Pacha ya Mnunka akitaka kiatu WPL

MSHAMBULIAJI wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa amesema uwepo wa mashabiki uwanjani unawapa morali wachezaji kupambania timu hiyo.

Mkenya huyo ni kinara wa mabao WPL akiweka kambani mabao 13 kwenye mechi 10, akifuatiwa na Stumai Abdallah wa JKT Queens mwenye nayo 10.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shikangwa alisema sababu ya timu hiyo kufanya vizuri inachangiwa na uwepo wa mashabiki na viongozi jukwaani wanaokuja kuiunga mkono timu hiyo.

“Timu juzi ilishinda mabao 11-0 nashukuru Mungu nilifunga mabao manne na baadhi ya mashabiki walivutiwa na kiwango changu nikaondoka hadi na pesa kwa hiyo ni jambo linalotutia moyo ukiangalia ni ligi ambayo haikuwa inafuatiliwa na wengi,” alisema Shikangwa na kuongeza;

“Kama nilivyowahi kukuambia mimi ni mshambuliaji na kazi yangu kufunga natamani kuibuka mfungaji bora wa ligi japo najua ushindani ni mkubwa.”

Kuhusu kurejea kwa Aisha Mnunka anayecheza eneo lake alisema, “Aisha amerudi tumekuwa na kombinesheni nzuri, ni mchezaji mzuri anayetumia akili kubwa na tutafunga mabao mengi.”

Shikangwa ni msimu wa tatu kucheza Ligi ya Tanzania na msimu wake kwanza 2022/23 aliibuka kinara akiweka kambani mabao 17, 2023/24 mabao nane na msimu huu tayari kafunga 13.