
YANGA imesharejea jijini Dar es Salaam ikitokea Mwanza ilipoenda kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji wao, Pamba Jiji katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, huku ikishuhudiwa kiungo mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Pacome Zouzoua akikosekana hata benchi.
Pacome alikosekana katika mchezo huo kwa kilichoelezwa kukwepa mtego wa kulikosa pambano la Dabi ya Kariakoo, kwani alikuwa ana kadi mbili za njano, hivyo kama angepewa katika mchezo huo huenda angelikosa pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka.
Wakati siku zimesalia siku chache kabla ya pambano hilo, gari la kiungo huyo raia wa Ivory Coast limeonekana kuwaka kutokana na kiwango cha kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua namba zake kuendelea kupanda katika kikosi cha Yanga tofauti na msimu wake wa kwanza.
Ubora wa kiungo huyo msimu huu ambao ni wa pili kwake na wa mwisho kutokana na mkataba aliosaini, ameendelea kuimarika baada ya kupunguza mechi na dakika akifikia rekodi aliyoiweka Yanga msimu wake wa kwanza.
Pacome alijiunga na Yanga msimu wa 2023/24 akitokea Ligi Kuu ya Ivory Coast alikokuwa mchezaji bora wa msimu (MVP) na alikuja kuongeza nguvu katika eneo la kiungo mshambuliaji akisaidiana na Stephane Aziz Ki, kinara wa upachikaji mabao msimu huo akifunga 21.
Nyota huyo msimu wake wa kwanza Yanga alipachika mabao saba na asisti nne katika mechi 23 akitumika kwa dakika 1520.
Kwa idadi hiyo ya msimu wa kwanza, Pacome alihusika katika mabao 11 kati ya 71 yaliyofungwa na timu hiyo ikitwaa ubingwa wa tatu kwa kukusanya pointi 80 katika mechi 30.
Msimu huu katika mechi 20 alizocheza akitumika kwa dakika 1117 amevuka rekodi ya kuasisti mara sita na kufunga mabao saba kama ya msimu uliopita, ikiwa na maana hadi sasa amehusika na mabao 13 ya timu hiyo inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 58 baada ya mechi 22.
KOCHA ATIA NENO
Licha ya kuikuta timu ikiwa tayari imeanza msimu, Kocha mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi alisema hawezi kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja lakini anafurahi anaifundisha timu ambayo ina nyota wengi wenye vipaji vikubwa.
“Ukiniuliza timu yangu ni mchezaji gani ni bora kuliko wote sitaweza kukupa ufafanuzi ambao utauelewa, kwa sababu kila mchezaji ana aina yake ya uchezaji na kwa asilimia kubwa timu ina vipaji vikubwa na wanajitambua,” alisema na kuongeza;
“Kuhusu Pacome kupanda kiwango, nafikiri ni suala rahisi kwani alikuwa bado hajazoea soka la Tanzania, sasa ni msimu wake wa pili, kama ulivyosema kutokana na kipaji kikubwa alichonacho naona akifanya mambo makubwa zaidi akiendelea kuitumikia timu hii.”
MECHI ZILIZOBAKI
v Simba (nyumbani)
v Tabora United (ugenini)
v Coastal Union (nyumbani)
v Azam FC (ugenini)
v Fountain Gate (ugenini)
v Namungo (nyumbani)
v Tanzania Prisons (ugenini)
v Dodoma Jiji (nyumbani)