Othman: ‘Tubaini utajiri uliopo kuendeleza visiwa Zanzibar’

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema kuwa visiwa hivyo vina utajiri mkubwa uliojificha, ambao ukitumiwa ipasavyo utavipaisha na kufanikisha maendeleo ya kiuchumi.

Hayo aliyasema leo, Aprili 5, 2025, wakati akifungua kongamano la mradi wa uhifadhi na utalii halali visiwani hapa, ‘Misali Holy Island as a Sacred Gift for a Living Planet (Al-mizan)’, katika Hoteli ya Golden Tulip, Mjini Zanzibar.

Al-mizan ni andiko la mradi wa elimu ya mazingira linalolenga kutoa ushauri na mikakati katika maeneo ya uhifadhi, uchumi wa buluu, na utalii halali, kwa madhumuni ya kukuza maendeleo ya nchi.

Mradi huo unatarajiwa kuchangia katika kulinda rasilimali za asili za Zanzibar, kuhamasisha utalii endelevu na kusaidia jamii kujikwamua kiuchumi kupitia mifumo ya utalii wa kijamii na endelevu.

Othman amesisitiza kuwa Zanzibar ina nafasi kubwa ya kutumia rasilimali zake za asili, kama vile maeneo ya Misali, kuendeleza sekta ya utalii na uhifadhi, huku akiwataka wadau wote kushirikiana katika kutekeleza mikakati ya uhifadhi kwa faida ya vizazi vijavyo.

Akielezea baadhi ya mifano ya hatua zilizochukuliwa na mataifa makubwa katika historia, Othman amesema kuwa Serikali ya Uingereza mwaka 1911 ilimtuma Kapteni Bristol pamoja na mabaharia wenzake kwa lengo la kuchora ramani ya kisiwa cha Pemba na hifadhi ya asili ya kisiwa cha Misali.

Othman amesisitiza kuwa kisiwa cha Misali kina historia na urithi wa kipekee ambao hauna mfano katika ukanda wote wa Bahari ya Hindi, kuanzia Pembe ya Afrika hadi Cape Town, Afrika Kusini.

“Wakati mwingine tunashindwa kuelewa na kubaini utajiri wetu uliojificha, ulio chini ya vizingiti vya milango yetu hapa nchini. Hivyo, tunapaswa kutumia misingi na mafunzo yaliyomo katika Qur-an ili kuhimiza uhifadhi wa mazingira, kwa ajili ya kuimarisha uzuri wa mazingira na kuboresha maisha ya watu,” amesema Othman.

Amesema  licha ya kutambua changamoto zinazokabili uhifadhi wa mazingira, uchumi wa buluu na utalii halali kama sekta, Serikali ya Zanzibar itaendelea kufanya juhudi kubwa ili kushirikiana na wadau wote katika kujenga mazingira bora ya maendeleo ya jamii.

Othman amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha kuwa malengo ya uhifadhi na maendeleo yanafanikiwa kupitia ushirikiano wa karibu na mipango endelevu.

Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga amesema mradi huo ni muhimu na hakuna ubishi kwamba dhamira ya uwekezaji katika visiwa vya Zanzibar inaendelea kuakisi maadili ya kiutamaduni na ujumuishaji wa wenyeji katika ngazi zote.

Waziri Soraga amesema ili kufikia malengo ya mradi, ni muhimu kuhakikisha kuwa jamii za visiwa zinajumuishwa kikamilifu katika michakato ya maendeleo na kuwa na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wadau, na wananchi.

Amebainisha kwamba mradi wa Al-mizan ni fursa ya maendeleo kwa Zanzibar, endapo utapata msaada na ushirikiano kutoka kwa Serikali, huku ukizingatia tamaduni za eneo pamoja na misingi ya dini ya Kiislamu.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,  Othman Masoud Othman akizungumza katika uzinduzi wa kongamano la Mradi wa uhifadhi na utalii halali Visiwani hapa Al-mizan.

Naye, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, Sheikh Abdullah Talib Abdullah, amefafanua kuwa uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa rasilimali ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza maisha ya watu na uzuri wa dunia.

Amesisitiza kwamba utalii halali unajali maadili, na kwamba yote hayo ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

“Utalii halali ni wajibu unaosisitizwa katika misingi ya Uislamu. Hata hivyo, kutokana na hatua ya kuupuuza kwa makusudi, ulimwengu unashuhudia changamoto nyingi, zikiwemo za mabadiliko ya tabianchi. Tunapaswa kujifunza kutoka kwa maelekezo ya dini yetu na kuchukua hatua madhubuti kulinda mazingira yetu,” amesema Sheikh Abdullah.

Akitoa maelezo mafupi kuhusu mradi huo, Mark Bryant kutoka Mpango wa Kimataifa wa Kiislamu wa Elimu na Sayansi ya Uhifadhi wa Mazingira (IFEES), amesema kuwa Zanzibar inapaswa kulinda uoto wake na uzuri wa asili kupitia uwekezaji unaoheshimu tamaduni na maadili ya kipekee ya visiwa hivyo.

Bryant amesema kwamba kufanya hivyo kutawawezesha wananchi wa Zanzibar kujiwekea mazingira bora ya kukuza uchumi wa kisiwa hicho, kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema  uhifadhi wa asili ni muhimu kwa kuhakikisha kwamba rasilimali za mazingira zinatumiwa kwa njia endelevu, zinazosaidia katika maendeleo ya uchumi, utalii, na ustawi wa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *