
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, yupo Juba nchini Sudan Kusini, kujaribu kuwapatanisha viongozi wakuu wa nchi hiyo, baada ya kukamatwa na kuzuiwa nyumbani kwa Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar, siku ya Jumatano usiku.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Dennis Onyango, msemaji wa Odinga, amethibitisha kuwasili kwa mwanasiasa huyo mkogwe wa Kenya jijini Juba, siku ya Ijumaa asubuhi.
Siku ya Alhamisi, rais wa Kenya William Ruto ambaye pia ni Mwenyikiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema siku ya Alhamisi, baada ya kushauriana na viongozi wa ukanda wa Afrika Mashariki na Waziri Mkuu wa Ethiopia, alimtuma mjumbe maalum, ambaye ni Odinga kujaribu kutafuta suluhu ya mzozo unaoendelea.
Jitihada za kimpatanisha Machar na Riek Machar, zinakuja wiki kadhaa baada ya kuanza kushuhudiwa kwa mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wanaojiita White Army katika jimbo la Upper Nile, wanaoripotiwa kumuunga mkono Machar.
Chama cha Machar, SPLM IO kimetangaza kuvunjika kwa mkataba wa amani wa mwaka 2018, uliotiwa saini kati ya rais Kiir na Machar, na wawili hao kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, baada ya kiongozi wake kukamatwa.
Umoja wa Mataifa, umeonya uwekezano wa kutokea tena kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe iwapo, suluhu haitapatikana. Siku ya Ijumaa, hali ya utulivu ilishuhudiwa jijini Juba, huku wakaazi wakiendelea na shughuli zao za kawaida.