Palestina yatoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni kuhusu kitongoji cha al-Bastan

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetahadharisha kuhuusu uharibifu huo kamili wa kitongoji cha al-Bastan cha Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na utawala pandikizi wa Israel na hasa baada ya Wapalestina 1,500 kulazimishwa kuyahama makaazi yao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetangaza katika taarifa yake kwamba, kuharibiwa kitongoji cha al-Bastan katika mji wa Selwan wa Quds Tukufu ni sehemu ya sera ya ubaguzi  wa rangi wa  utawala huo bandia unaoikalia kwa mabavu Palestina.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, malengo makuu kabisa  ya vitendo hivyo ni kukiangamiza kabisa kitongoji hicho na kuwahamisha Wapalestina na kuwaweka walowezi wa Kizayuni.

Inapaswa kutaja hapa kuwa, mabuldoza ya utawala pandikizi wa Israel yalifanya unyama huo siku ya Jumatano.

Hayo yamejiri huku walowezi wa Kizayuni wakichoma moto baadhi ya magari ya Wapalestina katika kitongoji cha  Sheikh Jarrah cha mji wa Quds Mashariki na kukimbia.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeitaka jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yao ya kisheria na kimaadili ili kukomesha jinai hizo za kinyama zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel.