Othman aonya wagombea wenye masilahi binafsi 

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo (Taifa), Othman Masoud Othman amesema chama hicho hakitawavumilia watu wenye malengo binafsi katika kipindi cha kutafuta wagombea wa kukiwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, amesema hayo leo Ijumaa Aprili 11, 2025 alipozungumza na viongozi wa chama hicho Mkoa wa Kaskazini, Unguja. 

Amesema ni vyema kila mwanachama kutambua dhamira ya dhati ya chama hicho, ikiwemo kuendeleza mapambano ya kudai Zanzibar itakayokuwa na uwezo wa kuendesha mambo yake.

“Katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, chama hakitamvumilia mtu yeyote mwenye lengo binafsi katika kipindi hiki cha kutafuta wagombea wa nafasi mbalimbali, lazima nyote mfahamu lengo letu ni kuiona Zanzibar inajiendesha na si kutawaliwa na watu wenye masilahi binafsi,” amesema.

Othman amesema ACT-Wazalendo itaendelea kuhubiri mikakati ya uendeshaji wa Serikali na kila mwananchi anufaike na rasilimani za nchi.

Kwa mujibu wa Othman, Zanzibar iliwahi kuzitangulia nchi nyingi za Afrika katika maendeleo, ila kwa sasa yote yamebadilika na imekuwa miongoni mwa nchi za mwisho kimaendeleo. 

“Sisi tuna maono na tuna malengo na nchi hii, hivyo tunachohitaji ni mamlaka tuweze kuyatekeleza na kurudisha heshima ya nchi hii,” amesema. 

Amesema zipo haki nyingi za kiutu na kidemokrasia ambazo wananchi walistahili kupatiwa lakini wananyimwa na kutengwa katika mambo muhimu, hivyo ni wakati kwa wananchi kuungana na chama hicho kinachoipigania Zanzibar.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema wapo tayari kupambana kwa njia za kidemokrasia na wanaamini chama hicho kitashinda.

“Tangu 1995 ulipoanza mfumo wa vyama vingi vya siasa Zanzibar, mwaka huu tunashukuru kuona mwamko umeongezeka wa wananchi katika kuidai haki yao ya kidemokrasia na mabadiliko ya nchi,” amesema.

Jussa amesema harakati za ukombozi zilizoasisiwa na viongozi, akiwemo hayati Maalim Seif Sharif Hamad, hazipaswi kubezwa, badala yake ziheshimiwe kwa kuwa ni sehemu ya kuwaenzi na kuendeleza maono yao.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Omar Ali Shehe amesema ziara zinazoendelea kufanywa na chama hicho zimekuwa na mafanikio ya kuamsha hisia za wanachama na kuwaanda kujipanga kuelekea uchaguzi mkuu.

Kikao hicho ni mwendelezo wa ziara ya mwenyekiti wa chama hicho kukutana na viongozi wa ngazi zote katika mikoa mitano ya Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *