Nyimbo maarufu Bongo zilizotengenezwa na Miikka Mwamba

Dar es Salaam. Ukubali au ukatae, ukweli utabaki kuwa Miikka ‘Mwamba’ Kari akiwa kama Prodyuza naye alichangia kwa sehemu kubwa katika ukuaji wa muziki wa Bongo kuanzia katikati mwa miaka ya 1990 hadi 2000.

Mwamba anatokea Finland na akaja Bongo kufanya mapinduzi akishiriki kutengeneza nyimbo kibao kali hadi kushinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) na kuwa Jaji wa shindano la Tanzania Pop Idols. Huyu ndiye Miikka Mwamba.

Mwaka 1993 ndipo Miikka Mwamba alikuja nchini kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa vitendo (field) baada ya kuhitimu Chuo Kikuu aliposomea sanaa. Akiwa hapa alifanya kazi kwa ukaribu na marehemu John Komba katika bendi ya TOT.

Baadaye alirejea Tanzania akitafuta sehemu ya kufanya kazi kama Prodyuza, kwa mara ya kwanza akiwa na rafiki yake wakaenda MJ Records kutafuta nafasi ila wakamkosa Master J na mwisho wa siku akapata kazi FM Studio.

                     

Pale FM Studio aliajiriwa, hivyo alikuwa hachukui fedha kwa wasanii bali alikuwa analipwa mshahara kama mfanyakazi mwingine kuanzia mwaka 1999 hadi 2004 ulipomalizika mkataba wake na kurejea kwao ili kuwa karibu na familia yake.

Wimbo wa Dully Sykes ‘Julieta’ ndio ulimtambulisha Miikka katika Bongofleva kisha wasanii wengine kama Daz Nundaz, Saida Karoli, Mad Ice, Dudu Baya, Banana Zorro, Hardmad n.k ndipo wakaenda kurekodi kwake nyimbo zilizofanya vizuri.

Hata hivyo, moja ya nyimbo zilizoliweka juu zaidi jina la Miikka ni ‘Barua’ wa kundi la Daz Nundaz ambao wanatajwa kuwa wasanii wa kwanza kutambulisha muziki wa kuimba katika Bongofleva baada ya utawala wa muda mrefu wa rap.

Wimbo uliomtoa kimuziki Banana Zorro, Mama Yangu (2003) aliutengeneza Miikka Mwamba ambaye alibadilisha kila kitu ambacho Banana alitaka kiwepo katika wimbo huo kisha akaja na ufundi wake uliopelekea ngoma hiyo kubamba.  

Mwaka 2003 wakati Dudu Baya anasoma Nairobi, Kenya ndipo aliandika wimbo wake, Nakupenda Mpenzi (Tentemente), aliporudi Bongo akaurekodi kwa Miikka Mwamba na kumshirikisha Vivian Tillya.

Licha ya kazi zake kuwa maarufu sana, Miikka hakupenda kuwa mbele ya kamera ndio sababu ya uchache wa picha zake katika mitandao. Aliamini anayepaswa kupiga picha kila mara ni wasanii kwa sababu ya kujitangaza na kazi zao ila sio yeye Prodyuza.

                    

Miikka Mwamba ndiye Prodyuza wa kwanza kurekodi wimbo wa Shetta ambaye wakati huo alikuwa darasa la nne, huku Ali Choki akijitolea kumlipia msanii huyo aliyetoka na kundi la Darstamina gharama za kurekodi.  

Miongoni mwa nyimbo alizoshiriki kutengeneza Miikka Mwamba ni Eno Maiki (Ziggy Dee), Babygal (Mad Ice), Kamanda (Daz Nundaz), Kwenye Chati (Balozi Dola Soul), Mkiwa (K Sal), Kitu Gani (D Knob), Maria Salome (Saida Karoli),  Tamala (Hardmad), Mama (Banana Zorro) n.k.