
LICHA ya kupata ushindi wa kwanza katika mechi nne zilizopita za Ligi Bara na kuvunja pia rekodi ya maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jen. Isamuhyo, bado kaimu kocha mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amelia na safu ya ushambuliaji akisema inawangusha.
Singida ilipata ushindi huo wa bao 1-0 juzi na kuitibulia JKT iliyokuwa imecheza mechi 10 mfululizo zikiwamo tisa za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho nyumbani bila ya kupoteza, bao pekee likiwekwa kimiani na mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Jonathan Sowah aliyefunga dakika ya 51.
Hilo lilikuwa bao la pili kwa mchezaji huyo kutoka Ghana, baada ya awali kufunga wakati Singida ilipotoka sare ya 2-2 na Kagera Sugar na timu timu hiyo ilikuwa haijapata ushindi tangu iliposhinda 2-1 dhidi ya KenGold, mechi iliyopigwa Desemba 24 mwaka jana. Mechi tatu zilizopita ilikuwa haijashinda kwani ilifungwa 1-0 na Simba mwishoni mwa mwaka jana, kisha kutoka sare hiyo ya 2-2 na Kagera kabla ya kufungwa 2-0 na KMC na juzi ndipo ikazinduka na ushindi huo wa 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma anayekaimu nafasi hiyo baada ya Kocha Miloud Hamdi kutimkia Yanga, alisema ushindi alioupata dhidi ya JKT ilikamilisha mpango waliokuwa nao katika mchezo huo na anaamini matokeo hayo yamewarudisha mchezoni ili kukabioliana na Yanga.
Singida itakuwa wageni wa Yanga katika mechi inayochezwa Jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Ouma alisema ameangalia katika mechi mbili mfululizo timu yake imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi lakini inashindwa kutumia, huku ikikubali nyavu zao kutikiswa na wapinzani na kwenye mchezo wa juzi dhidi ya JKT Tanzania aliandaa kikosi kuto kuruhusu bao.
“Hakuna uwiano mzuri kwenye safu yangu ya ushambuliaji licha ya kuwa na wachezaji wazuri eneo hilo ukiangalia mchezo wetu na KMC tulitengeneza zaidi ya nafasi saba hatukuweza kuzitumia wapinzani waliweza kufika maeneo yetu na kutumia nafasi,” alisema na kuongeza;
“Mchezo wetu na JKT Tanzania mipango ilikuwa ni kuhakikisha haturuhusu wapinzani kutufunga na sisi tupambane kutumia nafasi tunazotengeneza hilo limefanikiwa.”
Ouma alisema anaendelea kufanyia kazi changamoto ya washambuliaji wake kukosa uelewano mzuri na anaamini akifanikiwa kwenye hilo timu yake itafanya viziri eneo hilo.
“Elvis Rupia na Jonathan Sowah wote ni wachezaji wazuri na wazoefu ni suala la muda kuwajenga ili waweze kufanya vizuri kila wanapopata nafasi ya kucheza pamoja.”
Akizungumzia mchezo wao na Yanga, Ouma alisema hatarajii urahisi kutokana na aina ya timu anayoenda kukutana nayo huku akiweka wazi kuwa matokeo waliyoyapata dhidi ya JKT Tanzania yamerudisha morali kwa wachezaji wake.
Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 37 kwenye mechi 19 walizocheza imefunga mabao 25 ikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 15 kwenye mabao ya kufungwa Sowah (2) na Rupia (8) wamehusika kwenye mabao 10.