Papa Leo XIV alaani unyonyaji, masikini kutengwa

Roma. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Leo wa XIV, amelaani unyonyaji wa watu maskini, huku akitoa wito wa umoja ndani na nje ya kanisa.

Amebainisha hayo leo Mei 18, 2025 wakati wa misa maalumu ya kusimikwa kuwa kiongozi wa kanisa hilo baada ya kuchaguliwa Mei 8, 2025 na makardinali 133 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Misa hiyo imefanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kuhudhuriwa na viongozi wa dunia, familia za kifalme na makumi ya maelfu ya waumini.

Papa huyo wa 267, aliwasili mjini Vatican kwa kutumia gari la kipapa (popemobile) na kupokewa kwa shangwe na vifijo na umati wa watu alipokuwa akizunguka kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kwa kutumia gari hilo maalumu.

Wakati akizunguka na gari lake, Papa Leo, ambaye kwa mara ya kwanza anatoka Marekani, alionekana kusimama kwa muda mfupi na kumbusu mtoto.

Sauti za pamoja zilizosema “Viva il Papa” zilisikika mara kadhaa, zikifuatiwa na nderemo na makofi mengi alipokuwa akiingia uwanjani kwa ajili ya kuanza kwa misa hiyo maalumu.

Usalama ulikuwa wa hali ya juu katika tukio hilo, na mamlaka za jiji la Roma zilisema Ijumaa iliyopita kwamba walikuwa wamefunga eneo lenye uwezo wa kuhifadhi hadi watu 250,000.

Miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo ya saa mbili leo Jumapili ni Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky na Rais wa Peru, Dina Boluarte, kiongozi wa nchi ambayo Papa Leo alihudumu kama mmisionari na askofu kwa miongo kadhaa.

Mataifa kutoka kote duniani yamewakilishwa, Vatican ikiwakaribisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 150 duniani.

Katika mahubiri yake, Papa Leo amesema hakuna nafasi ndani ya Kanisa Katoliki kwa “propaganda za kidini” au mbio za madaraka, bali ametoa wito wa umoja.

Amelaani, pia, mfumo wa kiuchumi unaotumia rasilimali za dunia kupita kiasi na kuwaweka pembeni walio maskini zaidi.

Papa Leo ameonyesha unyenyekevu sawa na ule wa mtangulizi wake, Papa Fransisco, akisema hakuchaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki kwa sababu ya sifa zake binafsi, bali anauchukua wadhifa huo kama ndugu, anayetaka kuwa mtumishi wa imani na furaha ya wote.

Ingawa Papa Leo alichaguliwa Mei 8, 2025, mwanzo rasmi wa upapa wake umeanza leo Mei 18, 2025 na kikao chake cha kwanza cha hadhara na umma kimepangwa kufanyika Mei 21, 2025.

Alama za madaraka

Misa ya leo Mei 18, 2025 ilikuwa imejaa ishara nyingi, ikiwemo kumvisha Papa Leo alama rasmi za ofisi kama vile: Pallium (vazi la sufi ya kondoo linaloashiria huduma yake ya kichungaji kwa Kanisa na nafasi yake kama mchungaji wa kondoo wake).

Pia, amevishwa pete ya mvuvi ikiwa ni ishara ya mamlaka ya Papa kama mrithi wa Mtakatifu Petro, aliyekuwa mvuvi kwa taaluma na ambaye Wakatoliki humchukulia kama papa wa kwanza.

Makofi mengi yalisikika wakati Papa akikabidhiwa vazi na kulivaa kwa mara ya kwanza katika misa hiyo.

Vatican imetoa maelezo kuhusu pete hiyo: ina picha ya Mtakatifu Petro kwenye eneo la nje, huku maandishi ya “Leo XIV” na nembo ya Papa yakiwa yamechorwa kwa ndani.

Maaskofu wote huvaa pete kuonyesha uhusiano wao na makanisa wanayoyaongoza, lakini pete ya Papa kama Askofu wa Roma inaashiria ndoa yake ya kiroho na kanisa lote.

Wakati pete hiyo ilipokabidhiwa, Papa Leo alionekana kuguswa sana na tukio hilo, akaitazama kwa muda kidole chake cha pete kwa unyenyekevu.

Masomo ya maandiko matakatifu wakati wa misa hiyo yalijikita kwa Mtakatifu Petro na kifungu muhimu kutoka Injili ya Yohane, maandiko yanayoonekana kuwa msingi wa huduma ya kipapa kama mrithi wa Petro.

Mabadiliko sherehe za Kipapa

Sherehe za kusimikwa kwa mapapa zimebadilika kwa miaka mingi. Kwa karne nyingi, sherehe hizo zilihusisha pia kutawazwa kwa taji, ambapo taji ya kipapa iliwekwa juu ya kichwa cha papa mpya.

Kutawazwa kwa namna hiyo mara ya mwisho kulifanyika mwaka 1963 kwa Papa Paulo VI. Hata hivyo, baadaye aliamua kuuza taji hilo na kupeleka mapato kwa mashirika ya misaada.

Wakatoliki wa Marekani walilinunua taji hilo, ambalo sasa limehifadhiwa na linaonyeshwa katika Basilika ya Kitaifa ya Kumbukumbu Takatifu ya Mama Yetu wa Misaada huko Washington, D.C.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *