Pamba mambo bado, yalazimishwa sare na Namungo nyumbani

Safari ya Pamba Jiji kutoka nafasi za chini na kusogea juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara bado haijawa rahisi, kwani leo imeshindwa kufurukuta nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Namungo FC.

Pamba Jiji imepata matokeo hayo leo Aprili 3, 2025 katika mchezo wa mzunguko wa 24 wa ligi hiyo ambao umepigwa kuanzia saa 8:00 mchana.

Baada ya matokeo hayo, Pamba Jiji imefikisha alama 23 na kusalia katika nafasi ya 13 baada ya mechi 24 ikishinda tano, sare nane na kupoteza 11 huku ikifunga mabao 15 na kuruhusu 26. Namungo nayo imebaki kwenye nafasi ya 12 na alama zake 24 ikishinda mechi sita, sare sita na kupoteza 12 huku ikifunga mabao 17 na kuruhusu 29.

Hiyo ni sare ya tano kwa Pamba Jiji katika uwanja wake wa nyumbani msimu huu ikiwemo dhidi ya Dodoma Jiji (0-0), Tanzania Prisons (0-0), Kagera Sugar (1-1) na Mashujaa FC (2-2), huku ikishinda mechi tatu pekee dimbani hapo dhidi ya Azam FC (1-0), Ken Gold (1-0) na Costal Union (2-0).

Mchezo huo ambao umeanza kwa tahadhari timu hizo zikishambuliana kwa zamu, Namungo ndiyo wamekuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 21 likifungwa na Jacob Masawe aliyemalizia krosi ya upande wa kushoto iliyopigwa na Antony Mlingo.

Baada ya bao hilo, Pamba imeshtuka na kuanza mashambulizi ya kasi langoni kwa Namungo na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 38 kupitia kwa Abdoulaye Yonta Camara baada ya mabeki wa Namungo kushindwa kuokoa mpira mrefu ndipo kiungo huyo mshambuliaji akapiga shuti la kudonoa ambalo kipa, Jonathan Nahimana aliugusa kidogo lakini ukajaa nyavuni.

Dakika 45 za kwanza hazikuwa na mbabe kwani timu hizo zimekwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa kwa kufungana bao 1-1, huku kukiwa na kosakosa kibao.

Miongoni mwa hizo ni ile ya dakika ya 12, kiungo wa Pamba, Samuel Antwi alifumua shuti kali lakini likapaa juu kidogo ya lango. Dakika ya 26 winga, Zabona Mayombya wa Pamba Jiji alipiga shuti ambalo lilipanguliwa na kipa na kuwa kona.

Dakika ya 45, mshambuliaji wa Namungo, Fabrice Ngoy anafanya shambulizi na kufumua shuti ambalo linadakwa na kipa wa Pamba, Mohamed Camara.

Kipindi cha pili kimeanza kwa mabadiliko ya wachezaji, ambapo Pamba Jiji ilimpumzisha beki, Samson Madeleke na kuingia Christopher Oruchum ambaye baada ya mchezo huo ametangazwa kuwa nyota wa mchezo (MVP).

Pamba imefanya mabadiliko mengine dakika ya 72 ikiwatoa Deus Kaseke na Zabona Mayombya na kuingia John Nakibinge na ShassirI Nahimana, huku Namungo ikimuingiza Emmanuel Charles kuchukua nafasi ya Jacob Masawe aliyeshindwa kuendelea na mchezo baada ya kupata majeraha dakika ya 83.

Mabadiliko mengine yalikuwa dakika ya 84, Pamba ikiwatoa Yonta Camara na James Mwashingwa na nafasi zao kuchukuliwa na Allain Mukeya na Bakari Francois, huku Namungo ikiwatoa Najim Mussa na Fabrice Ngoy na kuingia Ayoub Semtawa na Pius Buswita.

Licha ya mabadiliko hayo ya kuboresha vikosi lakini mchezo haukuwa na mabadiliko makubwa ambapo hadi dakika 90 zinakamilika Pamba Jiji 1-1 Namungo.

Baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ amesema mchezo haukuwa bora upande wao kwani hawakucheza vizuri na kushindwa kuondoka na alama tatu nyumbani, huku akiwatia moyo mashabiki kutokata tamaa kwani bado wana nafasi ya kufanya vizuri.

“Mechi haikuwa vizuri kwa upande wetu tumeshindwa kufuata maelekezo vizuri na kupoteza nafasi kadhaa lakini tuna mechi sita zikiwemo nne za nyumbani ambazo tutarekebisha makosa na kufanya vizuri,” amesema Minziro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *