
Manchester,England. Kiungo wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes ametaja wachezaji nane ambao wanatakiwa kuonyeshwa mlango wa kutokea na timu hiyo baada ya msimu huu kumalizika.
Scholes ambaye aliichezea Man United idadi ya mechi 714 kabla hajastaafu anaamini kuondoka kwa wachezaji hao nane na ujio wa nyota wapya kutasaidia kuimarika kwa timu hiyo.
Katika hali ya kushangaza, Scholes amemtetea kipa Andre Onana ambaye mashabiki wengi wa Manchester United wanataka aondoke akisema kuwa anastahili kuendelea kupewa imani ndani ya klabu hiyo.
“Nadhani ningembakisha. Naendelea kuamini kuna mengi yanakuja kutoka kwake lakini kwa sasa ningembakisha,” alisema Scholes.
Wachezaji ambao Scholes anatamani kuona wakipewa mkono wa kwaheri ndani ya Mancheter United ni Matthijs de Ligt, Lisandro Martinez. Luke Shaw, Mason Mount, Antony, Joshua Zirkzee, Casemiro na Marcus Rashford.
De Ligt, Martinez. Shaw na Mount,anataka waachwe kwa sababu ya majeraha ambayo wamekuwa wakiyapata mara kwa mara na kupelekea kuigharimu timu kwa kuwakosa katika mashindano tofauti.
“Nampenda sana mchezaji. Kama hayupo fiti uza,” alisema Scholes.
Hata hivyo Scholes amesema kuwa Manchester United isije kuthubutu kuwaacha makinda Kobbie Maino na Alejandro Garnacho kwa vie ni wachezaji wazuri na wanaufahamu vyema utamaduni wa klabu.
Scholes ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kuibuka kwa tetesi kuwa Chelsea inajipanga kuhakikisha inamnasa Maino ikiwa hatofikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya na Man United.
Lakini pia kumekuwepo na taarifa kuwa Man United pia inajipanga kumuonyesha mlango wa kutokea Garnacho ambaye inaripotiwa kwamba anawaniwa vilivyo na Juventus inayoshiriki Ligi Kuu Italia.
Katika kundi hilo la wachezaji ambao Scholes amependekeza watemwe, Marcus Rashford ana uwezekano mkubwa wa kuachana na klabu hiyo kutokana na mahusiano yasiyoridhisha ambayo amekuwa nayo na meneja Ruben Amorim.
Amorim amekuwa hamtumii Rashford katika kikosi chake tangu alipojiunga nayo akitokea Sporting Lisbon.