
Dar es Salaam. Hatimaye msanii Bongo Movie, Joyce Mbaga (32) maarufu Nicole Berry na mwenzake Rehema Mahanyu (31), wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.
Msanii huyo na mwenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni, Jumatatu Machi 10, 2025, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kutokana na kupokea amana (fedha) kutoka kwa umma bila kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Licha ya dhamana yao kuwa wazi, lakini siku hiyo walishindwa kutekeleza masharti ya dhamana, wakapelekwa mahabusu hadi watakapoyatekeleza, huku kesi yao ilipangwa kutajwa, Machi 24, 2025.
Hata hivyo, Nicole na mwenzake wameachiwa huru leo Jumatatu, Machi 17, 2025, na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhani Rugemarila, anayesikiliza kesi hiyo, baada ya kutimiza masharti haya ya dhamana.
Ingawa siku rasmi ya kufika mahakamani ni Machi 24, 2025 lakini wamepelekwa mahakamani leo Jumatatu Machi 17, 2025 kwa amri maalumu ya Mahakama ya kuwatoa mahabusu kuwapeleka mahakamani (remove order) kwa ajili ya kudhaminiwa baada ya kuomba kutokana na kukamilisha masharti hayo ya dhamana.
Masharti hayo waliyopewa ni pamoja na kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali za mitaa na kama ni mwajiriwa awasilishe barua ya ofisi yake.
Sharti jingine lilikuwa ni kuwasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya Sh185.51 milioni, ambazo wanadaiwa kuzipokea kama amana kutoka kwa umma bila kuwa na kibali.
Nusu ya fedha hizo walizopaswa kuzitoa ni Sh92. 75 milioni, kiasi ambacho washtakiwa wote wakitakiwa kugawana au kukichangia. Hivyo Kila mshtakiwa alitakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh46,378,750.”
Hata hivyo, Nicole amedhamiwa kwa hati ya nyumba yenye thamani ya Sh100 milioni iliyotolewa na mmoja wa mdhamini wake, ambao majina yao hayajafahamika.
Mwenzake, Rehema kwa upande wake amedhaminiwa na Ramadhan Juma pamoja na Joyce Isdon, pamoja na hati yanyumba yenye thamani ya Sh57 milioni.
Washtakiwa wote mahakamani wamewakilishwa na Wakili wa kujitegemea, Nashon Nkungu, huku upande wa mashtaka uliwakilishwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Rhoda Kamungu.
Katika kesi hiyo Nicole na mwenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu, wanayodaiwa kuyatenda makosa hayo kati ya Julai 2024 na Machi, 2025 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam.
Shtaka la kwanza ni la kuongoza genge la uhalifu, kwa lengo la kujipatia fedha, shtaka la pili ni la kupokea fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni na shtaka la tatu ni kuendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo kutoka BoT.
Akiwasomea mashtaka, katika shtaka la kwanza wakili Rhoda alidai kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo kwa lengo la kujipatia faida kwa kupokea amana au miamala kutoka kwa jamii bila kupata leseni.
Katika shtaka la pili, alidai kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025 wakiwa eneo lisilofahamika ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walipokea amana ya Sh185,515,000 (Sh185.51 milioni) kutoka kwa jamii bila kuwa na leseni.
Katika shtaka la tatu, wakili Rhoda alidai kuwa katika shtaka la tatu washtakiwa waliendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo inayotolewa na BoT.
Hata hivyo, hawakutakiwa kujibu chochote hadi pale upelelezi utakapokamilika na mahakama hiyo kupewa kibali cha kusikiliza kesi hiyo ndipo watakapojibu kama ni kweli au si kweli.
Baada ya kuwasomea mashtaka, wakili Rhoda alieleza Mahakama kwamba upelelezi bado haujakamilika na kwamba pia hawana pingamizi ya dhamana ya mshtakiwa.
Wakili Jeremiah Mtobesya anayemtetea Nicole na Avelina Nelson anayemtetea Rehema waliiomba mahakama itoe dhamana kwa wateja wao kwa sababu mashtaka wanayoshtakiwa nayo yanadhaminika.
Hakimu Rugemalira, aliwataka kuwasilisha mahakamani pesa taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha fedha kilichotajwa kwenye shtaka, kwa mujibu wa kifungu cha 148 (5) (e), cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Kwa mujibu wa kifungu hicho, pale shtaka linapohusisha fedha zinazozidi Sh10 milioni, kupata dhamana mshtakiwa anapaswa kuwasilisha mahakamani nusu ya kiasi hicho cha fedha au mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi hicho cha fedha kilichoko kwenye hati.
Hata hivyo, kama washtakiwa ni zaidi ya mmoja basi washtakiwa hao watapaswa kuchangia kwa kiasi sawa kiasi hicho cha pesa yaani hiyo nusu ya kiasi cha fedha kilichotajwa kwenye shtaka.