
Angola. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman na Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu wanadaiwa kuzuiwa kuingia nchini Angola kushiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD).
Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwenye msafara wake ameambatana na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Nasra Nassor Omar na maofisa wengine wa chama hicho.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo-Zanzibar, Ismail Jussa ameliambia Mwananchi leo Alhamisi Machi 13, 2025 kuwa Othman na msafara wake wamezuiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Luanda jijini Angola.
Tayari ACT Wazalendo imetoa taarifa ya kulaani tukio hilo ililoliita la udhalilishaji wa kiongozi huyo huku kamati yake ya uongozi ikikutana kwa dharura kujadili suala hilo, ambalo mamlaka za Angola hazijajitokeza kulizungumzia.
Wakati huohuo, Lissu ameandika kwenye ukurasa wake wa X kuwa mamlaka za uhamiaji za Angola zimewazuia na kukataa kuwaruhusu kuingia nchini humo, yeye pamoja na ujumbe wa zaidi ya viongozi wakuu 20 na wawakilishi wa vyama vya siasa kutoka Kusini mwa Afrika.
“Ambao tuliwasili Luanda mapema leo kwa ajili ya mkutano huo wa siku mbili, kundi hili linajumuisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa sasa kutoka Tanzania (Othman) , Rais wa zamani wa Botswana, Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho, pamoja na viongozi na wajumbe waandamizi kutoka Kenya, Sudan, Tanzania, Afrika Kusini, Namibia, Eswatini, Lesotho, Ujerumani, Marekani, Uganda, DRC, na Msumbiji,” Lissu ameeleza katika andiko hilo.
“Waangola na Watanzania ni ndugu wa damu. Tanzania ilimkaribisha Dk Antonio Agostinho Neto na wapiganaji wa MPLA katika miaka ya mwanzo ya harakati zao za uhuru. Tuliisaidia Angola kwa hali na mali wakati wa uvamizi wa kikoloni wa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini katika Kusini mwa Angola katika miaka ya 1970 na 1980,”ameandika Lissu
“Kama Angola, Tanzania ni mwanachama wa SADC, na kwa hivyo, sisi Watanzania hatuhitaji viza kuingia Angola.
“Matendo haya ya udhalilishaji kwa raia wa mataifa ndugu wa Afrika yanayofanywa na mamlaka za uhamiaji za Angola hayakubaliki na yanapaswa kulaaniwa kwa maneno makali kabisa,” amesema.