
Clement Mzize ndiyo jina ambalo linatajwa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na kiwango ambacho amefanikiwa kukionyesha kwenye michezo kadhaa aliyocheza msimu huu.
Huyu ndiye mshambuliaji mzawa anayeongoza kwa mabao kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara akiwa amefanikiwa kufunga mara tisa na ni dhahiri kuwa anaamini kuwa atakwenda na kasi hiyo hadi mwishoni mwa msimu.
Mzize aliyejiunga na Yanga akitokea kwenye timu ya vijana ndiye mchezaji pekee kwa kizazi hiki ambaye ametoka moja kwa moja kwenye kikosi hicho na kuonyesha kiwango bora kwenye ligi na michuano ya kimataifa.
Nyota huyo wa Yanga alifikisha mabao hayo baada ya majuzi Jumatano kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya KenGold na kufikisha idadi hiyo akiwafunika mastaa wa kigeni anaocheza kwenye ligi hapa nchini.
Ni kawaida kwa timu za Simba, Yanga na Azam kutumia kitita kikubwa cha fedha kwa ajili ya usajili wa wachezaji kutoka mataifa makubwa ya soka Afrika, lakini kupitia Mzize ni picha kwamba wapo wengi zaidi huko mtaani.
Ni ukweli usiofichika kuwa Mzize hakudumu kwenye timu ya vijana kwa zaidi ya mwaka mmoja na kupandishwa kwenye timu ya wakubwa baada ya Mwinyi Zahera kuona kuwa alikuwa na kipaji kinachostahili kucheza timu ya wakubwa.
Lakini jambo la kuonyesha utofauti kwa Mzize ni kitendo cha kuelezwa kuwa anatakiwa na Montpellier ya Ufaransa tangu akiwa timu ya vijana baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kwenye mashindano ya ya vijana yaliyokuwa yanajulikana kama Cambiasso ambayo Yanga ilishiriki.
Ukweli ni kwamba kipindi hiki Yanga hawakuwa na fedha kama ilivyo sasa, lakini utulivu wao kwa Mzize ulikuwa wa kiwango cha juu sana pamoja na kwamba walikuwa wanatambua kuwa wangepata fedha nyingi.
“Siyo kweli kwamba Zahera ndiye alimuona Mzize hapana, ngoja nikueleze vizuri Mzize alishiriki mashindano ya vijana akafanya vizuri na mashabiki wakawa wanampenda sana, lakini baadaye akaja akashiriki yale ambayo yaliandaliwa na Cambiasso ambayo Montpellier walikuwa waalikwa, huku Mzize alionyesha ubora wa juu sana.
“Baada ya mashindano hayo hawa jamaa walileta barua ya kumtaka Mzize akapewa Zahera ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi kama sikosei baada ya hapo ikaelezwa kwamba asiuzwe kwanza ndiyo akapandishwa kwa wakubwa na kuwa na ubora huu,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka Yanga.
Mzize ambaye amekuwa hatari kwenye mguu wa kulia kuonyesha kuwa ni mchezaji mahiri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika amefunga mabao matano msimu huu ambayo ni wachezaji wachache sana wamefunga barani Afrika kwa sasa.
Jambo pekee la kutazama kwa Mzize ni kwamba yenye ni mwakilishi wa kina Mzize wengi waliopo huko mtaani wakicheza, kuna wakati kwa upeo mdogo wa soka unaweza kupita mtaani ukakuta vijana wanacheza mechi na kiwango kinachoonyeshwa na baadhi ya wachezaji unaona kuwa walistahili kuwa Ligi Kuu na wale waliopo Ligi Kuu walitakiwa kucheza kule.
Tazama pale alipokuwa anacheza Mzize Iringa, mara nyingi kama alikuwa bora basi kuna wengine walikuwa bora kama yeye au zaidi, lakini nani amevivika kengele na kwenda tena pale, kama alipatikana yeye basi kuna kina Juma, Abdallah Peter na Issa wengine wengi huko mtaani Iringa, Mbeya, Songea na hata Kigoma.
Ni mazoea kwa mastaa wakubwa kuja hapa nchini na kusema kuwa Tanzania imejaliwa vipaji vikubwa vya soka, ndiyo kwa hiki ambacho anatuonyesha Mzize ni sahihi kukubaliana na kauli hizo, kiwango anachotajwa kununuliwa nacho kwa sasa hata Aziz Ki hafikii. Lakini kuna wengine wanasema ni kwa kuwa ni mshambuliaji ndiyo ni kweli ni mshambuliaji lakini waliomuona huku waliona washambuliaji karibu Afrika nzima na huyu akawa bora.
Ni wakati wa sisi kama nchi kuamka na kuachana na kauli kuwa Tanzania hakuna washambuliaji, tuende huko mikoani kwa mkakati maalumu kuhakikisha kuwa tunakuwa na kila Mzize wengine watano au sita kabla ya fainali za Kombe la Mataifa Afrika 2027 kwenye benchi la Taifa Stars kwani watu hawataki bilioni tatu kwa biashara ya soka.