Ombi la Antonio Guterres la kuzuia kuongezeka mivutano katika vita vya Ukraine

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuzuia kuongezeka mapigano nchini Ukraine.

Kwa mujibu wa ripoti ya mtandao wa Sahab, Antonio Guterres, huku akijibu ripoti ya New York Times kwamba  Rais Joe Biden wa Marekani  ameidhinisha mashambulizi ndani ya ardhi ya Russia  kwa kutumiwa makombora ya masafa marefu yaliyotengenezwa na Marekani, amesisitiza kuwa: ‘Kuongezeka kwa vita nchini Ukraine lazima kuepukwe haraka iwezekanavyo.’

Gazeti la New York Times Jumatatu, likiwanukuu maafisa wa Marekani, lilithibitisha kwamba Rais Biden wa Marekani ameidhinisha jeshi la Ukraine kutumia makombora ya  ATACMS yaliyotengenezwa Marekani kwa ajili ya kushambulia ndani kabisa ya ardhi ya Russia, kuimarisha nafasi zake za kijeshi na kuongeza udhibiti wa jeshi la Ukraine juu ya eneo la Kursk na kuwa vikwazo vyote kuhusiana na suala hilo vimeondolewa.

Gazeti la Ufaransa Le Figaro pia limeandika katika ripoti yake kwamba baada ya rais wa Marekani kutoa ruhusa kwa Ukraine kutumia silaha za masafa marefu za Marekani kushambulia maeneo ya kijeshi ndani ya ardhi ya Russia, Paris na London pia zimeiruhusu Kyiv kutumia silaha zao katika vita vyake dhidi ya Russia.

Mnamo Februari 21, 2022, Rais Vladimir Putin wa Russia alitambua rasmi uhuru wa Donetsk na Luhansk katika mkoa wa Donbas, baada ya kukosoa vikali upuuzaji wa nchi za Magharibi kuhusu wasiwasi wa kiusalama wa Moscow.

Mnamo Februari 24, rais wa Russia aliamuru shambulio la kijeshi lifanyike dhidi ya Ukraine na hivyo kubadilisha uhusiano ulioharibika kati ya Moscow na Kyiv kuwa mzozo wa kijeshi.