Operesheni maalumu kudhibiti ajali Zanzibar yaanza

Unguja. Jeshi la Polisi Zanzibar limeanzisha operesheni maalumu kwa lengo la kupunguza na kudhibiti ajali zinazotokea kutokana na uzembe wa madereva na watumiaji wengine wa barabara.

Jeshi hilo limetangaza kuwa askari wake watachukua hatua kali dhidi ya wale watakaobainika kuendesha kwa uzembe au kutozingatia sheria za usalama barabarani.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Naibu Kamishna wa Polisi, Zuberi Chembera amewataka askari wa usalama barabarani kuwajibika na kuhakikisha wanasimamia sheria za usalama barabarani ili kupunguza vifo na majeruhi yanayosababishwa na ajali hizo.

Maelekezo ya Zuberi kwa trafiki yameakisi ongezeko la ajali za barabarani Zanzibar ambapo takwimu za polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) kwa mwaka 2023 watu 385 wamepoteza maisha katika ajali 193 zilizoripotiwa, kati ya hao 342 walikuwa wanaume na wengine wanawake.

Takwimu hizo zimebainisha kuwa katika kipindi hicho jumla ya makosa 38, 895 yameripotiwa katika vituo vya polisi.

Pia, kwa kipindi cha mwaka 2024 jumla ya ajali 201 zimeripotiwa ambazo zimesababisha vifo zaidi ya 400, Katika kipindi hicho jumla ya makosa 49, 789 yameripotiwa sawa naongezeko la makosa 10, 894.

Sababu kubwa zikitajwa ni mwendo kasi, uzembe wa madereva ulevi na kutozingatia sheria za usalama barabarani.

Kufuatia hali hiyo Jeshi la Polisi Zanzibar wameanzisha operesheni maalumu kuwadhibiti madereva wanaosababisha ajali.

Pia, Zuberi amesema licha ya ajali nyingi kutokea, lakini kuna jambo la muhali linalofanywa na baadhi ya maofisa wa usalama barabarani, hivyo kusababisha ajali hizo kuongezeka.

“Lazima tubadilike tuhakikishe tunasimamia sheria za usalama barabarani, kila mmoja atimize wajibu wake kunusuru majanga haya kwa kuchukua hatua zinazostahiki,” amesema na kuongeza

“Tuchukue hatua bila kumuonea mtu, au kumuogopa mtu,” amesema.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na maofisa wa Polisi wa wilaya na wakuu wa usalama barabarani wa mikoa ya Unguja jana Machi 25, 2025 akisema ajali zinaongezeka badala ya kupungua.

Zuberi ametumia fursa hiyo kutaka ushirikiano kutoka kila sehemu na kwamba watashirikiana na mamlaka za leseni kuwafutia watu wote leseni ambao wataonekana kwenda kinyume na matakwa ya sheria ili liwe fundisho kwa wengine.

Mitazamo ya wananchi

Wakizungumza kuhusu hali hiyo baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti licha ya kupongeza lakini wamesema changamoto kubwa ipo kwa askari wa usalama barabarani, kwani wengi wao wanazingatia ujazo ndani ya magari hususani daladala bila kushughulikia matatizo mengine.

“Jambo kubwa linalotutesa Zanzibar askari wake hawana mpango wa kushughulika na matatizo mengine kwenye gari wao wanachoangalia ni kama gari limezidisha tu abiria,” amesema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mwananchi mwingine, Mudathir Waab ambaye amesema jambo hilo linachangia kuongezeka kwa ajali kwani dereva anaweza akaendesha mwendo mkali au hata gari ni bovu, lakini hawana muda nalo.

Katika mtazamo wake wa mawazo, Ashura Ahmed ameenda mbali akasema ipo haja askari wa usalama wa barabarani wawe wanabadilishana na wa upande wa Tanzania Bara, kwa lengo la kupunguza mazoea na madereva hali inayoweza kupunguza ajali.

 “Binafsi naona ipo haja kuwabadilisha askari kila baada ya muda fulani ili kuondoa yale mazoea, maana tunashuhudia mengi baadhi ya madereva wakisema kama kuna askari fulani huyo hana shida twende tu, sasa ukisikia kauli kama hizi ndio zinasababisha ajali na kugharimu maisha ya wengi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *