
BAADA ya kuifanikisha Singida Black Stars kutinga fainali ya Kombe la FA kocha wa timu hiyo Mkenya, David Ouma ameweka wazi kuwa anafurahia mafaniko ya soka ambayo anaendelea kupata nchini.
Singida BS iliichapa Simba kwa mabao 3-1 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), iliyopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati, Manyara.
Ushindi huo umemtengenezea Ouma rekodi ya kuwa kocha kutoka nje ya nchi aliyefundisha timu za madaraja ya kati na kupata mafanikio makubwa kwa muda mfupi.
Ouma ambaye huu ni msimu wa pili kuwepo Bara alianza na Coastal Union msimu uliopita 2023/24 ambapo aliiwezesha timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne kwa alama 43 na kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
Akaweka rekodi ya kuwapeleka Wagosi hao kutoka Tanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa mara ya pili baada ya kupita miaka 35.
Mara ya kwanza ilikuwa ni 1989 baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Bara msimu wa 1988 kabla ya msimu uliopita Ouma kukata kiu ya Wanamangushi kwa kuwarejesha tena CAF ilikotolewa katika raundi ya awali na Bravos do Maquiz ya Angola iliyopangwa baadaye Kundi A na Simba, ambayo ilifika fainali.
Matokeo ya kufungwa jumla ya mabao 3-0 na Waangola, yalimfanya kocha huyo kufungashiwa virago hata kabla ya msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Bara kuanza ambapo alikaa kwa miezi kadhaa kisha kujiunga na Singida Black Stars kama kocha msaidizi na baaadaye kukabidhiwa timu kama kocha mkuu.
Tayari ameiwezesha Singida BS kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao 2025/26 na kuweka rekodi ya timu hiyo kufuzu michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza akiwa na uhakika wa kumaliza ndani ya nafasi Top 4 ya Ligi Kuu Bara.
Pia ameiwezesha kufika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa mara ya kwanza kwenye historia yake, ambapo timu hiyo itamenyana na Yanga katika fainali itakayopigwa kati ya Juni 26-28.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema siri ya mafanikio yake ni ushirikiano ambao amekuwa akiupata katika timu ambazo amepita ambazo pia amekuwa akikubali mawazo mapya ya nini cha kufanya ili kufanikiwa ndani ya timu.
“Napenda kumhusisha kila mtu kwenye jambo lolote kwa sababu kila mtu ana jambo la kuchangia kuhusu kitu ambacho kina faida kwa wote, kwangu kocha na timu kwa ujumla,” alisema Ouma.
Aliongeza mafanikio hayaji kirahisi ila upambane usiku na mchana.
“Mahali ambapo Singida Black Stars imefika kwa sasa usikae nyumbani njoo uishangilie timu uone vijana wenu wanavyopambana,” alisema Ouma.
Kwa sasa Singida BS inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 53 baada ya michezo 28 ikisaliwa na miwili ikitenganishwa na Azam iliyopo nafasi ya tatu kwa pointi 57.