ONGEA NA AUNT BETTY: Nilimuacha kisa hana kazi, sasa namtamani

Swali: Nilikuwa na mchumba ambaye nilipanga nimuoe baada ya kujiweka sawa kimaisha.

Wakati tunakubaliana kuoana, mchumba wangu alikuwa na kazi na mama yake pia alikuwa na kipato cha kutosha.

Kwa bahati mbaya, ni kama upepo mbaya uliwapitia yeye na mama yake, wakawa hawana kazi na mzigo wa familia ukanielemea kwa kuwa mchumba wangu ndiyo mtoto wa kwanza wadogo zake watatu wanaosoma walikuwa wanamtegemea.

Nilijitahidi siku za mwanzoni kuwatatulia changamoto zao na za mama mkwe wangu mtarajiwa, lakini ilifikia mahali nikashindwa na kibinadamu niliamua kuachana na mpango wa ndoa na kila mmoja ashike hamsini zake.

Ajabu ni kwamba baada ya miaka miwili na miezi minane, aliyekuwa mchumba wangu amepata kazi nzuri kuliko ya mwanzo mara tatu, anabadili magari na hakika wana maisha mazuri kama familia, maana baba yao alifariki yeye na mama yake ndiyo wanaendesha hiyo familia.

Ananijulia hali kama kawaida akiniona mtandaoni. Natamani kurudiana naye ila ninashindwa kwa kuona aibu kutokana na nilivyomuacha akiwa amefulia. Naomba ushauri nifanyeje?

Jibu: Natamani kusema huna haya kwa kufikiria kumrudia, ila acha nikae kimya.

Katika maisha, uhusiano unaweza kukumbwa na changamoto nyingi, na mara nyingine mabadiliko ya hali ya kiuchumi yanaweza kuchangia katika uamuzi mgumu.

Ni muhimu kuelewa kwamba kukosa kazi na hali ngumu ya kifedha inaweza kuwa na athari kubwa si tu katika maisha binafsi, bali pia katika uhusiano.

Hapa hakuna ninaloweza kukushauri likakuweka mbali na aibu ya kurudi kwa mwanamke (mchumba), uliyediriki kumkimbia kwa zaidi ya miaka miwili kisa kukosa fedha.

Maana katika maelezo yako hakuna sababu nyingine zaidi ya hiyo iliyokufanya umuache katika kipindi kigumu zaidi ya kukimbia majukumu.

Natamani nikuambie uachane naye maana ndiyo njia pekee ya kukwepa aibu, ila sijajua huyo mchumba alikupenda kiasi gani, pengine anatamani umrudie.

Kwanza kabla hujakwenda kujidhalilisha jiulize mwenyewe unafanya hivyo kwa sababu ya mapenzi au unafuata mabadiliko yake ya kifedha. Kwani jamii na mhusika mwenyewe atakuwa anajua hivyo, sasa jiulize mwenyewe kwanza.

Ukishapata jibu panga miadi ya kukutana naye kujadili uchumba wenu uliofifia kwa zaidi ya miaka miwili.

Hakikisha unamweleza kilichokukimbiza kwa uwazi bila kuficha kuwa ulikimbia kwa sababu ulishindwa majukumu na siyo kumchukia, maana hakuna namna zaidi ya kuwa mkweli.

Baada ya hapo kuwa msikilizaji, muache azungumze, akulaumu, akulalamikie, usiwe mwepesi wa kujibu ili ujue ana msimamo gani na aliumia kiasi gani na kama nafasi yako bado ipo.

Usipokuwa makini anaweza kukubali muendelee kuwa pamoja kwa lengo la kukuonyesha cha mtema kuni, akiamini umefuata fedha na mali alizopata baada ya kuwa na kazi nzuri.

Pia ukubali kudhihakiwa na jamaa zake, wakiwamo wadogo zake ambao pia uliwakimbia, kwani ulikuwa ndiyo msaada pekee kwao baada ya dada yao kufulia.

Jiandae pia kisaikolojia kwa majibu yoyote, yanaweza kuwa mazuri au ya nyodo, hivyo hasira, ghadhabu unapokwenda kumuomba muendelee ziache nyumbani.

Mbinu nyingine ambayo nahisi inaweza kuwa nzuri, mfanye rafiki kwa muda kabla hujamwambia wazo lako. Hii itasaidia kuondoa joto la hasira za kuachwa. Ila hili liwe funzo kwako, kwani maisha hubadilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *