FAMILIA ya soka nchini imepata pigo jingine baada ya nyota wa zamani wa Nazareth ya Njombe, Simba, Mtibwa Sugar na Rayon Sports ya Rwanda, Geoffrey Mhando kufariki dunia asubuhi ya leo Jumapili, ikiwa ni siku chache tangu Mmiliki wa Kituo cha Alliance, James Bwire kuiaga dunia jijini Mwanza.
Bwire aliyekumbwa na mauti Januari 25 anatarajiwa kuzikwa leo Jumapili huko kijijini kwao wilayani Tarime, Mara, lakini kabla ya kufanyika kwa maziko hayo, mapema asubuhi hii wadau wa soka wamepata pigo jingine baada ya taarifa za msiba wa Mhando aliyefariki dunia baada ya kuugua ghafla.

Mwili wa Mhando aliyeng’ara miaka ya 2000, utahifadhiwa kesho mchana katika makaburi ya Mzambarauni yaliyopo Mbagala njia ya kwenda Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Katibu wa zamani wa timu ya Nazareth na mwanafamilia hiyo, Chris Kashililika aliliambia Mwanaspoti kuwa, Mhando aliumwa malaria na kulazwa kwa siku mbili katika hospitali ya Temeke hadi mauti yalipomfika asubuhi ya leo Jumapili.
“Jana jioni aliwaomba madaktari wamruhusu akaangalie mechi ya Yanga na Kagera Sugar, iliyokuwa ikipigwa KMC Complex, lakini walimkatalia walisema anatakiwa kupata mapumziko na aendelee na matibabu kwanza, licha ya kwamba hakuwa katika hali ya kuzidiwa,” amesema Kashililika na kuongeza;

“Umauti umemfika leo asubuhi, hivyo kama kuna wanamichezo wanataka kufika kujumuika nasi washuke kituo cha Mzambarauni, Mbagala njia ya kwenda Chamazi, tumeweka vibao vinavyoelekeza msiba ulipo.”
Kashililika amesema enzi za uhai wake, Mhando alikuwa anafundisha katika kituo cha TLFA walikuwa wanashirikiana na Emmanuel Gabriel na Kelvin Mhagama na mwaka huu alimaliza kozi ya Diploma B ya CAF.
“Lakini jambo jingine Mhando amewahi kuichezea timu ya taifa ya Rwanda mwaka 2001 alibadili jina na kuitwa Aziz Balinda, wakati huo wanacheza Rayon na wenzake kipa Chachala Muya, Gwakisa Mwandambo, Efraim Makoye na Mhagama,” amesema Kashililika.

Akiwa na Kituo cha Kukuza Vipaji cha Tigana Lukinja (TLFA), Mhando ndiye aliyekuwa pia skauti mkuu aliyekuwa akiibua na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana, kutokana na kuwa na jicho kali na enzi za uhai wake alitamba katika nafasi ya kiungo mshambuliaji kupitia timu hizo kabla ya kugeukia ukocha.