Nyakati za majonzi Bunge la 12, wabunge 10 wakifariki dunia-2

Dodoma. Bunge la 12 la Tanzania litahitimisha uhai wake wa miaka mitano (2020-2025), baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia na kulivunja Juni 27, 2025.

Safari ya Bunge hili ilianza Novemba 2020 baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huo.

Bunge la 12 lilizinduliwa Novemba 13, 2020 na Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Aliyekuwa Makamu wa Rais, wakati huo, Samia aliapishwa kushika wadhifa wa Rais Machi 19, 2021.

Katika uhai wa Bunge la 12, Taifa limepoteza wabunge 10 waliohudumu bungeni na kutoa mchango mkubwa katika utungaji wa sheria na uwakilishi wa wananchi.

Kuondoka duniani kwa viongozi hao kumeacha urithi utakaoendelea kukumbukwa katika maendeleo ya Taifa kwa namna walivyoacha alama katika nyanja za kisiasa.

Vifo vya watunga sera hawa baadhi wakihudumu nafasi za waziri na naibu waziri vilitokana na sababu za maradhi na wengine ajali za barabarani.

Waliofariki dunia ni Atashasta Nditiye wa jimbo la Muhambwe, Elias Kwandikwa (Ushetu), Francis Mtega (Mbarali), William Ole Nasha (Ngorongoro), Khatib Said Haji (Konde) na Mussa Hassan Mussa, (Amani).

Wengine ni Ahmed Yahaya Abdulwakil (Kwahani), Dk Faustine Ndugulile (Kigamboni), Irene Ndyamkama na Martha Umbula (wabunge wa Viti maalumu).

Martha aliyekuwa mbunge wa viti maalumu mkoani Manyara alifariki dunia Januari 20, 2021 katika Hospitali ya HCG Mumbai nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kwandikwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alifariki dunia Agosti 2, 2021 akipatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.

Kwandikwa aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akishughulikia ujenzi kati ya Agosti 9, 2017 hadi mwaka 2020.

Ole Nasha alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji. Kifo chake kilielezwa kilitokea kutokana na shinikizo la damu.

Katika utumishi wake bungeni kwa miaka sita, alitoa hoja 16, maswali ya msingi 166 na nyongeza 318.

Ole Nasha aliyefariki dunia Septemba 27, 2021 akiwa nyumbani kwake Mtaa wa Medeli jijini Dodoma alizikwa kwao Ngorongoro Oktoba 2, 2021.

Aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mei 20, 2021, Bunge lilipokea taarifa ya kifo cha Khatib Said Haji, kilichotokea saa 11:45 alfajiri ya siku hiyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. Alizikwa siku hiyohiyo Kisiwani Pemba. Alifikishwa Muhimbili Mei 10, 2021.

Irene aliyekuwa mbunge wa viti maalumu mkoani Rukwa, alifariki dunia Aprili 24, 2022 katika Hospitali ya Tumbi wilayani Kibaha mkoani Pwani alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mbunge wa Amani, Mussa Hassan Mussa alifariki dunia Oktoba 13, 2022 nyumbani kwake Zanzibar, huku mbunge wa Kwahani, Abdulwakil alifariki dunia Aprili 8, 2024, visiwani humo kutokana na shinikizo la damu na kuzikwa Aprili 9, kijijini kwao Buyuni, Zanzibar.

Dk Ndugulile alifariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kifo chake kilitokea miezi michache baada ya kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Dk Ndugulile, Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo, alikuwa aanze kazi WHO Machi 2025.

Aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kati ya mwaka 2017 hadi 2020 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kati ya Desemba 2020 hadi Aprili 2021.

Waliofariki kwa ajali

Mbunge wa Mbarali, Mtega alifariki dunia Julai Mosi, 2023 kwa ajali ya pikipiki aliyokuwa akisafiria kutoka shambani kwake kurejea nyumbani iliyogongana na trekta katika Tarafa ya Ilongo, Kata ya Chimala mkoani Mbeya.

Pikipiki hiyo aina ya boxer alikuwa akiiendesha mwenyewe.

Februari 10, 2021 wabunge walipokea taarifa ya kifo cha mbunge Nditiye ambaye alipata ajali ya gari.

Mbunge huyo aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, alipata ajali ya gari eneo la Nanenane, Nzuguni mkoani Dodoma Februari 12, 2021.

Alifariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Katika wizara hiyo Nditiye alishughulikia masuala ya mawasiliano kuanzia Oktoba, 9, 2017 hadi 2021.

Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Nafasi zilivyojazwa

Katika uchaguzi uliofanyika Mei 17, 2021 wananchi wa Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma walimchagua Dk Florence Samizi kuchukua nafasi iliyoachwa na Nditiye kwa kura 23,441 kati ya kura 35,339 zilizopigwa katika uchaguzi huo.

Emmanuel Cherehani alishinda uchaguzi jimbo la Ushetu kwa kura 103,357 kati ya 106,945 zilizopigwa, huku Mohamed Said Issa alijaza nafasi ya Konde katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 9, 2021 baada ya kupata kura 2,391 kati ya 3,338 zilizopigwa katika uchaguzi huo.

Katika uchaguzi mdogo uliofanyika Mbarali, Bahati Nyimbo aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, alichaguliwa kuwa mbunge jimboni humo Septemba 19, 2023 baada ya kupata kura 44,334 kati ya 56,095 zilizopigwa.

Jimbo la Ngorongoro, Emmanuel Shangai alichaguliwa kwa kura 62,017 kati ya 62,528 zilizopigwa Desemba 11, 2021.

Jimbo la Amani nafasi ilijazwa na Abdul Yusuf Maalim baada ya kushinda kwa kura 4,242 kati ya 5,042 zilizopigwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba 17, 2022, huku Kwahani nafasi ikijazwa na Khamis Yussuf Mussa kwa kura 7,092 kati ya 7,383 zilizopigwa katika uchaguzi huo.

Kwa upande wa viti maalumu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilimteua Aziza Ally Sleyum kujaza nafasi ya Bahati Ndimbo, huku Tamima Haji Abass akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Irene Ndyamkama na nafasi ya Martha Umbula ilijazwa na Yustina Rahhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *