Kibaha. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani likiendelea kumshikilia mmiliki wa kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, Stephano and Agape Foundation, kwa tuhuma za ubakaji wa watoto watano, baadhi ya wafanyakazi, majirani na viongozi wa mtaa wameeleza namna walivyopata taarifa.
Polisi inamshikilia Stephano Maswala, ambaye ni mmiliki wa kituo hicho, anayedaiwa kuwabaka watoto watano wanaolelewa kituoni hapo kwa nyakati tofauti.
Februari 8, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salimu Morcase, alitoa taarifa kuwa wanamshikilia Stephano kwa tuhuma ya kuwabaka watoto hao kati ya Oktoba 2024 hadi Januari 2025.
“Mtuhumiwa alikuwa anawabaka watoto akiwadanganya kuwa anawatengeneza kisaikolojia ili wasisumbuliwe na wanaume mitaani na wafanye vizuri kwenye masomo yao ya sekondari,” amesema Morcase katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Leo, Februari 11, 2025, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mlandizi (OCD) Kasanga amekiri kuwepo kwa kesi hiyo huku akisema upepelezi unaendelea.
Mwandishi wa gazeti hili leo ametembelea kituo hicho kilichopo Mtaa wa Guest Mpya, Mlandizi, mkoani Pwani, na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi wa kituo, viongozi wa mtaa, majirani na polisi, ambao wameeleza namna walivyopata taarifa ya tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi, mlezi wa watoto kituoni hapo, Devotha Mwaishuya, amesema kufuatia tukio hilo, watoto saba wameshaondolewa kituoni hapo, huku waliobaki wakieleza kuishi kwa hofu.
Amesema kituo hicho, kilichoanzishwa mwishoni mwa 2023, kilikuwa kinahudumia jumla ya watoto 29—watoto 17 wakiishi kituoni na wengine 12 wakiishi nje ya kituo.
“Tayari watoto saba wameshahamishwa, bado 10, ambao leo tumeambiwa twende nao wote kwenye kituo cha Mtongani,” amesema.
Mlezi huyo amesema kati ya watoto watano wanaodaiwa kubakwa na mchungaji, wanne wanasoma sekondari na hawakai kituoni hapo, huku mdogo wao akiwa ni binti wa miaka 10 anayesoma shule ya msingi.
“Huyu mdogo anaishi hapa hapa. Mwanzoni alikuwa anakataa, lakini alipoulizwa zaidi ndipo akasema ni kweli. Nilimuuliza wakati anafanyiwa hivyo mama (mke wa mchungaji) alikuwa wapi? Akadai alikuwa akimuita usiku na kumfanyia.”

Amedai binti huyo alipelekwa kituoni hapo na maofisa wa ustawi wa jamii kwa maelezo kuwa alikokuwa akiishi alikuwa akifanyiwa ukatili wa kingono na binamu yake.
Ushuhuda wa mwalimu
Mwalimu wa malezi, Upendo Petro, amedai alipewa taarifa za binti huyo na wengine wanne kufanyiwa ukatili na mjumbe wa Kata ya Kawawa.
“Ilikuwa Januari 30, saa 9 kasoro alasiri, alikuja mjumbe wa Kata ya Kawawa akasema amesikia kuna mtoto anafanyiwa vitendo vya ukatili. Hakuwa anafahamu ni wa darasa gani, ila alimtaja jina. Tukaulizia darasa la pili hakuwepo, tukamkuta darasa la kwanza. Alihojiwa, akaeleza,” amesema.
Amedai siku iliyofuata, yeye, mwalimu mkuu na mwalimu mwingine walikaa na binti huyo ili kupata maelezo zaidi, na walipomuhoji alidai kufanyiwa vitendo hivyo.
“Tulimuuliza anafanyiwa wapi? Akadai kanisani kwa mchungaji kuna kochi. Tulipomdadisi zaidi, akadai kitendo hicho anafanyiwa kila siku, labda itokee siku hiyo mchungaji asiwepo,” amesema.
Kauli ya mchungaji msaidizi
Msaidizi wa mchungaji Stephano, Steve Masenga, ambaye naye ni mchungaji, amesema taarifa za kiongozi huyo kukamatwa ni za kweli.

“Hata sisi tunasikia kwamba anatuhumiwa kubaka, lakini hatujui kinachoendelea. Tumebaki kituoni, tunasubiri taratibu nyingine za polisi na ustawi wa jamii,” amesema.
Kwa upande wake, mjumbe wa nyumba 10 wa eneo hilo, Lucy Kigina, amesema wana taarifa za mchungaji huyo kutuhumiwa kubaka.
“Maadamu ziko polisi, basi tusubiri ifanye kazi yake, tutajua ukweli,” amesema.
Akielezea namna kituo hicho kilivyoanza, Lucy amesema Machi 2024, mchungaji Stephano alimfuata na kumwambia amtafutie watoto kwa kuwa alikuwa anaanzisha shule ya chekechea na kituo cha kulea watoto yatima.
“Nilimshirikisha mwenyekiti, akasema kama anafanya hivyo ni sawa. Ila mimi sikuridhika na mazingira. Januari mosi, 2025, nikaja nikakuta watoto wameongezeka. Nikampongeza mchungaji, lakini nikamhoji wanaishije kwenye nyumba hiyo? Akasema walishahama, hapo pamebaki ni kituo tu,” amesema.
Kauli za majirani
Baadhi ya majirani wa eneo hilo wamesema tangu kituo hicho kianzishwe, hawajakuwa na ukaribu nacho.
“Ni watu ambao tunawaona wanaingia na kutoka, hatuna ukaribu nao. Maisha yao ni wenyewe kwa wenyewe tu,” amesema Hidaya Juma.
Jirani mwingine, ambaye ni mfanyabiashara wa chapati mita 300 kutoka kituoni hapo, Hamida Rajabu, amesema hata watoto wa kituo hicho wakitumwa dukani, wanakwenda kwa kukimbia na kurudi kwa kukimbia.
“Hata wakija kununua chapati, ukiwaambia kuna foleni, huwa hawasubiri, wanaondoka. Kifupi, watu wa pale hawajichanganyi na majirani,” amesema.
Hata hivyo, mwalimu Vumilia amesema mchungaji huyo amekuwa akipita na kusalimia shuleni hapo mara kwa mara.
“Ni mtu mtaratibu. Nilimzoea kwa kuwa walikuwa wakija kuchota maji ya kisima hapa shuleni pale ikitokea ya Dawasa yamekatika. Sikuwahi kusikia matukio ya ajabu dhidi yake hadi lilipotokea hili,” amesema.