Ongezeko la bodaboda na uhusiano wake kiuchumi

Bila shaka utakubali kuwa bodaboda imetoa ajira kwa watu wengi husuan vijana na kutokana na changamoto ya ukosefu wa ajira, hivi sasa kuna utani mpya mtandao ambao unawahimiza wanafunzi kujifunza udereva wa bodaboda wanapoelekea kumaliza masomo yao.

Bodaboda zinaongezeka na madereva wanaongezeka, takwimu za Benki kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2024 pekee Tanzania ilitumia Dola za Marekani 147.0 (Sh383.2 bilioni) kuagiza bodaboda nje ya nchi, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa.

Takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa ardhini (Latra) mwaka 2023/2024 zinaonyesha kuwapo kwa ongezeko la leseni za bodaboda zilizotolewa kwa asilimia 44.5 katika mwaka wa fedha 2023/2024 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Ongezeko la bodaboda zilizopewa leseni ya kufanya shughuli zake nchini kumeibua mitazamo tofauti kutoka kwa wadau na vijana,  huku ukosefu wa ajira ukitajwa kuwa moja ya sababu.

Ripoti hiyo ya Latra inabainisha kuwa Mamlaka ilitoa leseni 46,146 (D1) za pikipiki katika kipindi kilichoripotiwa, ikiwa ni ongezeko kutoka leseni 31,937 zilizotolewa kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2022/2023.

Leseni zilizotolewa kwa pikipiki zilichangia takriban asilimia 54.1 ya leseni zote zilizotolewa kwa magari ya kubeba abiria binafsi.

Kadhalika ripoti ya hiyo inaeleza kuwa idadi kubwa ya leseni za pikipiki zilitolewa katika eneo la kusini ambapo kanda hiyo ilibeba asilimia 39.1, zikifuatiwa na maeneo ya kati na ziwa ambapo kila moja ilikuwa na asilimia 17.8.

Eneo la mashariki lilichangia asilimia 16.4 wakati eneo la kaskazini lilikuwa na sehemu ndogo zaidi ya asilimia 8.9.

Kwa upande wa bajaji jumla ya leseni 22,408 zilitolewa ikiwa ni pungufu kwa asilimia 12.2 ikilinganishwa na leseni 25,512 zilizotolewa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2022/2023.

Katika kipindi kilichoripotiwa, idadi kubwa ya leseni za bajaji zilitolewa katika eneo la kusini likibeba asilimia 35.9, zikifuatiwa na kanda ya mashariki kwa asilimia 25.8, kanda ya kati kwa asilimia 14.7, kanda ya kaskazini kwa asilimia 12.9.

Sehemu ndogo zaidi ya leseni, yaani asilimia 10.7, zilitolewa katika eneo la Kanda ya Ziwa.

“Ajira hakuna, hii ndiyo sehemu pekee naweza kupata kitu kidogo kuendesha maisha, na hadi sasa nina pikipiki mbili baada ya kumaliza mkataba kwenye ile moja,” anasema Denis Kaswagula ambaye ni mhitimu wa chuo mwaka 2018 (bila kutaja kozi aliyosomea).

Anasema baada ya kukaa mtaani kwa miaka mitatu tangu kumaliza chuo, alikata tamaa ya kupata kazi ikiwa ni baada ya kusambaza barua sehemu mbalimbali bila mafanikio.

“Nilichoka, nikakata tamaa, siku moja nikiwa na rafiki yangu ambaye ni bodaboda alisema bosi wake anatafuta mtu wa kuendesha pikipiki nikaona acha nijaribu, niliweka malengo na sasa maisha yanaenda,” anasema Kaswagula.

Hoja yake inaungwa mkono na Vicent Antony ambaye anaeleza kuwa kupitia chombo hicho sasa amenunua kiwanja na anaendelea kuwekeza kidogokidogo ili aanze kujenga.

“Familia yangu inakua, naangalia namna niweke hata chumba na sebule ili tuhamie maana sikupata bahati ya kusoma lakini huku nimefanikiwa kidogo,” anasema Antony.

Wasemavyo wachambuzi

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Balozi Morwa amesema licha ya kuwapo kwa ongezeko hili na kutoa ajira kwa vijana lakini bodaboda haiwezi kuwapa maendeleo, kwa sababu mapato ni kidogo.

“Haiwezi kuleta mapinduzi inazuia tu wasiwe wazururaji, vijana wanaoendesha wengi wanapata tu hela ya kula, hawana elimu ya fedha hawajui kuweka akiba kuwa mbunifu kwa wateja ili wajiingizie kipato badala yake wanajiingiza katika ulevi,” amesema Dk Morwa.

 “Bila akiba hakuna uchumi, lazima uweke akiba bila hivyo ujue siyo maisha ni kama maisha ya ndege. Sasa hili linafanya waendelee kuleta vurugu barabarani na kutengeneza jeshi lao na kutumika wakati wa siasa kwa sababu wanahadaika kirahisi, hivyo hata viongozi wanaochaguliwa wanakuwa hawafai jambo ambalo linadidimiza uchumi,” amesema.

Pia amesema bodaboda nyingi zinaendeshwa na watu ambao hawana elimu kubwa kwani wengi waliomaliza shahada wanataka kazi za ofisini.

“Usomi tunaotengeneza vyuoni kuna shida mtoto anamaliza shahada anaona kufanya bodaboda haiwezekani, wengi wanaona kusoma ni kufanya kazi ofisini lakini Kenya utawakuta wanaendesha bodaboda, daladala hawa ndiyo wanakuwa kwenye nafasi ya kufanya maendeleo,” amesema Dk Morwa.

Amesema ikiwa kazi hiyo itafanywa na waliomaliza shahada uchumi unaweza kubadilika kwa sababu wanajua kusimamia fedha na vitu vya kufanya ili waendelee.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom) na mdau wa elimu, Dk Luka Mkonongwa alizungumzia suala la wahitimu kuingia katika bodaboda amesema mbali na kuleta ajira kwa vijana ambao wamemaliza vyuo lakini hasara inayopatikana ni kubwa kuliko faida.

Amesema bodaboda zimekuwa zikisababisha vifo vya watu na ulemavu jambo ambalo linapunguza nguvu kazi ya Taifa ambayo ingeweza kutumika katika sekta nyingine.

“Ukitaka kujua suala hili ni gumu hata usimamizi wake ni kama haufanyiki unavyotakiwa, angalia suala la uvaaji wa kofia ngumu nani anafuatilia, angalia wanaobeba watu wawili (mshikaki) nani anafuatilia ni kama wameamua kunyamaza, kuongeza bodaboda ni kama kuongeza vifo,” anasema Dk Mkonongwa.

Kuhusu ajali

Hata hivyo, pikipiki kwa mujibu wa takwimu za Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani 2023, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2023 jumla ya matukio 435 ya ajali za pikipiki yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio ya ajali 448 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Idadi hiyo ni pungufu ya matukio 13 sawa na asilimia 2.9. Hata hivyo, katika kipindi hicho, idadi ya vifo vya ajali za barabarani iliongezeka kwa vifo 44 kutoka vifo 332 vilivyoripotiwa mwaka 2022 hadi vifo 376 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 13.3.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi ajali hizi husababishwa na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto na kutofuata sheria za usalama barabarani.

“Uchakavu wa vyombo vya usafiri, ubovu wa miundombinu, ulevi, uzembe na uwepo wa vipuri visivyokidhi viwango,” imeeleza ripoti ya Jeshi la polisi.

Hali hii inaweza kuwa zaidi ya inavyoripotiwa kwani Taasisi ya Tiba na Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (Moi), inasema inapokea takribani majeruhi wa ajali za barabarani 700 kwa mwezi.

Kati ya majeruhi hao, asilimia 60 ambayo ni sawa na wajeruhi sita kati ya 10 wanatokana na ajali zinazohusiana na pikipiki, maarufu bodaboda.

Takwimu hizo zilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa hiyo, Dk Lemeri Mchome Jumanne ya Julai 2, 2024 hospitalini hapo, wakati akipokea msaada wa fedha pamoja na viti mwendo kutoka kampuni ya Watu Credit.

“Kwa kiwango kikubwa wagonjwa wengi wana uhusiano wa moja kwa moja na ajali za pikipiki aidha walikuwa abiria, dereva wa bajaji au gari limepata ajali kwa sababu lilikuwa linakwepa bodaboda au bajaji,” alisema Dk Mchome.

Anaelezwa kuwa asilimia 75 ya majeruhi hao hawana ndugu na hawana msaada wa kifedha kugharamia matibabu, kwa kuwa ajali zikitokea wanaletwa na raia wema pamoja na askari wa usalama barabarani.

“Asilimia 25 iliyobakia ni vijana ambao hawana ndugu kabisa, walikuja mjini kutafuta kipato. Tunakaa nao kwa zaidi ya miezi mitatu, gharama zinaongezeka,” alisema Dk Mchome.

Pia alisema wengi wao wanaumia vichwani, huku asilimia 75 wakiumia mikono na miguu:

 “Uhitaji wa vifaa ni kwa wale wagonjwa waliovunjika migongo na mifupa mikubwa, ndio tunawaomba wadau waje kuwasaidia.”

Hivyo, amesema kutokana na Sera ya Afya, Wizara inawagharamia matibabu, lakini baadaye ndugu wakijitokeza wanaombwa kuchangia matibabu hayo.