
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza leo Jumanne, Juni 10, kwamba mkutano ujao na Marekani kuhusu masuala ya nyuklia umepangwa kufanyika Jumapili huko Muscat, Oman.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Duru ijayo ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani imepangwa kufanyika Jumapili ijayo mjini Muscat,” msemaji wa wizara hiyo Esmaeil Baqaei amesema katika taarifa yake na kuongeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kiongozi mkuu wa ujumbe wa Iran katika mazungmzo hayo Abbas Araghchi “watazuru Norway Jumatano na Alhamisi.”
Rais wa Marekani Donald Trump hapo awali alisema kwamba mazungumzo haya yangefanyika siku ya Alhamisi, shirika la habari la AFP linaripoti.
Iran na Marekani zimekuwa na duru tano za mazungumzo tangu mwezi Aprili, chini ya upatanishi wa Oman, katika jaribio la kufikia makubaliano yaliyopangwa kuizuia Tehran kupata silaha za nyuklia kwa kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo vinavyodhoofisha uchumi wake.
Siku ya Jumatatu, Juni 9, Iran ilitangaza kwamba hivi karibuni itawasilisha pendekezo lake la makubaliano kuhusu suala la nyuklia la Iran kwa Marekani, baada ya kukosoa pendekezo la Marekani.
“Baada ya kukamilika, hivi karibuni tutapendekeza mpango wetu wenyewe kwa upande mwingine, kupitia Oman. Ni pendekezo la busara, la kimantiki, na lenye uwiano, na tunapendekeza kwa dhati kwamba upande wa Marekani uchukue fursa hii,” msemaji wa Wizara ya Mambo y Nje ya Iran Esmaeil Baqaei alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki mjini Tehran.