King Kibadeni kiboko
HUWEZI kuamini, lakini ndivyo ukweli ulivyo, imepita miaka 47 na miezi saba na siku kadhaa tangu mshambuliaji nyota wa Simba, Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’ alipofunga hat trick ya kwanza na ya pekee katika mechi za Dabi ya Kariakoo.
Kibadeni alifunga mabao hayo matatu katika mechi iliyopigwa Jumanne ya Julai 19, 1977 akifunga dakika ya 10, 42 na 89 ambapo Simba iliifumua Yanga 6-0. Seleman Sanga alijifunga dakika ya 20 na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ alifunga dakika ya 60 na 73.

Kama hujui hadi sasa zimeshapigwa dabi 102 tangu mechi hiyo iliyokuwa la 11 na hakuna nyota yeyote aliyeifikia rekodi hiyo ya Kibadeni ambaye hakuwahi kufunga tena katika dabi hadi anastaafu soka.
Ni Pazi na Kaseja tu
LICHA ya kupigwa dabi 113 za Ligi ya Bara tangu 1965, lakini ni makipa wawili tu waliowahi kufunga mabao katika mechi hizo, kila mmoja akifunga mkwaju wa penalti, halafu wote wakiichezea Simba.
Alianza Idd Pazi ‘Father’ katika mechi ya Machi 10, 1984 alipoitanguliza Simba kwa mkwaju wa penalti wa dk 20 kabla ya Abeid Mziba ‘Tekero’ kuchomoa dk 39 na pambano hilo kuisha kwa sare ya 1-1.

Juma Kaseja alikuja kujibu mapigo Mei 6, 2012 katika ushindi wa 5-0 , Simba ikiiua Yanga, kipa huyo akifunga bao la nne dakika 69, Emmanuel Okwi akifunga mawili dakika ya 1 na 65, Patrick Mafisago dakika ya 58 na Felix Sunzu dakika 74 kila mmoja akifunga kwa alifunga penalti.
Dabi 113, penalti 15
DABI ya Kariakoo sio mchezo, kwani licha ya kupigwa mechi 113 katika Ligi ya Bata tangu mwaka 1965, zimeshuhudiwa penalti 15 pekee, huku ni mchezo mmoja pekee wa Mei 6, 2012 ndipo ulioshuhudiwa zikipigwa tatu wakati Yanga ikifungwa mabao 5-0.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hashim Abdallah ambaye anafahamika kama ni Yanga damu n aliwahi kushiriki uchaguzi wa klabu hiyo, alitoa penalti hizo zilizofungwa na Patrick Mafisango, Juma Kaseja na Mzambia Felix Sunzu.
Wazawa na kapu la mabao
INASHANGAZA sana. Katika mechi 113 za Dabi ya Kariakoo zilizochezwa Bara tangu 1965, makipa wazawa ndio wamekuwa wahanga wa kupigwa mabao mengi katika mechi za vipigo vikubwa, kuanzia ile ya Juni 1, 1968 pale Yanga ilipoinyoosha Simba kwa mabao 5-0. Kipa aliyebebeshwa kapu la mabao alikuwa ni Mbaraka Salum, aliyeingia katika rekodi ya kuwa kipa wa kwanza kula ‘mkono’ katika dabi.
Mechi ya Julai 19, 1977, kipa wa Yanga aliyebugia mabao sita alikuwa ni; Bernard Madale aliyekaa katika milingoni mktatu ya Yanga akiwa ndiye kipa pekee aliyeruhusu mabao mengi zaidi.
Kipa aliyefuata alikuwa ni Said Mohammed ‘Nduda’ wa Yanga aliyepokea mabao manne katika kipigo cha 5-0, Mei 6, 2012 baada ya Mghana Yew Berko kupigwa bao moja na ‘kujivunja’, huku Aishi Manula wa Simba alifunga hesabu kwa kutunguliwa pia ‘mkono’ wakati Yanga ikishinda 5-1, Novemba 5, 2023.
Kwa rekodi hizo ni kama vile Diarra Djigui (Yanga) na Moussa Camara (Simba) wapo salama Machi 8.
Yanga ni wazee wa kuazima!
ACHANA na kitendo cha kuanzimwa nyota watatu kutoka Simba, Monja Liseki, Shaaban Ramadhani na Alphonce Modest kwa ajili ya kuwatumia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998, rekodi zinaonyesha Yanga na ishu za kuazima wachezaji ni kama uji na mgonjwa.
Mwaka 1968 katika Dabi ya Kariakoo ambayo Yanga ilishinda 5-0, iliwaazima wachezaji wawili, Saleh Zimbwe kutomka African Sports ya Tanga na Gilbert Mahinya kutoka Sunderland (Simba) na hata mwaka 1988 ilimuazima Abubakar Salum ‘Sure Boy’ kutoka Sigara ili imtumie katika michuano ya Klabu Bingwa kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup). Unaweza kuwaita wazee wa kuazima.
Keegan ndiye mkali wao
PAMOJA na kupigwa Dabi ya Kariakoo 113 kuanzia mwaka 1965-2024, lakini unaambiwa ni Omar Hussein ‘Keegan’ ndiye nyota anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi wa muda wote katika Dabi ya Kariakoo, akitupia sita na zote ni dhidi ya Simba. Keegan alihamia Simba baadae lakini hakuongeza idadi hiyo ya mabao, akifuatiwa na nyota wawili wote wakiwa ni wa Simba, Edward Chumila na Dua Said walikuwa na zali la kuitungua Yanga kila mmoja akiwa na mabao matano, huku kukiwa na mastaa wengine wliofunga mabao manne kama Sekilojo Chambua, Said Mwamba ‘Kizota’, Abeid Mziba, Mussa Hassan Mgosi, Jerson Tegete na Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio.