Pamba yaishusha Kagera, Yanga yaiadhibu Namungo

Dar es Salaam. Wakati Yanga ikifanikiwa kuongeze gepu la pointi hadi kufikia nne dhidi ya Simba, hatimaye Pamba Jiji imeishusha rasmi Kagera Sugar kutoka Ligi Kuu hadi Championship.

Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo na kufikisha pointi 73 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiiacha Simba ikiwa na pointi 69 na mchezo mmoja mkononi, huku Pamba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KenGold ambayo imeshashuka daraja, na hivyo kuungana na Kagera Sugar ambayo ilipoteza mchezo juzi kwa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa.

Kitendo cha Pamba ambayo ilikuwa kwenye nafasi mbaya kupata ushindi huo kimeifanya timu hiyo kusogea hadi nafasi ya 11 ikiwa na pointi 30 kwenye msimamo, huku Kagera ikibaki nafasi ya 14 na pointi 22 ikibakiza michezo miwili tu ili kumaliza msimu.

Wachezaji wa Kagera Sugar. Picha na Kagera Sugar

Tofauti ya Kagera na Fountain Gate ambayo ipo nafasi ya 14 ikiwa kwenye mstari wa kucheza ‘play off’ ni pointi saba, hivyo ni rasmi timu hiyo imeshuka daraja baada ya kukaa kwenye Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 mfululizo.

Kagera imefanikiwa kufunga 22 tu msimu huu hadi sasa, huku yenyewe ikiruhusu 40, imeshinda michezo mitano tu, imepoteza 16 na kutoka sare saba tu.

JKT yaiweka pabaya Fountain

JKT Tanzania imezidi kuiweka pabaya Fountain Gate katika msimamo wa Ligi Kuu Bara huku zikisalia mechi mbili kumaliza msimu huu.

Hiyo ni baada ya JKT Tanzania kuutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani wa Meja Jenerali Isamuhyo kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo uliofanyika mapema leo.

Kipigo hicho kimeifanya Fountain Gate kusalia na pointi 29 ikiendelea kuwepo kwenye mstari wa kucheza mechi za mtoano play off kupambania kutoshuka daraja, huku JKT Tanzania ikihitaji pointi moja pekee katika mechi mbili zilizobaki ili kuwa salama zaidi. Kwa sasa ina pointi 35 baada ya mechi 28.

Fountain Gate yenye maskani yake Manyara, mechi mbili za kupambana itoke nafasi iliyopo sasa itacheza dhidi ya Coastal Union (Juni 18) ugenini na Azam (Juni 22) nyumbani ambapo inahitaji kushinda zote, huku ikiziombea mabaya Pamba Jiji, KMC na Tanzania Prisons.

Katika mchezo wa huo ambao Fountain ilipoteza, JKT Tanzania ilikuwa na siku nzuri kwani hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mohamed Bakari dakika ya 7 na Shiza Kichuya dakika ya 45. Kipindi cha pili, JKT Tanzania ikaongeza bao la tatu dakika ya 59 mfungaji akiwa Edward Songo.

Mfungaji wa bao pekee la Fountain Gate ni William Edgar dakika ya 87 ambalo limemfanya mshambuliaji huyo kumaliza ukame wa mabao baada ya kutocheka na nyavu kwa takribani siku 146 kwani kabla ya hapo mara ya mwisho alifunga Desemba 13, 2024 wakati Fountain Gate ikishnda 3-2 dhidi ya Coastal Union.

Upekee wa bao hilo lililoondoa ukame kwa Edgar ni namna ambavyo lilipatikana kwani mshambuliaji huyo mara ya mwisho alifunga tarehe 13, kisha akafunga tena tarehe kama hiyo japo mwezi na mwaka tofauti.

Yanga mambo safi

Ikiendeleza wimbi la ushindi mbele ya mashabiki wachache waliojitokeza kwenye Uwanja wa KMC, Yanga iliendelea kuiweka pabaya Namungo baada ya kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Stephen Aziz Ki katika dakika ya 27 kwa shuti kali, akipokea pasi ya Maxi Nzengeli, huku bao lingine likifungwa na Prince Dube ambaye alipata pasi kutoka kwa Kibwana Shomary na kufunga kwa ustadi mkubwa katika dakika ya 30 ya mchezo huo.

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la mshambuliaji wao, Prince Dube katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo leo Mei 13, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex. Picha na Michael Matemanga

Kipindi cha pili,  Yanga ilipunguza kasi, lakini ikijipatia bao la tatu katika dakika ya 75 kupitia kwa Maxi ambaye alifanikiwa kuonyesha kiwango kizuri kwenye mchezo huu.

Huu ni ushindi wa 24 kwa Yanga msimu huu baada ya kucheza mechi 27, ikipoteza mbili na kutoka  sare moja, lakini timu hiyo imeendelea kukaa kileleni na pointi 73, ikifunga mabao 71 na kuruhusu kumi tu, ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi kwenye ligi kwa sasa na kuruhusu machache.

Bao la Dube ni la 13 kwake msimu huu, akiwa ndiye kinara kwa upande wa Yanga, lakini akiwa tofauti ya mabao mawili na kinara Jean Charles Ahoua mwenye mabao 15, huku Aziz KI akifanikiwa kufunga bao lake la tisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *