Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuwa walinzi wa miundombinu iliyowekwa kwa ajili ya anuani za makazi, akieleza Serikali imetumia gharama kubwa kuisimika kurahisisha utambuzi wa maeneo na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Ametoa tamko hilo leo Jumamosi Februari 8, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi yenye kaulimbiu: “Tambua na tumia anwani za makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma.”
Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa anuani za makazi (NaPa) jijini Dodoma.
Majaliwa amesema licha ya Serikali kugharimia miundombinu ya kuweka anwani za makazi, kuna wananchi ambao siyo waaminifu wamekuwa wakiing’oa jambo ambalo ameeleza kuwa halikubaliki.
“Tunazo taarifa kwamba anuani za makazi zilizobandikwa kwenye nyumba zetu, vibao tulivyoviweka kuonyesha mtaa na barabara, tunao Watanzania ambao siyo waaminifu wanang’oa mabango hayo na kwenda kuyauza. Watanzania Serikali yetu imetumia gharama kubwa kutengeneza mifumo hii na kuiweka kwenye mitaa yetu ni muhimu kwetu kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii tuliyoiweka kwenye maeneo yetu,” amesema.

Majaliwa amesema: “Iwe ni bango umeliweka kwenye nyumba inaonyesha namba ya nyumba tulilinde kwa sababu lina manufaa au nguzo na bango linaonyesha barabara A, barabara B mtaa fulani. Alama hizi ni muhimu kwetu na hasa tunapoingia kwenye mfumo wa dijitali, kwa usalama wetu lakini kwa uhakika wa mahitaji yako, kwa hiyo ni muhimu tukashirikiana kulinda alama hizi, kila mmoja awe mlinzi wa maeneo haya.”
Amesema mfumo wa anuani za makazi ni daftari la kidijitali la wakazi na makazi kwa ajili ya kuwezesha kutambua masuala mbalimbali kulingana na uhitaji ikiwa ni pamoja na kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma za kijamii.
Amesema pia, unaimarisha masuala ya ulinzi na usalama katika nchi kwa kuwezesha kutambua tukio limetokea wapi na kujua eneo hilo lipo sehemu gani.

Majaliwa amesema litachochea uchumi na ukuaji wake, kuwezesha biashara mtandao kufanyika wakati wote kwa kila anayetaka kufanya biashara na ufanisi wake utapatikana kutumia mfumo wa NaPa.
Pia, itarahisisha uwezo wa kukabiliana na majanga kwenye maeneo ambayo sasa yatakuwa yanalindwa kwa kutumia mfumo wa kidijitali.
Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kukamilisha sheria ya anwani za makazi ili utaratibu na matumizi ya mfumo huo waufanye wakiwa na sheria inayowalinda.
Amesema sheria itasaidia kuweka masharti ya kimsingi ya kutumia anwani za makazi kwa ajili ya kupokea huduma na matokeo hayo yatokane na ulinzi wa kisheria.
Ameagiza washirikiane na wadau ambao wanajihusisha na mambo ya kidijitali, waratibu vifaa vinavyosaidia utendaji kazi na kuzifikia hadi ngazi ya vijiji, mitaa na shehia kuhakikisha utendaji kazi katika mfumo huo unafanikiwa.
“Lengo hapa ni kwamba mfumo huu uweze kutumika hadi vitongojini, uwanufaishe Watanzania ili kuwatambua,” amesema.

Ameiagiza Wizara ya Tamisemi kusimamia utendaji wa mfumo wa anuani za makazi kwa sababu wao ndiyo waliopo kwenye maeneo walipo watu wanaotumia mfumo huo.
“Najua ninyi ndio mnasajili vyombo vya usafiri kwenye maeneo yenu, nendeni mkawapate na mkawape elimu ya kutumia mfumo wa kidijitali katika kuongoza safari zao wanapotoa huduma kwenye maeneo ya jamii ili vyombo viwe na ramani ya kuwaelekeza wanapokwenda,” ameagiza.
Ameagiza Wizara ya Fedha ishirikiane na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuboresha mfumo wa NaPa kwa kuongeza moduli itakayosimamia vyombo vya moto ili kuhakikisha mambo hayo yanakamilika kwa haraka.
Majaliwa ameagiza wahakikishe magari yote ya Serikali yanafungwa mfumo wa NaPa na kuhamasisha wasafirishaji wa umma kutoka sekta binafsi kufunga mfumo huo kurahisisha utambuzi wa maeneo nchini.
Pia, amezindua mfumo wa barua ya utambulisho kwa njia ya kidijitali ambayo itawawezesha wananchi kupata utambulisho kutoka kwenye ofisi za mitaa kwa njia ya kidijitali badala ya kwenda kwenye ofsisi za mitaa kusubiri kwa muda mrefu.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema wameandaa mpango wa miaka miwili unaoanza leo baada ya uzinduzi wa matumizi ya mfumo wa anwani za makazi.
Amesema mpango huo ni kuhakikisha waratibu na watendaji wote wapatao 21,487 wa mikoa na halmashauri zote za Tanzania Bara na Zanzibar wanapatiwa vishikwambi vya anwani za makazi.
Waratibu ni 62 wa mikoa, 390 wa halmashauri, pia watendaji 3,956 wa kata, 4,263 wa mitaa, 12,318 wa vijiji, 110 wa wadi na 388 wa shehia.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayub Mohamed Mahamudu amesema asilimia 100 ya Zanzibar imeshaingizwa kwenye mfumo wa anwani za makazi na kwamba nyumba zote zimeshapatiwa namba, hivyo kuwarahisishia wageni wanaofika kujua mahali wanapokwenda.