
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ameitaka wizara husika kushirikiana kwa karibu na vyama vya wafanyakazi pamoja na waajiri, kuendeleza majadiliano ya kina na ya mara kwa mara ili kuhakikisha hoja na changamoto zinazowakabili wafanyakazi zinapatiwa suluhisho la kudumu.
Ametoa maagizo hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa leo, Mei Mosi, 2025 katika viwanja vya Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.
“Endeleeni kukaa vikao vya wadau, punguzeni hoja hizi na muwe mnanipa taarifa kila hatua mnayofikia. Mkikwama, leteni kwangu. Ninaamini hakuna hoja itakayoshindikana,” amesema Dk Mwinyi.
Amesisitiza kuwa mafanikio na maendeleo ya Zanzibar yanachangiwa moja kwa moja na jitihada za wafanyakazi, hivyo Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.
Kuhusu nyongeza ya mishahara kwa mwaka huu, Dk Mwinyi amesema suala hilo litategemea hali halisi ya bajeti ya Serikali, hasa ikizingatiwa kuwa mwaka huu nchi itafanya uchaguzi mkuu, ambao unahitaji matumizi makubwa ya fedha.
“Kila mwaka tuna utaratibu wa kuongeza mishahara, lakini mwaka huu tusubiri tuone bajeti yetu itakuwaje. Kama mnavyojua, tuna uchaguzi mkuu unaotumia bajeti kubwa,” amesema na kuongeza:
“Nimeelekeza Wizara ya Fedha kufanya tathmini ya kina kuona kiasi gani kinaweza kutengwa kwa ajili ya nyongeza ya mishahara, kulingana na hali ya kifedha ya Serikali.”
Ameongeza kuwa iwapo wataendelea kuongoza baada ya uchaguzi, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi kubwa zaidi, huku maslahi ya wafanyakazi yakiendelea kupewa kipaumbele.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi, Uchumi na Uwekezaji), Shariff Ali Shariff, amesema Serikali imefanya vikao vitano na wadau mbalimbali, ambapo hoja 16 zimejadiliwa, kati ya hizo, 11 ziliwasilishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc) na tano na Umoja wa Waajiri Zanzibar (Zanema).
Amesema mazungumzo hayo yanaendelea, na kwamba hoja nyingi ziko katika hatua nzuri za utekelezaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Zatuc, Khamis Mwinyi, amesema licha ya kuipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua katika kutekeleza baadhi ya hoja zilizoibuliwa mwaka jana, ameibua hoja mpya 10 zinazogusa masilahi ya wafanyakazi visiwani humo.
Miongoni mwa hoja hizo ni wito kwa Serikali kumaliza malipo ya madeni kwa wafanyakazi waliohamishwa wakati wa utekelezaji wa mchakato wa ugatuzi wa mamlaka, ambao hadi sasa bado hawajapata haki zao kikamilifu.
Aidha, ameitaka Serikali kufikiria upya muundo wa vyuo vya elimu ya kati, akiomba vigatuliwe kutoka vyuo vikuu kwa madai kuwa vinapokaa chini ya vyuo vikuu, havitoi taaluma ya kutosha, bali vinawandaa vijana kutafuta kazi bila kuwa na ujuzi wa kutosha.
Katika hatua nyingine, katibu huyo amependekeza kuanzishwa kwa posho ya kuanzia kwa wafanyakazi wapya, akieleza kuwa wengi wao wanakumbana na changamoto za kifedha baada ya kuajiriwa, hali inayowaathiri kimaisha na kitaaluma.
Kuhusu wafanyakazi waliopo chini ya kampuni, hasa zile za wakandarasi, amesema bado kuna idadi ya wafanyakazi ambao hawajalipwa stahiki zao, licha ya kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea Zanzibar.
Ameongeza kuwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika mazingira magumu wanahitaji kupewa kipaumbele, akisema mishahara yao kwa sasa hulipwa kwa mzunguko wa Aprili hadi Aprili, mfumo ambao unahitaji mapitio ili uendane na hali halisi ya maisha.
Katibu huyo pia ameibua changamoto zinazowakumba wafanyakazi wanaohamishwa kutoka ofisi moja kwenda nyingine, akisema wengi wao wanapowasili vituo vipya hawapewi majukumu rasmi, hali inayowalazimu kurudi makao makuu ya utumishi kufuatilia hatma yao.
Hoja nyingine iliyoibuliwa ni ya kuongeza siku za likizo kwa wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti, akieleza kuwa siku 100 zinazotolewa sasa hazitoshelezi, hivyo Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza muda huo kwa kuzingatia mahitaji ya kiafya na malezi ya watoto hao.
Pia, amelitaja deni la muda mrefu linalowakabili waliokuwa wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano waliokuwa wakihudumu katika viwanja vya michezo, ambao hadi sasa bado hawajalipwa stahiki zao.
Licha ya hoja hizo, katibu huyo amewahimiza wafanyakazi kuendelea kudai haki zao kwa kufuata njia halali na zilizowekwa kisheria, huku wakitimiza wajibu wao kazini kwa weledi na uadilifu.
Ametoa tahadhari kwa baadhi ya wafanyakazi wanaotumia njia zisizotambuliwa na sheria katika kudai haki zao, akisisitiza kuwa njia hizo zinaweza kuwaathiri na kuwanyima haki zao halali, huku akisisitiza kuwa sheria imeelekeza utaratibu sahihi wa kudai haki.