
LICHA ya kwamba imeshapita miaka zaidi ya sita tangu Emmanuel Okwi alipoondoka nchini baada ya kumalizana na Simba aliyokuwa akiichezea, lakini jina lake bado linaendelea kutajwa ikielezwa ndiye mchezaji aliyekuwa tishio kwa miaka ya karibuni katika Dabi ya Kariakoo.
Okwi ni mmoja ya wachezaji waliobahatika kucheza katika vikosi vya watani wa jadi akianza na Simba kisha Yanga na baadae kurudia tena Simba hadi anaondoka na kwenda kucheza soka la kulipwa Misri, akikumbukwa kwa bao lililoinyamazisha Yanga katika dabi ya kwanza ya Machi 8, 2015.
Okwi aliyefunga pia mabao mawili wakati Yanga ikifumuliwa mabao 6-0 na Simba katika pambano lililopigwa Mei 6, 2012 likiwamo la kwanza alililofunga sekunde chache tu tangu filimbi ya kwanza ya mchezo huo ulioondoka na aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga.
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti jana juu ya wanavyoina Dabi na wanavyokumbuka maandalizi ya mechi kama hizo kwa wachezaji waliokipiga timu zote, asilimia kubwa wamemtaja Okwio wakisema alikuwa balaa kwa namna alivyokuwa msumbufu na kasi uwanjani, kwani ni mmoja ya waliofunga huku na kule.
Okwi aliitungua Simba wakati akiitumikia Yanga katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyopigwa Des 21, 2013 ambapo Yanga ilicharazwa mabao 3-1, yeye akifunga dakika ya 87, baada ya Amissi Tambwe kufunga mara mbili dk 14 na 44 na Awadh Juma ‘Maniche’ dk 66 kuitanguluiza Simba.
Mastaa mbalimbali waliowahi akiwa na Simba JINA la aliyekuwa winga wa kushoto wa Simba na Yanga, Emmanuel Okwi ndilo linaloongoza kutajwa alikuwa tishio mechi za dabi, kutokana na namna alivyokuwa anawapa kazi ngumu mabeki kumkaba.
Okwi aliyeichezea Simba kwa misimu tofauti 2009-2013, 2014/15, 2017-2019 na Yanga ni 2013/14 ametajwa na mabeki wengi waliokabana nao enzi akiuwasha kuwa, alikuwa anawapasua kichwa namna ya kumkaba.
Mwanaspoti limezungumza na mastaa mbalimbali waliocheza Simba na Yanga katika nyakati tofauti, wanaiona dabi ya Machi 8 itakuwa ngumu kutokana na timu hizo kupishana pointi chache, ambapo kwa sasa ni Clatous Chama, Jonas Mkude waliotoka kwa Wanamsimbazi wamebakia Wanajangwani.
Yanga mwenyeji wa dabi hiyo ndio inayoongoza kileleni kwa pointi 58 katika mechi 22 imeshinda 19,sare moja na imefungwa mechi mbili kwa upande wa Simba inashika nafasi ya pili ina pointi 54 imecheza mechi 21, imeshinda 17, sare tatu na imefungwa mmoja.
AMIR MAFTAH
“Wakati nikiwa Yanga ambako nilicheza 2007-2010 nilikuwa namhofia sana Okwi ambaye ilikuwa inahitaji akili kubwa kumkaba, kilichokuwa kinanisaidia nilikuwa bora, wakati nipo Simba nilikocheza 2010-2013 Yanga ilikuwa na washambuliaji kama Godfrey Bonny (marehemu) na Ben Mwalala ambao walihitaji umakini kuwakaba,” alisema Maftah na kuongeza;
“Dabi bora ambayo sitaisahau maishani mwangu ni ya mwaka 2012 tulivyoifunga Yanga mabao 5-0 nilikuwepo kikosini,ilitupa heshima kubwa, lakini ushauri wangu kwa mechi ya Machi 8, mabeki Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ waongeze umakini wa kuwazuia Clement Mzize, Prince Dube na Aziz Ki, kwa mabeki wa Yanga Ibrahim Bacca na Dickson Job wawe makini na Kibu Denis na Leonel Ateba, mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na mpishano wa pointi.”
DEOS MUNISHI ‘DIDA’
Kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ alisema wakati wa maandalizi timu hizo hazina tofauti, zinakuwa na presha kubwa kwani ni mechi ambayo inaweza ikamuondoa mchezaji katika ramani ya soka, endapo akicheza chini ya kiwango.
“Yanga wakati imechukua ubingwa mara tatu mfululizo ndizo zilikuwa dabi zangu bora mshambuliaji niliyekuwa namhofia alikuwa Okwi, nikiwa Simba sijawahi kudaka mechi ya dabi, Machi 8 itakuwa mechi ngumu kulingana na pointi ambazo timu hizo zimepishana dakika 90 zitaamua,” alisema Dida anayecheza Geita Gold kwa sasa.
BENO KAKOLANYA
Kipa wa Namungo, Beno Kakolanya amecheza Yanga(2018-2019) na Simba (2019-2023) anazungumzia maandalizi ya klabu hizo namna yanavyokuwa na presha kubwa kwa wachezaji na viongozi, kila upande ukiwa unataka pointi tatu.
“Msimu wangu wa kwanza kucheza Yanga dabi bora kwangu ni ya 2018/19 tulitoka kwa suluhu, nilicheza kwa kiwango kikubwa, maandalizi timu zote zinakuwa na presha kubwa, hizo mechi zinaweza zikashusha kiwango cha mchezaji ama kumpandisha,” alisema Kakolanya.
HARUNA MOSHI ‘BOBAN’
“Kila timu ina miiko na tamaduni zake ingawa presha hazitofautiani, kuhusu mechi ya Machi 8 itakuwa ngumu zimepishana pointi kidogo, ngumu kutabiri nani anaweza akaibuka na ushindi, kikubwa ni umakini wa wachezaji kuzipambania timu zao,” alisema Boban aliyeichezea Simba kwa misimu tofauti 2004-2009, akaondoka kwenda Gefle IF 2010/11 akarejea tena 2011 -2013 na Yanga 2018 lilikuwa chaguo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera.
DANNY MRWANDA
“Kiuongozi timu hizo zipo tofauti na siwezi kulizungumzia hilo, ila katika maandalizi presha ipo kote kwani ni mechi ambazo zinaweza zikampa thamani mchezaji ama kumuondoa katika ramani ya soka, kuhusu mechi ya Jumamosi ngumu kutabiri nani ataibuka mshindi dakika 90 zitaamua,” alisema Mrwanda aliyecheza Simba kwa nyakati tofauti msimu wa 2006-2008, 2009/2010, 2012/13 na Yanga 2014/15.
NURDIN BAKARI
Beki wa zamani wa Simba (2004-2007) na Yanga (2007-2013), Nurdin Bakari anasema maandalizi ya dabi ni tofauti na mechi zingine viongozi wanakuwa muda wote kambini, ulinzi mkali kuhakikisha hakuna ambaye anafikiriwa vibaya.
“Kwa mara ya kwanza kucheza dabi ilikuwa msimu wa 2004/2005 nikiwa Simba, tulichezea Mwanza tuliifunga Yanga mabao 2-1, nilitoa asisti mbili za mabao, nilimkaba kisawasawa mchezaji ambaye alikuwa wa moto kipindi hicho Said Maulid ‘SMG’ hadi nililia machozi ya furaha,” alisema Bakari na kuongeza;
“Nikiwa Yanga mchezaji ambaye alikuwa hatari kwa Simba ni Okwi, Haruna Moshi ‘Boban’ na Patrick Mutesa Mafisango apumzike kwa amani, hao jamaa walikuwa ni balaa, ukizubaa tu inakula kwako, kuhusu dabi ya Machi 8 ni ngumu mmoja wapo akishinda bado taswira ya ubingwa haiwezi kuonekana kutokana na upinzani uliopo.”
ALPHONCE MODEST
Beki wa zamani wa Pamba, Simba, Yanga na Mlandege, Alphonce Modest alisema; “Yanga hawana mchezo kabisa na kambi ya wachezaji, pengine kwa sababu nilitoka Simba ndio maana walikuwa wakali, ingawa presha ni ile ile, haina utofauti kabisa.”
Wengine waliowahi kukipiga Simba na Yanga kwa vipindi tofauti ni; Zamoyoni Mogella, Edibily Lunyamila, Juma Kaseja, ‘SMG’, Ramadhan Hassan ‘Kessy’, Athuman Idd ‘Chuji’, Gadiel Michael, Ally Mustafa ‘Barthez’, Ibrahim Ajibu, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga na Jean Baleke.
Wapo pia kina Bernard Morrison, Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa, Akida Makundi, Athuman Abdallah ‘China’, Yew Berko, Doyi Moke, Ismail Suma, Godwin Aswile, Willy Martin, Said Mwamba ‘Kizota’, Method Mogella, Thomas Kipese, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, Joseph Katuba na wengine kibao baadhi wakishatangulia mbele ya haki na wale wanaoendelea na maisha nje ya ulimwengu wa soka.