
HUTOKEA mara chache mno katika soka, lakini utani wa jadi wa Simba na Yanga ni zaidi ya burudani, kwani mwaka 1988 Wekundu wa Msimbazi waliponea kushuka daraja kwa msaada wa watani wao hao.
Ndiyo, baada ya kunusuriwa na Tukuyu Stars msimu wa 1987 kwa kufungana 5-5 na Simba kuepuka kushuka, msimu wa 1988, Yanga ilisamehe ubingwa ili wamwokoe mtani kwa kukubali kipigo cha 2-1 katika mechi iliyopigwa Julai 23, 1988, bao la ushindi likifungwa na John Makelele ‘ZigZag’ baada ya kusetiwa mpira na kipa Sahau Kambi aliyeshindwa kuudaka mpira wa kichwa cha Malota Soma dk 58.
Kitu cha ajabu ni, Yanga ilikuwa inahitaji sare ibebe ubingwa msimu huo ikichuana na Coastal ambayo ililala 2-0 kwa African Sports, lakini kipigo cha 2-1 mbele ya Simba, kiliifanya Wagosi wabeba taji kwa tofauti na mabao, ila furaha ni Simba ikiponea kwa mara ya pili mfululizo kushuka.
Msimu wa 1989, Simba ikiwa bado hali mbaya iliokoka kushuka daraja baada ya sare ya 1-1 na African Sports yenye uhusiano na Yanga, kama sivyo huenda leo ingekuwa ni histori nyingine kwa Mnyama.