Roma. Ibada rasmi ya kuwekwa wakfu kwa Papa Leo wa XIV, papa wa kwanza kutoka Marekani, inaendelea katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, ikihudhuriwa na viongozi wa dunia, familia za kifalme, na maelfu ya waumini.
Papa huyo wa 267, aliwasili mjini Vatican kwa kutumia gari maalumu la kipapa (popemobile) na kupokelewa kwa shangwe na umati mkubwa wa watu alipokuwa akizunguka katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, kwa kutumia gari hilo lililoundwa kwa ajili hiyo.
Ibada ya leo Mei 18, 2025 itakuwa alama na ishara nyingi za kidini, ikiwemo kumvisha rasmi Papa Leo mavazi ya ofisi yake, ikiwemo (pallium) vazi la sufi ya kondoo linaloashiria jukumu lake la kichungaji kwa kanisa na nafasi yake kama mchungaji wa kundi lake na pete ya mvuvi, inayoashiria mamlaka ya Papa kama mrithi wa Mtakatifu Petro, ambaye alikuwa mvuvi kwa kazi na Wakatoliki wanamchukulia kama papa wa kwanza.

Miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo ya saa mbili leo Jumapili ni Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky na Rais wa Peru, Dina Boluarte kiongozi wa nchi ambayo Papa Leo alihudumu kama mmisionari na askofu kwa miongo kadhaa.
Mataifa kutoka kote duniani yamewakilishwa, Vatican ikiwakaribisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 150 duniani.

Mei 8, 2025, makardinali walio na umri chini ya miaka 80 kutoka duniani kote, walimchagua Robert Prevost kuwa Papa mpya ambapo saa 12:07 jioni (saa 1:07 usiku saa za Afrika Mashariki na Kati), ilishuhudiwa moshi mweupe kupitia dohani katika kanisa dogo la Sistine kuashiria kuwa Papa amepatikana.
Kengele zilisikika zikigongwa wakati wa tukio hilo ikiwa ni sehemu ya shangwe za kupatikana Papa mpya, makardinali 133 walimchagua mrithi wa Papa Francis aliyefariki dunia Aprili 21, 2025.
Siku hiyo, umati wa watu, wapatao 20,000 waliofika kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro kumkaribisha Papa mpya, walilipuka kwa shangwe na nderemo wakipeperusha bendera za nchi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Baadhi ya watu walioshuhudia kufuka kwa moshi huo walitumia simu zao za mkononi kuchukua kumbukumbu ya tukio hilo. Moshi mweupe ulitanguliwa na mweusi uliofuka kwa nyakati tofauti mara mbili, Mei 7, 2025 usiku.

Katika historia ya kanisa, mkutano uliofanyika kwa muda mfupi unakadiriwa kuwa saa 10 uliofanyika mwaka 1503 baada ya kifo cha Papa Pius III. Makardinali walikutana na kumchagua Papa Julius II.
Mkutano mrefu zaidi katika historia ulichukua takribani miaka mitatu (siku 1,006) alipochaguliwa Papa Gregory X mwaka 1271.
Papa Leo XIV, mpenda mchezo wa tenisi aliyejulikana pia kwa jina la ‘Bob’ anatajwa kuwa mtu atakayeendeleza maono ya Papa Francis.

Amefanya kazi kwa miaka mingi nchini Peru na alikuwa chaguo maarufu miongoni mwa makardinali wa Amerika ya Kusini na Amerika Kaskazini, ingawa amekuwa kimya kutoa maoni yake kuhusu masuala kama vile makasisi wanawake na mambo ya namna hiyo.