Othman ahimiza viongozi kuacha fitna wakigombea uongozi

Pemba. Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amewahimiza viongozi wa chama hicho kujenga umoja na kuepuka fitna wakati wa kuwania nafasi za uongozi na kuongeza umakini kuelekea uchaguzi mkuu, ili kukabiliana na uporaji wa haki dhidi ya demokrasia.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema hayo leo Jumanne, Aprili 8, 2025 alipokutana na viongozi wa chama Mkoa wa Kaskazini Pemba Micheweni.

Amesema chama hicho kinahitaji zaidi umoja na mshikamano utakaofanikisha kufikia lengo la kuinusuru Zanzibar na kuleta Zanzibar moja, mpya na yenye mamlaka kamili.

Amewataka watia nia wote kuitumia vema fursa hiyo kwa kuchaguana kwa uwazi, ili kupata viongozi watakaoleta mabadiliko.

Viongozi mbalimbali wa chama cha ACT-Wazalendo walioshiriki katika kikao cha chama kilichofanyika Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba leo Jumanne Aprili 8, 2025.

“Mamlaka kamili haiwezi kupatikana iwapo viongozi wa chama hatutakuwa na umoja na mshikamano, hivyo nawasihi watia nia wa nafasi mbalimbali kuitumia fursa hii ya kidemokrasia kuchaguana kwa uwazi ili kupata viongozi watakaoleta mabadiliko ya kweli Zanzibar,” amesema Othman

Sambamba na hilo, amesema wapo baadhi ya viongozi wa umma wanaotoka hadharani kuhubiri amani mbele ya wananchi, lakini wanashindwa kuonesha dhamira ya kulitekeleza jambo hilo kwa vitendo.

Akitaja baadhi ya matukio hayo, Othman amesema namna ya mamlaka hizo zilivyosimamia uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura ambapo ilionyesha matumizi mabaya ya nguvu za dola na pia ukiukwaji wa haki wa makusudi dhidi ya wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Omar Ali Shehe amesema utoaji vitambulisho vya Mzanzibari mkazi ni haki ya kila mmoja, hivyo Serikali hawapswi kulichukulia jambo hilo kisiasa.

Kikao hicho ni sehemu ya vikao vya mwenyekiti huyo kukutana na viongozi wa ngazi zote za chama hicho kwa ajili ya kupeana nasaha za maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *