
Rome. Papa Francis amewashukuru waumini na wasio waumini wa Kanisa Katoliki kwa kuendelea kumuombea afya njema tangu alipolazwa Februari 14,2025.
Papa Francis (88) amelazwa katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma akisumbuliwa na maradhi kwenye mfumo wa upumuaji. maradhi hayo yamesababisha asionekane hadharani kwa zaidi ya wiki tatu.
Katika ujumbe wake wa sauti (audio) kwa waumini alioutoa jana jioni Machi 6,2025, Papa Francis, amesikika akizungumza japo kwa shida. Kauli yake hiyo imeelezwa kuwarejeshea matumaini waumini wa kanisa hilo ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi kumuombea apone.
Hotuba ya Papa Francis, iliyorekodiwa na kutangazwa kupitia vipaza sauti katika uwanja wa Mtakatifu Petro huko Vatican kabla ya sala ya Rozari ya jana jioni, ilikuwa mara ya kwanza kwa wafuasi wake kusikia sauti yake tangu alazwe hospitalini takriban wiki tatu zilizopita.
“Nawashukuru kwa dhati kwa maombi yenu kwa ajili ya afya yangu kutoka uwanjani nami nawasikiliza kutokea hapa hospitalini. Mungu awabariki na Bikira Maria awalinde. Asanteni,” alisema Papa Francis, akizungumza taratibu kwa lugha ya Kihispania ambayo ni lugha yake ya asili.
Baada ya kusikika sauti ya kiongozi huyo wa kiroho, umati uliokuwa kwenye uwanja huo ulilipuka kwa kupiga makofi kuashiria furaha ya kumsikia tena kiongozo wao huyo aliyetangazwa kuwa na hali mbaya ya kiafya mara kwa mara akiwa hospitalini hapo.
Ingawa Papa ametoa jumbe zilizoandikwa kutoka hospitalini na Vatican imetoa taarifa mbili kwa siku kuhusu hali yake.
Bado hajatoa ujumbe wa video unaomuonyesha mwonekano wake tangu Februari 14 alipolazwa hospitalini akipambana na changamoto kwenye mapafu ikiwa ni pamoja na homa ya mapafu (bronchitis) na nimonia kwenye mapafu yote (double pneumonia).
Hii ni mara ya nne kwa Papa Francis kulazwa hospitalini tangu ashike wadhifa huo na sasa hivi ndiyo amekaa hospitalini kwa muda mrefu zaidi katika historia ya kuugua kwa kiongozi huyo tangu awe Papa mwaka 2013.
Papa Francis amekuwa na matatizo ya mapafu kwa sehemu kubwa ya maisha yake. Akiwa kijana aliwahi kuugua nimonia kali iliyosababisha sehemu ya pafu lake moja kuondolewa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Vatican, madaktari wanaomtibu wamesema hali ya kiafya ya Papa Francis inaendelea kufuatiliwa kwa ukaribu baada ya kukumbwa na changamoto ya upumuaji mara kadhaa hususan Jumatatu iliyopita, ingawa hali yake imeimarika tangu wakati huo.
Vatican imeripoti leo asubuhi kuwa Papa Francis hajakumbana na changamoto tena ya kwenye mfumo wa upumuaji inayotishia maisha yake na hana homa.
“Anaendelea na tiba ya kupumua na mazoezi ya viungo na alikuwa na siku yenye shughuli nyingi Alhamisi, akifanya kazi kadhaa na kupokea Ekaristi kabla ya chakula cha mchana,” imesema Vatican.
Ratiba ya kiongozi huyo kutoka Argentina imepunguzwa ili kumpa nafasi ya kufuatilia matibabu yake kwa karibu.
Kiongozi huyo hakuhudhuria ibada ya Jumatano ya Majivu, ambayo huashiria mwanzo wa Kwaresma, kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka 12 ya kuhudumu kwenye wadhifa huo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.