
BAADA ya Lucas Sendama kujiunga na Stand United ‘Chama la Wana’ katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu, mshambuliaji huyo amesema ni wakati sahihi kwake wa kupambana na kuirejesha heshima yake baada ya kuanza msimu vibaya.
Nyota huyo amerejea tena ndani ya kikosi hicho kwa mara ya pili baada ya kukitumikia msimu uliopita, ingawa Agosti mwaka jana alijiunga na ‘Wanajeshi wa Mpakani’ Biashara United, ambako hata hivyo, mambo yameenda tofauti na kuamua kurejea.
“Nimeamua kurudi sehemu ambayo naamini nitarejesha kiwango changu kama ilivyokuwa mwanzo, nilikuwa na malengo makubwa na Biashara United ila mambo yamekuwa tofauti na nilivyotegemea, nimeamua kujitafuta upya kwa miezi hii sita iliyobakia.”
Sendama alisema kurejea kwake Stand United sio changamoto kubwa kutokana na kutambua mahitaji ya timu hiyo, huku akiomba mashabiki kuendelea kuwapa sapoti, akiamini msimu huu unaweza ukawa bora kwao na kukirejesha kikosi hicho Ligi Kuu Bara.
Nyota huyo wa zamani wa Kurugenzi FC ya Simiyu na DTB ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars, tangu ajiunge na timu hiyo amekuwa na mwanzo mzuri ndani ya kikosi hicho cha kocha Juma Masoud baada ya kufunga mabao matatu katika michezo minne.