Nyongeza ya pensheni inapokabwa koo na kikokotoo

Miaka 21 iliyopita muungwana kutoka Kijiji cha Msoga ambaye sasa ni mstaafu, kama mstaafu wenu mpendwa, pamoja na kwamba ustaafu wao upo na tofauti sana kama mchana na usiku, aliamka siku moja na kuamua kuwapa nyongeza ya Sh50,000 wastaafu wake wa kima cha chini, waliokuwa wakipata pensheni ya Sh50,000 kwa mwezi, na nyongeza hiyo ikafanya tupokee pensheni ya Sh100,000 kwa mwezi.

Muungwana yule wa Msoga hakungoja miezi mitatu wala nini. Mwisho wa mwezi uleule aliotangaza nyongeza hiyo kwa wastaafu, ikaingia mifukoni mwa wastaafu bila hadithi nyingi. Tukumbuke miaka 21 iliyopita kaki moja ilikuwa ni pesa inayokuwezesha kuingia kwenye duka la Mpemba la mtaa na wateja uliowakuta wakamtaka mpemba akuhudumie wewe kwanza, kwa sababu laki ilikuwa pesa tofauti na miaka michache baadaye, wajukuu walipoigeuza laki kuwa si pesa!

Ndiyo, miaka 21 iliyopita wastaafu tuliokuwa kima cha chini tulichokiita cha chizi, tulitangaziwa kupata nyongeza ya Sh50, 000 kwenye pensheni yetu ya Sh50,000 tuliyokuwa tukipata kwa mwezi,  na mwisho wa mwezi huohuo nyongeza hiyo ikaingia kwenye mifuko yetu na kutufanya tupate pensheni ya shilingi laki moja kwa mwezi. Neno kikokotoo lilikuwa likiozea kwenye kamusi yetu tu!

Oktoba mwaka 2024 hatimaye siri-kali ikatangaza kuwapa wastaafu nyongeza ya pensheni baada ya miaka 21 ya kuomba na kuomboleza, ikitofautiana na alichofanya yule muungwana mstaafu kutoka Msoga ambaye aliwapa wastaafu nyongeza ya pensheni bila kusubiri kuombwa wala kubembelezwa na mtu.

Yeye aliona tu ni muda muafaka kuwapa nyongeza wastaafu, basi. Inasikitisha kwamba siri-kali haikuona muafaka kuwapa nyongeza ya pensheni wastaafu kwa miaka 21!

Nyongeza yenyewe kiduchu ikawekwa na mkwara mzito. Kwamba pamoja na kwamba imetangazwa Oktoba 2024, itawabidi wastaafu kusubiri miezi mitatu hadi Januari 2025 ndipo nyongeza hiyo itakapoingia mifukoni mwao! Wastaafu wakaishia kujiuliza kwa nini nyongeza kiduchu hiyo ya shilingi alfu hamsini tu ichukue miezi mitatu mizima kutayarishwa! Wangekuwa wameongezwa shilingi laki tano inayowastahili si wangeambiwa wasubiri mwaka mzima?

Miezi mitatu ikapita huku wastaafu wakipitisha sikukuu za ‘Tisa Desemba’ iliyoahirishwa, Krisimasi na hata mwaka mpya wakipiga miayo huku wakijipa matumaini ya kupokea pensheni mpya ya Sh150,000 au na zaidi, iliyokuwa inakuja kwenye mifuko yao. Ndiyo, mstaafu mwema wa Msoga aliwaongeza Sh50,000 miaka 21 iliyopita, kwa nini siri-kali ishindwe hivyo zaidi miaka 21 baadaye, Januari 2025?

Pamoja na kujiuliza sana kwa nini nyongeza hiyo itangazwe Oktoba halafu itolewe Januari, hakuna mstaafu yeyote aliyekumbuka kikokotoo kwa sababu kilikuwa hakituhusu sisi wa kale.

Yule Muungwana wa Msoga alitupa nyongeza ya Sh50,000 bila kikokotoo kilichokuwa bado kiko darini kikiota ukungu tu, kwa nini siri-kali ikihusishe na nyongeza yetu miaka 21 baadaye, hata kama kimetolewa ukungu!

Mwisho wa mwezi wa Januari ukafika na wastaafu wakakiona kilichomtoa kanga manyoya, kama sio kilichomfanya nyoka, mkubwa mzima wa kutembea mpaka leo bado anatambaa! Pensheni ilikuwa ileile ya Laki si Pesa…huku kila mstaafu akipata shilingi elfu saba, tisa au kumi, lakini bila nyongeza ya elfu hamsini iliyoahidiwa wala nini!

Siri-kali ilikuwa imetekeleza kile lilichokisema kwa mbwembwe wakati inatangaza nyongeza ya mstaafu kuwa ni katika juhudi za kumjali mstaafu na kumwezesha kupambana na hali ngumu yake ya maisha, lakini hapo hapo inaruhusu nyongeza yake hiyo ikabwe koo na kikokotoo kifanye vitu vyake na wastaafu wabaki na buku saba au tisa badala ya shilingi alfu hamsini! Huku ni kumjali mstaafu wa taifa?

Hatujaambiwa rasmi lakini inaelekea ndivyo ilivyo, ndio maana wahusika wameuchuna tu na hakuna anayejitokeza kuwaambia ukweli wastaafu kuwa nyongeza yao ya Sh50,000 imepitiwa na kikotoo na sasa wamepata hizo walizopata! Hivi inakuwaje umpe mstaafu nyongeza ya shilingi alfu hamsini baada ya miaka 21 ya kulia na kuomboleza, halafu uruhusu kikotoo kiifyeke nyongeza hiyo na kumuachia buku saba, yaani pensheni ya shilingi Laki moja na elfu saba?

Hivi unamkataje nyongeza yake ya pensheni mstaafu wa umri wa miaka 75 na kuendelea ili nchi iokoe  nini? Wahusika mbona hamna huruma hivyo? Hivi mngeiacha hiyo shilingi elfu hamsini kama yule Muungwana wa Msoga miaka 21 iliyopita, na kumfanya mstaafu ajiendee zake Kinondoni kwa amani miaka michache iliyobaki, nchi ingekuwa imepata hasara gani?  Wastaafu wenyewe wa kima cha chini wamebaki wangapi?

Tuna wawakilishi wa wananchi zaidi ya 350 kule Dodoma ambao kila mmoja anapokea shilingi milioni 14 kwa mwezi ambazo ukijumlisha marupurupu na marapurapu yao ni shilingi…mama wee!…karibuni milioni 16 kwa mwezi zisizokatwa kodi, rudia hapo, zisizokatwa kodi! Halafu watu hawana huruma wanaacha kikokotoo kifanye vitu vyake kwenye nyongeza ya pensheni ya Sh50,000, na hakuna hata muwakilishi wa wananchi anayekohoa!

Kikokotoo sasa kikate kodi mishahara ya kutisha ya wawakilishi wa wananchi na nyongeza ya Sh50,000 ya wastaafu irudishwe haraka kwao!

 0754 340606 / 0784 340606