Nyumba 1,000 Dar kuunganishiwa gesi

Dodoma. Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ipo katika mpango wa kuunganisha gesi nyumba zaidi ya 1,000 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambapo kati ya nyumba hizo, nyumba 279 zitapatikana Wilaya ya Kinondoni.

Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi April 17, 2025 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dastan Kitandula alikuwa akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Nishati ambaye hakuwepo bungeni leo.

Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Kinondoni (CCM), Tarimba Gulam ambaye amehoji Serikali imefikia wapi katika mradi wa kusambaza gesi ya kupikia majumbani wilayani Kinondoni.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo amehoji kipaumbele cha Serikali ni kipi katika kuwafanya wananchi wapate huduma za nishati safi ya kupikia ambacho ndicho kipaumbele cha nchi kwa sasa.

Naibu Waziri amesema katika Wilaya ya Kinondoni, Serikali imeshapeleka miundombinu ya usambazaji gesi asilia ambapo jumla ya nyumba 155 zimeunganishwa na mtandao wa matumizi ya gesi asilia katika eneo la Mikocheni.

Hata hivyo, Naibu Waziri amesema kuna mambo ambayo hayakuwa yameweka vizuri lakini kwa sasa kila kitu kimekaa vizuri hivyo wananchi watarajie neema ya kuunganishiwa gesi ili iwasaidie kuondokana na matumizi ya nishati isiyo salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *