Nyumba za wageni tishio Zanzibar, Simba v Stellenbosch CAFCC

Ikiwa imesalia siku moja kabla ya mechi ya nusu fainali ya kwanza ya  Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na Stellenbosch, hali ya Zanzibar imeanza kubadilika kwenye maeneo ya makazi karibu na Uwanja wa New Amaan.

Taarifa kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa nyumba za kulala wageni na hoteli ndogo katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Amaan, Mazizini na Tomondo zimeanza kujaa kutokana na wimbi la mashabiki, wanahabari na wageni kutoka Bara pamoja na mataifa mengine waliotua kwa ajili ya mechi hiyo.

Wamiliki wa baadhi ya nyumba za kulala wageni wamedai kupata maombi mengi ya nafasi za kulala kiasi cha kuzidi uwezo wa maeneo yao wa kawaida.

“Mara tu ratiba ilivyotangazwa kuwa Simba wanacheza nusu fainali hapa Zanzibar, simu zetu hazijakaa kimya. Tuna wageni kutoka Dar, Arusha, Mwanza na hata Afrika Kusini. Wengi wanataka malazi karibu na uwanja, lakini nafasi zimejaa,” ameema Salma Ahmed, meneja wa nyumba  moja ya wageni iliyopo Mazizini.

Wakati idadi ya nafasi inapungua, baadhi ya maeneo yameongeza bei kwa huduma zilezile. 

Malazi ya kawaida yaliyokuwa yanapatikana kwa Sh40,000 kwa usiku mmoja, sasa yanagharimu hadi Sh70,000  huku baadhi ya hoteli za kati zikiweka masharti ya kulipia kwa siku tatu mfululizo.

Kwa mashabiki au wageni waliopanga kuingia Zanzibar dakika za mwisho, ni wazi kuwa watakumbana na changamoto kubwa ya kupata sehemu ya kulala watahitaji mbinu mbadala ikiwemo kuongea na marafiki au jamaa waishio Zanzibar kwa ajili ya malazi.

Hiyo ni ili waweze kutumia maeneo ya mbali kama Fuoni, Mbweni au Kisauni ambako bado kuna nafasi, japo ni mbali na uwanja.

Vilevile watahitajika kuweka miadi ya mapema kwa njia ya mtandao kwa hoteli zinazopatikana kwenye tovuti na kufikiria kupanga kwa pamoja ili kupunguza gharama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *