiti, anaweza kupata hata shaba kama alioshinda Beijing 2008.
Ledecky (US) – kuogelea

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, kuna mtu yeyote anaweza kumzuia bingwa huyo wa mara saba wa Olimpiki?
Akiwa yuko tayari kushiriki mara ya nne, Ledecky mwenye umri wa miaka 27, anatajwa kuwa mwogeleaji wa kike aliyefanikiwa sana katika Olimpiki.
Ana nafasi ya kuweka rekodi kwani anatarajiwa kushindana katika matukio manne – mita 400, mita 800, mita 1500 na mita 4×200.
Ana medali 10 tayari, Ledecky anaweza kuvunja rekodi ya Jenny Thompson mwenye medali 12 ikiwa atashinda zaidi.
Noah Lyles (US) – mkimbiaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkimbiaji wa Marekani amejiwekea malengo makubwa.
Analenga kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda medali nne za dhahabu kwenye mbio hizo za Olimpiki, akilenga kushinda katika mbio za mita 100, 200 na 4×100 na 4×400 za kupokezana vijiti.
Alishinda dhahabu katika mashindano matatu ya kwanza kati ya mashindano hayo kwenye mashindano ya dunia mwaka jana.
Ikiwa hilo halitoshi, ana malengo ya kushinda rekodi za dunia za mita 100 na 200 za gwiji wa Jamaica Usain Bolt.
Tangu achukue medali ya shaba ya mita 200 huko Tokyo 2020, Lyles ametawala mbio kwenye jukwaa la kimataifa na anaonyesha kipaji na ushujaa ambao unaweza kujaza pengo la Bolt tangu astaafu 2017.
Faith Kipyegon (Kenya) – mkimbiaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Bingwa wa Olimpiki mara mbili wa mbio za mita 1500 na anashikilia rekodi ya dunia kwa umbali huo.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 30 anawinda medali mbili za dhahabu mjini Paris atakapo rudia mbio za mita 1500 na 5,000, kama ilivyokuwa katika mashindano ya dunia ya mwaka jana.
Kipyegon alianza maisha yake ya riadha akiwa na umri wa miaka 16 na alishinda taji lake la kwanza la kimataifa akikimbia bila viatu katika mashindano ya World Junior Cross Country Championships mwaka 2011.
Neeraj Chopra (India) – mrusha mikuki

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni maarufu sana nchini India na ana wafuasi milioni tisa kwenye Instagram.
Mwanamichezo wa kwanza wa India kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki, Chopra ana lengo la kutetea taji lake katika kurusha mkuki mjini Paris.
Mafanikio yake ya kushangaza huko Tokyo, ambapo pia alikuwa mwanamichezo wa kwanza wa Asia kushinda dhahabu ya Olimpiki ya mkuki.
Miongoni mwa wanaoweza kumpa changamoto ni Arshad Nadeem kutoka Pakistani – taifa hilo ni mpinzani mkubwa wa India katika michezo.
Nadeem anajivunia historia ya kuwa mwanariadha wa kwanza kutoka Pakistani kufuzu katika fainali ya Olimpiki ya Tokyo 2020.
Alitwaa medali ya fedha nyuma ya Chopra kwenye mashindano ya dunia ya mwaka jana na anaweza kuwa mshindi wa kwanza wa medali ya Olimpiki ya nchi yake mwaka huu.
Olha Kharlan (Ukraine) – vitara

Chanzo cha picha, Getty Images
Bingwa huyo mara nne wa dunia alikuwa katika hatari ya kukosa michezo hiyo kwa sababu ya marufuku iliyowekwa kwa kukataa kupeana mkono na mpinzani wake wa Urusi.
Kharlan aliondolewa kwenye mashindano ya dunia ya mwaka jana baada ya kukataa kupeana mikono kufuatia ushindi wake dhidi ya Anna Smirnova.
Mshindi huyo mara nne wa medali ya Olimpiki ameahidi kuleta “tumaini” kwa raia wa Ukraine huku kukiwa na vita vinavyoendelea kufuatia uvamizi wa Urusi miaka miwili iliyopita.
Hakuna wanamichezo wa Belarus au Urusi ambao wamealikwa kushiriki mjini Paris, Kharlan mwenye umri wa miaka 33 anasema hayo ni “mafanikio.”
Stephen Curry (US) – mpira wa kikapu

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyota wa NBA Stephen Curry atacheza mechi yake ya kwanza ya Olimpiki mjini Paris.
Mlinzi wa timu ya Golden State Warriors, ni sehemu ya timu ya wanaume ya Marekani iliyo na nyota wengi ambao wanawinda medali ya 16 ya dhahabu ya Olimpiki. Wameshinda kila dhahabu tangu 2004.
Medali ya Olimpiki ndiyo kitu pekee kinachokosekana kwenye medali za Curry, ana mataji manne ya NBA, tuzo mbili za Mchezaji Bora wa NBA (MVP) na mbili za Kombe la Dunia.
LeBron James, mfungaji bora wa muda wote wa NBA, atacheza kwenye michezo hiyo kwa mara ya kwanza tangu London 2012, huku Kevin Durant akitafuta kuwa mwanariadha wa kwanza wa kiume kushinda medali nne za dhahabu za mpira wa kikapu.
Shelly-Ann Fraser-Pryce (Jamaika) – mkimbiaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Ana umri wa miaka 37. Anashiriki Olimpiki yake ya tano na ya mwisho. Ni bingwa mara tatu wa Olimpiki.
Bingwa mara tano wa dunia wa mbio za mita 100, anakabiliwa na majeraha msimu huu lakini atashindana katika tukio lake la kihistoria mjini Paris pamoja na mchezaji mwenzake Shericka Jackson, ambaye anawinda medali yake ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki.
Watakuwa kwenye timu ya mbio za mita 4×100 za kupokezana vijiti huku Jamaica ikitaka kutetea ubingwa wao.
Wanamichezo wengine
Isabell Werth: Mwanamichezo wa Ujerumani katika mchezo wa farasi Isabell Werth, 55, hajawahi kukosa ushindi wa medali ya dhahabu katika Olimpiki yoyote ambayo ameshiriki.
Akielekea kwenye mchezo wake wa saba, atakuwa na matumaini ya kuongeza dhahabu ya saba na fedha tano na kupanua rekodi yake ya kuwa mpanda farasi mwenye historia nzuri katika Olimpiki.
Mlenga shabaha, Nino Salukvadze: Nino Salukvadze, pia ana umri wa miaka 55, atashiriki katika mashindano yake ya 10 ya Olimpiki. Salukvadze atakuwa wa kwanza kushirikia mara kumi mfululizo katika miachuano hiyo.
Katika mieleka, Mijain Lopez: Raia huyu wa Cuba anaweza kuwa mwana mieleka wa kwanza katika mchezo wowote kushinda medali tano za dhahabu mfululizo.
Mwaustralia Jess Fox: Amekuwa akitawala mbio za mitumbwi na anaweza kuwa mtu wa kwanza kushinda dhahabu tatu za mitumbwi kwenye michezo hiyo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla