Nusu fainali ya vigogo Ulaya, Ronaldo, Lamine na Mbappe

Paris, Ufaransa. Timu za Ufaransa, Hispania, Ujerumani na Ureno zimefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya

UEFA Nations League baada ya kushinda michezo yao ya hatua ya robo fainali juzi.

Hispania ambao ni mabingwa watetezi walikuwa na wakati mgumu baada ya kusubiri hadi hatua ya matuta ili kupata tiketi iliyowapeleka nusu fainali ya michuano hiyo kwenye mchezo mgumu dhidi ya Uholanzi ambao walionekana kuwa bora kwa muda wote uwanjani.

Katika mchezo huo timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3 na kuwa na matokeo ya jumla ya 5-5 ambayo yaliwapeleka kwenye mikwaju ya penalti iliyoipa Hispania ushindi wa mikwaju 5-4 na sasa wanasubiri kuvaana na Ufaransa kwenye mchezo wa nusu fainali utakaopigwa Juni 4, mwaka huu.

Ufaransa ambao walikuwa hawapewi nafasi kubwa, walifanikiwa kuingia hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Croatia na kufanya matokeo kuwa 2-2, ambapo walikwenda kwenye mikwaju ya penalti na Wafaransa hao wakaibuka na ushindi wa mikwaju 5-4.

Sasa wanatarajiwa kuvaana na Hispania kwenye mchezo wa nusu fainali ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote kutokana na upinzani uliopo wa timu hizo. Katika michezo kumi ya hivi karibuni ambayo timu hizo zimekutana, Hispania inaonekana kuwa kinara ikishinda sita, sare mmoja na kupoteza mitatu.

Mechi nyingine kali ya hatua ya nusu fainali itawashuhudia wababe wawili, Ujerumani ambao watavaana na Ureno, ikiwa ni mechi nyingine inayosubiriwa kwa hamu kubwa.

Ujerumani ilipata nafasi ya kutinga hapa baada ya kuiondoa Italia kwa jumla ya mabao 5-3 baada ya sare ya 3-3 kwenye mchezo wa mwisho juzi.

Sasa itatakiwa kuhakikisha inaonyesha umwamba wake kwa wapinzani waop Ureno ambao hawakuwa na kazi ndogo kufika kwenye hatua hii wakifanikiwa kuitupa nje Denmark baada ya kuichapa mabao 5-2 na kuondoa kwenye mashindano hayo kwa ushindi wa jumla wa 5-3 baada ya kupoteza kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza.

Katika michezo mitano ya hivi karibuni, Ujerumani wanaonekana kuwapoteza Ureno baada ya kushinda yote.

Washindi wa hatua ya nusu fainali watafanikiwa kucheza mchezo wa fainali Juni 8 nchini Ujerumani, hii itakuwa fainali ya nne ya michuano hiyo na timu zitakazopoteza nusu zitawania nafasi ya tatu siku hiyohiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *