
KIUNGO mshambuliaji wa Tabora United, Offen Chikola amesema mapumziko ya Ligi Kuu Bara kupisha mechi za Kalenda ya FIFA yamemsaidia kuondoa uchovu mwilini uliotokana na kucheza mechi mfululizo.
Chikola ambaye ana mabao saba na asisti mbili katika Ligi Kuu Bara msimu huu, alisema watakaporejea kuendelea na ligi tayari mwili wake upo fiti na ana hamu ya kufanya makubwa zaidi katika mechi zilizosalia kufunga msimu.
“Narudi na nguvu mpya, natamani mechi zilizosalia nifunge mabao siyo chini ya 10, ingawa najua mechi za mwisho za kufunga msimu zinakuwa na ushindani na ngumu kwani kila timu inakuwa inapambania malengo yake,” alisema Chikola anayemkubali Mohamed Salah wa Liverpool kutokana na kasi yake, kukokota mipira, umaliziaji na utimamu wa mwili.
Tabora United katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ipo nafasi ya tano baada ya mechi 23, imeshinda 10, sare saba na kupoteza sita ikikusanya pointi 37.
Nje ya kutamani kufunga, Chikola alisema matarajio yake ni kuiona timu hiyo inamaliza ndani ya Top 3.
Katika mechi 23 ambazo Tabora imecheza msimu huu, Chikola kacheza 22, kati ya hizo tano hakumaliza dakika 90 ambazo ni dhidi ya Mashujaa (dk79), Simba (dk82), Prisons (dk75), JKT Tanzania (dk65) na Fountain Gate (dakika 78).
“Ukiachana na hayo yote nashukuru nimekuwa na msimu mzuri ambao makocha wameniamini kuwa muhimu kikosi cha kwanza,” alisema nyota huyo.