
KATIBU wa zamani wa Yanga na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omar Kaya sambamba na Yohana Msita wameula baada ya kuteuliwa katika nafasi mbili tofauti ndani ya klabu ya Singida Black Stars.
Msita ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Utawala wakati Kaya ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Fedha wa klabu hiyo iliyopo Ligi Kuu Bara na iliyotinga 16 Bora ya Kombe la Shirikisho.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo jana imeeleza viongozi hao wameteuliwa kwa mujibu wa katiba ya Singida BS.
“Bodi ya Wakurugenzi ya Singida katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika Machi 9, imemteua Mhe Yohana Stephen Msita kutokea wilayani Manyoni mkoani Singida kuwa Makamu Mwenyekiti (Utawala) na Omari Kaya kuwa Makamu Mwenyekiti (Fedha),” taarifa hiyo ilisomeka hivyo na kuongeza;
“Msita ni mdau mkubwa wa michezo mwenye uelewa wa kutosha wa masuala ya mpira wa miguu na kiu ya mafanikio, uteuzi huo umefanyika kutimiza matakwa ya katiba ya klabu yetu ambayo kwenye safu ya uongozi inatambua nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wawili utawala na fedha,” ilisema taarifa hiyo.
Singida, iliyopo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu, kesho itashuka uwanjani kuvaana na KMC katika mechi ya hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati Manyara.
Singida ilifika hatua hiyo kwa kuing’oa Leo Tena kwa mabao 4-0 katika hatua ya 32 Bora, huku KMC ikiwatupa nje mabingwa wa zamani wa Ligi ya Bara, Cosmopolitan kwa mabao 2-0 na mshindi wa mchezo huo atakata tiketi ya kutinga robo fainali kuanza msako wa taji la michuano hiyo.
Bingwa wa michuano hiyo huiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika na kwa sasa watetezi ni Yanga ambayo jioni ya leo inashuka uwanjani kuvaana na Coastal Union kukamilika mechi za hatua ya 32 Bora ili kuungana na klabu 15 zilizotangulia ikiwamo Simba, Pamba Jiji na Kagera Sugar zilizofuzu jana kwa kupata ushindi mbele ta TMA Stars, Kiluvya Utd na Namungo mtawalia.