Panyaroad aliyeitawala dunia kimuziki

Marekani. Katika ya mdororo wa uchumi. Anguko la viwanda lililosababisha Great Depression. Biashara za magendo zikitawala. Magenge ya kimafia yakiwa fasheni ya mitaa. Ni wakati huo alizaliwa mtoto.

Chicago, Illinois, maskani ya maharamia wa Chicago Outfit, chini ya underworld chief, Al Capone a.k.a Scarface, ndipo mtoto alikulia. Baba fundi seremala, mama ofisa wa benki, lakini akapata ugonjwa wa akili. Akapelekwa taasisi ya watu wa magonjwa ya akili.

Baba, fundi seremala, akaajiriwa na genge hatari la Jones Boys. Ni Zama za Adui wa Umma (Public Enemy Era). Mtoto kila alipogeuka alikutana na mitikasi ya kigangsta. Unatamani kuwa unachoona. Mtoto akaapa kuwa gangsta. Yeye na wenzake wakawa panya wa mtaani. Road rats. Panyaroad!

Mtoto akiwa na umri wa miaka saba, mawindoni na mdogo wake, walikutana na panyaroad wengine, wakamvunja kidole. Wakampasua usoni. Baba yao akaona Chicago siyo salama, akawabeba wanaye, wakahamia jimbo la Washington.

Mtoto ameshakuwa panyaroad. Akiwa Washington State, siku moja usiku, yeye na wenzake walivunja jengo la kituo cha kijamii ili kutafuta chakula. Walipoingia ndani, mtoto aliona piano. Akaigusa, ikatoa mlio. Akabonyeza tena na tena. Ule mlio ukaakisi ndani kabisa ya moyo. Kila seli ya mwili ilimwambia: “Hiki ndiyo kitu chako.”

Quincy Delight Jones Jr, mtayarisha muziki mwenye kiti cha peke yake. Hafananishwi, halinganishwi. Hiyo ni hadithi, jinsi piano ilivyobadili mtazamo wa maisha yake. Ikafuta fikra za ugangsta, akaanza kufuata ndoto za kuwa mwanasayansi ndani ya sanaa ya muziki.

Akiwa shule, alianza kujifunza kupiga vyombo mbalimbali vya muziki. Trumpet ilimteka, akawa master wa kuipuliza. Katika umri wa miaka 13, Quincy Jones “Q”, angekwenda nightclubs na kupuliza trumpet kwa umahiri kabisa.

Alipokuwa na umri wa miaka 14, alimvutia mwanamuziki Billie Holiday, akamchukua kama trumpeter wake. Akiendelea kusaka mlango wa kutokea, Q alifanya kazi na wanamuziki Count Basie na Clark Terry, kisha kupitia gwiji wa trumpet, Dizzy Gillespie, aliweza kuonekana kwenye show ya kwanza ya televisheni, ya mfalme wa Rock and Roll, Elvis Presley.

Uwezo wa Q, ulimshawishi galacha Lionel Hampton, akamjumuisha kwenye bendi yake katika ziara ya kuizunguka dunia. Ndani ya bendi ya Hampton, Q alionesha umahiri katika upangiliaji wa muziki kwenye nyimbo. Alihitajika zaidi.

Q akiwa Ulaya kwenye ziara ya bendi ya Hampton, alijikuta ametengeneza deni la dola 145,000. Aliamua kuomba kazi studio ya Mercury Records. Akawa Mmarekani mweusi wa kwanza kuwa makamu wa rais kwenye label kubwa ya muziki Marekani. Hiyo ilikuwa mwaka 1961.

Mtayarishaji wa muziki wa Marekani, Quincy Jones akiwa amebeba tuzo za Grammy enzi za uhai wake.

Ndani ya Mercury Records, kila kitu kilifunguka kwa kasi kwenye maisha ya Q. Pigo lililogonga platinum, “My Party”, wimbo wa Lesley Gore, halafu akashusha albamu yake “Big Band Bossa Nova”. Hapo imeshagonga mwaka 1962.

Kazi za Q zilimtikisa the grand master wa muziki, Frank Sinatra, akampigia simu, kisha wakakubaliana watengeneze albamu mbili. Upacha wa hali ya juu uliibuka baina ya Q na Sinatra. Maajabu ya Q yaliendelea kwenye kazi za Aretha Franklin, Louis Armstrong na Sammy Davis Jr, halafu albamu yake ya pili, “Body Heat”, ikitinga 10 bora Marekani.

Mwaka 1978, Q alifanya kazi na kijana aliyekuwa na umri wa miaka 19. Jina la kijana huyo ni Michael Jackson. Alikuwa prodyuza wa wimbo “Ease on Down the Road”, ambao Michael “MJ” aliimba na Diana Ross.

Q ndiye alitengeneza soundtracks zote za musical film “The Wiz”, ambayo MJ ni actor, Diana Ross ni actress. MJ pia ameimba “You Can’t Win” ndani ya movie hiyo. Kipindi hicho, MJ baada ya kuwa star tangu akiwa mtoto, akiwa na music group la familia yake, “The Jackson 5”, alitamani kutoka kivyake.

Awali, nje ya The Jackson 5 au The Jacksons, MJ alikuwa ameshatoa albamu nne; “Got To Be The” ambayo MJ aliitoa akiwa na umri wa miaka 13, “Ben”, aliyotoa siku 25 kabla hajatimiza umri wa miaka 14, “Music & Me” akiwa na miaka 14, na “Forever, Michael” alipokuwa na miaka 16. Sasa MJ alitaka kutoka kiutu-uzima, akakutana Quincy “Q”.

Kupitia kazi walizofanya pamoja kwenye The Wiz, Q aliouona haraka ukuu wa MJ, akawekeza muda, nishati na maarifa yake yote kwa kijana huyo. Akamfunda kimuziki, halafu akamtengenezea MJ albamu yake ya tano akiwa solo, nje ya The Jackson 5, “Off The Wall”, iliyotoka Agosti 10, 1979.

Off The Wall iligonga mauzo triple diamond (30 platinum). Zaidi ya nakala 31 milioni ziliuzwa. Kisha, albamu balaa la dunia, “Thriller”, iliyotoka Novemba 29, 1982, ambayo mauzo yake kwa jumla yanakadiriwa kufika nakala 200 milioni. Thriller ni albamu inayotajwa kuwa bora kuwahi kutokea duniani.

Albamu ya tatu ya MJ kufanya na Q ni “Bad”, iliyotoka Agosti 31, 1987. Kwa MJ ni albamu ya saba. Zaidi ya nakala milioni 100 ziliuzwa kutokana na santuri hiyo. Ndiyo maana MJ ni mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa mno duniani. Albamu tatu ambazo MJ alifanya na Q zilimpaisha kwenye kilele kisichofikika.

Kutoka kazi za Sinatra hadi MJ, kisha project ya hisani, “We Are The World”, kusaidia janga la ukame Ethiopia mwaka 1985, mauzo yake yakikadiriwa kuzidi nakala milioni 10. Hiyo ndiyo sababu Q ni prodyuza ambaye nyimbo zake zimenunuliwa kuliko yeyote.

Tangu miaka ya 1960 mpaka 1990, ukiongeza kazi za genius wa muziki, Ray Charles, jumlisha uhusika wa Q kwenye filamu na vipindi vya televisheni, midundo yake,  hasa “Soul Bossa Nova”,  ilivyopamba movie kama soundtracks, jibu ni dhahiri kwamba Quincy ni mtu wa kazi zenye matokeo makubwa.
Kuanzia miaka ya 1960 mpaka 2000, ilikuwa fasheni kwa filamu na vipindi vya televisheni Marekani kuwekewa muziki na Q “The Composer”. Q ni nembo ya entertainment Marekani. Kwa jumuiya ya muziki wa Kimarekani hasa black American community, Q ni statesman. Maisha yake ni mstari wa hamasa kwa kila mwenye ndoto ya sanaa.

Q the warrior
Quincy ameishi duniani miaka 91, miezi saba na siku 20. Amini kuwa miaka yake 50 ya baadaye, ni ushuhuda kuhusu Mungu anavyoweza kumbakisha mtu hai ili aitende kazi ya wito.

Mtayarishaji wa muziki wa Marekani, Quincy Jones akiwa aliyekuwa msanii nguli duniani Michael Jackson katika moja ya tuzo za Grammy. Picha na Mtandao

Pengine Q angefariki dunia kabla ya kukutana na Michael Jackson. Ilikuwa mwaka 1974, Q alikuwa na umri wa miaka 41. Mshipa wake wa damu kwenye ubongo ulijaa na kuunda umbo kama puto (brain aneurysm), kisha kumwaga damu kwenye ubongo. Ulikuwa ugonjwa hatari kutokana na teknolojia ya kitabibu wakati huo.

Madaktari wakasema nafasi yake ya kuepuka kifo ni ndogo. Wakamfanyia oparesheni ya kwanza kwa takriban saa 8 (dakika 480). Wakagundua ana brain aneurysm nyingine. Madaktari wakamweleza kwamba nafasi yake ya kuishi ni moja kwa 100. Akajiandaa kuagana na ulimwengu.

Wakati huo, Q alishafanya maajabu mengi kama prodyuza na alishakaa kwenye kilele cha dunia kupitia kazi za Frank Sinatra, Dinah Washington, Aretha Franklin, Lesley Gore na wengine. Taarifa kuwa Q alikuwa kwenye siku za mwisho wa maisha yake, ziliwashitua watu wengi. Marafiki wakaona lazima wafanye tukio la kumuaga kwa heshima.

Ikaandaliwa concert baabkubwa. Ikatarajiwa hiyo ndiyo ingekuwa kumbukumbu ya mwisho ya Q, kwani baada yake asingechukua kitambo kirefu, angefariki dunia. Wanamuziki wakubwa Marekani walijitolea kutumbuiza bure kumuaga Q.

Alifanyiwa oparesheni ya pili. Ikafanikiwa. Madaktari walimwambia angeweza kuendelea kuishi, lakini walimpa masharti ya kutopiliza tena trumpet. Baada ya kutoka hospitali, wakaulizana, sherehe ya kumuaga ifutwe? Wakasema “big no”, party liendelee kusherekea Q kutoboa.

Madaktari walipojua Q angefanyiwa sherehe, walimtahadharisha asipandwe mizuka sana, ingekuwa hatari kwake. Unawezaje kutopandisha mizuka wakati unashuhudia magwiji, Richard Pryor, Marvin Gaye, Sarah Vaughan na Sidney Poitier, wakiimba nyimbo za kukukweza? Q mizuka ilipanda sana na hakuna alitokea.

Aliambiwa asipulize tena trumpet, akapuliza. Ujeuri huo kwa afya yake ndiyo matunda ya “Thriller”, “We are the World”, soundtrack ya filamu ya “The Color Purple” na kazi zake zote alizofanya baada ya mwaka 1974. Hakuna kilichotokea, na aliishi miaka 50 baada ya brain aneurysm.

Q, alizaliwa Machi 14, 1933 na kufariki dunia Novemba 3, 2024. Maisha yake, kwa tafsiri ya mamlaka laini (soft power), Q aliitawala dunia kupitia mikono yake na mdomo uliopuliza trumpet. Nyimbo alizozitengeneza ziliichengua dunia.

Aliitawala sayari kupitia albamu tatu za MJ, “Off The Wall”, “Thriller” na “Bad”. Akaifanya dunia iwehuke kwa nyimbo za Frank Sinatra. Akauimbisha ulimwengu “We Are The World”. Hiyo ndiyo nguvu ya soft power. Kwa kipaji chake, maarifa na uthubutu, alijiundia kilele cha peke yake kimuziki na sanaa kwa jumla.

Q alikuwa mwanaharakati. Alijengwa na shujaa Martin Luther King Jr, walipokutana mwaka 1955. Ukiacha ushiriki wake wa kutengeneza nyimbo za Hip Hop na hamasa yake iliyowajenga watayarishaji mahiri wa Hip Hop, akiwemo Dr Dre, mwaka 1995, aliandaa kongamano aliloliita “Quincy Jones Hip-Hop Symposium”, ambalo maudhui yake yalikuwa kuifunda jumuiya ya Hip Hop kufanya muziki bila vurugu.

Kilikuwa kipindi ambacho ulimwengu wa Hip Hop ulitawaliwa na vurugu, hasa matumizi ya bunduki. Q akiwahutubia wana-Hip Hop waliohudhuria, aliwaambia: “Ningetamani sana kuona ninyi vijana mnaisha angalau kufikia umri wangu.” Wakati huo Q alikuwa na umri wa miaka 62.

Q, alishinda tuzo 28 za Grammy, alinyakua Primetime Emmys, Tony na nyingine nyingi. Mwaka 2011, Q alitunukiwa Medali ya Taifa ya Sanaa, kutoka Ikulu ya Marekani, White House. Ni Mmarekani mweusi wa kwanza kuteuliwa kuwania Tuzo za Academy, kupitia wimbo “The Eyes of Love”, ambao ni soundtrack ya filamu “Banning”, iliyotoka mwaka 1967.

Kazi yake ya kimuziki kwenye filamu “In Cold Blood” ya mwaka 1967, ilimfanya aingie kwenye vipengele viwili vya Tuzo za Academy, akiweka rekodi ya kuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kufanya hivyo. Halafu mwaka 1971, Q, alikuwa Mmarekani mweusi wa kwanza kuwa mwongozaji wa muziki kwenye Tuzo za Academy.

Mwaka 1995, Q alikabidhiwa Tuzo ya Academy ya matendo bora ya kibinadamu, inayoitwa Jean Hersholt Humanitarian Award. Mwaka 1983, Chuo cha Muziki cha Berklee, kilichopo Boston, Massachusetts, kilimtunuku shahada ya udaktari wa heshima kwenye muziki. Unapaswa kumwita Dk Quincy Jones au simply Dk Q.

Los Angeles, California, kuna shule ya msingi inaitwa Quincy Jones, kwa heshima ya Q. Ni mmoja kati ya watu 15 pekee kutunukiwa tuzo ya Grammy Legend, ambayo ilianzishwa mwaka 1958. Mwaka 2013, Time Magazine walimtaja Q katika orodha ya watu 10 wenye umri zaidi ya miaka 80, waliokuwa na ushawishi zaidi ulimwenguni.

Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton, aliandika kuhusu Q kuwa “aliibadilisha sura ya tasnia ya muziki jumla”, wakati Rais wa 44, Barack Obama, aliandika: “Alijenga wasifu wake kikazi kutoka mitaa ya Chicago hadi kwenye vilevile vya Hollywood.”Mpaka anafariki dunia, Q alikuwa na utajiri unaofikia dola 500 milioni (Sh1.34 trilioni). 
Katika maisha yake, alifunga ndoa na wanawake watatu tofauti na kutalikiana nao wote. Alijaliwa kupata watoto saba.