Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeanika mafanikio lukuki ya ufanisi kiutendaji ambayo yamepatikana katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia mafanikio hayo, Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, anasema Mfuko unaendelea kusimamia vizuri shughuli za hifadhi ya jamii kwa kuifikia sekta binafsi na sekta ya waliojiajiri.
Katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia, Umma wa Watanzania umeendelea kupata elimu kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye kwa kujiunga na kuchangia NSSF.
Aidha, kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, Bw. Mshomba anasema NSSF wanaungana na Watanzania wote kumpongeza na kumshukuru Mhe. Dkt. Samia kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika kuongoza nchi ambapo sasa anatimiza miaka minne tokea alipoapishwa kushika wadhifa huo.
“Napenda kutumia fursa hii kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo kwa Watanzania ambapo katika uongozi wake tunashuhudia akiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati. Kwa upande wa NSSF, miradi hiyo imekuwa ni fursa kwetu kupata wanachama pamoja na kukusanya michango,” anasema Bw. Mshomba.
Kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii kwa ujumla, Bw. Mshomba ameeleza kuwa Watanzania ni mashuhuda wa namna ambavyo Mhe. Rais Dkt. Samia ameisimamia vizuri na kuwa na ufanisi mkubwa katika kipindi ambacho amekuwa madarakani.
NSSF inatekeleza majukumu makuu manne ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama kwa mujibu wa Sheria ya NSSF, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao. Kwa mujibu wa sheria, wanaotakiwa kuandikishwa kuwa wanachama wa NSSF ni wafanyakazi walioajiriwa katika sekta binafsi, raia wa kigeni wanaofanya kazi Tanzania Bara, watumishi wa taasisi za kimataifa zinazofanya kazi Tanzania Bara na wananchi waliojiajiri.
Ongezeko la wanachama, uwekezaji na ukuaji wa mfuko
Akizungumzia mafanikio ya NSSF kwa upande wa uandikishaji wanachama, Mshomba anasema Mfuko unaendelea kutambua na kuandikisha wanachama wapya katika sekta binafsi na sekta ya waliojiajiri, ambapo katika kipindi cha miaka minne (Machi, 2021 mpaka Februari, 2025) ya Serikali ya awamu ya sita, NSSF imeandikisha jumla ya wanachama wapya 1,052,176.
Kwa upande wa ukusanyaji michango, Mshomba anasema kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali ya awamu ya sita kuvutia uwekezaji na kufungua fursa mpya za biashara pamoja na jitihada za NSSF kuboresha utendaji wake, Mfuko umeongeza uwezo wake wa kukusanya michango ambapo jumla ya shilingi trilioni 6.99 zimekusanywa kutoka kwa wanachama.
Aidha, wastani wa makusanyo ya michango kwa mwezi yameongezeka kutoka trilioni 1.13 katika mwaka ulioishia mwezi Februari 2021 hadi kufikia trilioni 2.15 mwezi Februari 2025, sawa na ongezeko la asilimia 90.

Daraja la Kigamboni ni moja ya miradi iliyotekelezwa na NSSF.
Mshomba anasema katika kipindi cha miaka minne, thamani ya Mfuko imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.8 mwezi Februari 2021 na kufikia trilioni 9.2 mwezi Februari 2025, sawa na ongezeko la asilimia 92.
Anasema, tathimini inaonesha hali ya ustahimilivu wa Mfuko ni asilimia 90.7 kwa kipindi kilichoishia mwezi Juni 2023 ukilinganisha na asilimia 87.7 iliyokuwepo katika tathimini ya kipindi kilichoishia mwezi Juni 2020. Hali hii inaashiria uhai na uendelevu wa Mfuko. Aidha, Mfuko umeendelea kulipa kodi ya Serikali kwa mujibu wa sheria na hivyo kuchangia katika kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa hapa nchini.
Mshomba anasema Mfuko umelipa kodi ya shilingi bilioni 380 ambayo ni sawa na wastani wa shilingi bilioni 75 kwa mwaka. Aidha, katika siku ya walipa kodi, Mfuko ulitunukiwa tuzo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya mlipa kodi mzuri kwa hiari kitaifa kwa mwaka 2023/24.
Malipo ya mafao
Mshomba anasema katika kipindi cha miaka minne, Mfuko ulilipa mafao ya shilingi trilioni 3.10 na malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69 kutoka shilingi bilioni 537.08 katika mwaka ulioishia mwezi Februari 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 909.16 mwezi Februari 2025.
Anasema katika mabadiliko ya kanuni ya ulipaji mafao ya kustaafu (KIKOKOTOO) yaliyofanyika na kuanza kutekelezwa mwezi Julai, 2022 wastaafu wa NSSF walianza kupokea mkupuo wa awali wa asilimia 33 ukilinganisha na asilimia 25 waliokuwa wakilipwa kabla ya mabadiliko hayo. Aidha, kutokana na Serikali ya awamu ya sita kuwajali wastaafu, Mfuko umeendelea kuboresha tena ulipaji wa mafao kwa wanachama wote waliokuwa wanalipwa mkupuo wa awali wa asilimia 33 na kufikia asilimia 35. Ongezeko hili lilifanyika kwa wastaafu wote waliostaafu kuanzia mwezi Julai, 2022.
“Uamuzi huu wa Serikali wa kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kwa wanachama wa NSSF pia umezingatia uendelevu wa Mfuko,” anasema Bw. Mshomba.
Anasema Mfuko katika hatua za mwisho za kuboresha kiwango cha kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000. Viwango vingine vya pensheni vinatarajiwa pia kuongezeka kwa kati ya asilimia 2 na asilimia 20.
Maboresho ya huduma na matumizi ya Tehama
Kuhusu maboresho ya huduma na matumizi ya TEHAMA, Mshomba anasema Mfuko umefanya maboresho mbalimbali katika utendaji ili kuwezesha wanachama kupata huduma mbalimbali kwa urahisi na kupunguza usumbufu, ambapo moja ya hatua hizo ni kuanzishwa kwa mikoa ya mipya ya huduma ya Ubungo na Kigamboni, Dar es Salaam pamoja na kupandishwa hadhi vituo vitatu vya Mkuranga, Hai na Mbezi Beach kuwa na hadhi ya ofisi za wilaya.
Bw. Mshomba anasema kwa kuzingatia matumizi ya TEHAMA ni moja ya maeneo yanayotiliwa mkazo na Serikali ya awamu ya sita, Mfuko umebainisha eneo hilo kuwa la kipaumbele ambapo baadhi ya maboresho ya mifumo yamewezesha waajiri na wanachama wa NSSF kujihudumia na kupata huduma mbalimbali kupitia mifumo ya TEHAMA, pasipo kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
“Matumizi ya TEHAMA katika utendaji wa Mfuko yameongezeka kutoka asilimia 48 iliyokuwa imefikiwa mwezi Februari 2021, hadi kufikia asilimia 87.5 mwezi Februari 2025, ikitarajiwa kufikia asilimia 100 ifikapo mwezi Juni 2025,” anasema Bw. Mshomba.
Mradi wa Mkulazi
Akizungumzia mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi, Mshomba anasema Mfuko kupitia kampuni tanzu ya Mkulazi, umekamilisha ujenzi wa kiwanda hicho. “Kiwanda hiki kilizinduliwa tarehe 7 Agosti 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya uzalishaji wa sukari ya majumbani kuanza rasmi mwezi Julai 2024,” anasema Bw. Mshomba.
Anasema hadi kufikia mwezi Februari 2025 tani 19,124 za sukari ya majumbani zilikuwa zimezalishwa na kupelekwa sokoni. Kiwanda kimetoa fursa za ajira 8,302 ambapo ajira za moja kwa moja ni 1,665 na zisizo za moja kwa moja ni 6,637. Matarajio ni kwenda kutoa fursa za ajira zaidi ya 11,315 ya baada ya uzalishaji sukari kufikia kiwango cha juu. Aidha, mradi huo pia unatarajiwa kuzalisha megawati 15 za umeme ambazo kati yake megawati 7 zinatarajiwa kuingizwa katika gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupokelea na kupoza umeme cha Msamvu Morogoro.
Kuwaondolea kero Wananchi wa Kigamboni
Mshomba anasema Mfuko unaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwaondolea kero wananchi wa Kigamboni ambao walikuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu viwango vya tozo walizokuwa wakilipa wanapovuka Daraja la Nyerere, Kigamboni.
Anasema kupitia uamuzi wa Serikali, viwango vya tozo vilishushwa na kuanzisha malipo kwa utaratibu wa vifurushi (bundle) ambavyo vina unafuu mkubwa kwa watumiaji wa Daraja.
Bw. Mshomba anasema wastani wa makusanyo ya mapato katika Daraja la Nyerere, yameongezeka kwa mwezi kutoka shilingi bilioni 1.13 mwezi Februari 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 1.89 katika kipindi cha mwezi Februari 2025, sawa na ongezeko la asilimia 66.
Changamoto za miradi ya uwekezaji iliyokuwa imesimama zimetatuliwa
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Mshomba anasema Mfuko umetatua changamoto zilizokuwa zinakabili miradi ya ujenzi na kusababisha miradi ya Dungu, Toangoma, Kijichi III, Mzizima na Hoteli ya kitalii Mwanza kusimama kati ya mwaka 2016 na 2021 kupisha zoezi la ukaguzi maalumu. Anasema utatuzi uliofanyika unahusisha upatikanaji wa mwendesha hoteli kwa ajili ya miradi ya Mzizima na hoteli ya kitalii ya Mwanza pamoja na kutatua changamoto za mikataba na wakandarasi waliokuwa wametekeleza miradi ya Dungu, Toangoma na Kijichi III.
“Kwa sasa miradi yote hii inaendelea na kutarajiwa kukamilika kati ya Juni 2025 na Juni 2026,” anasema Bw. Mshomba.
Skimu ya Uchangiaji wa Hiari kwa Wananchi waliojiajiri
Mshomba anasema Mfuko unajivunia kutoa huduma za hifadhi ya jamii kwa wananchi walioajiriwa kwenye sekta binafsi na waliojiajiri kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020- 2025 na Ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia umuhimu wa Watanzania kujiunga na kunufaika na sekta ya hifadhi ya jamii, jukumu ambalo linatekelezwa vyema na NSSF.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete akitoa elimu kwa wananchi waliojiajiri wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya “NSSF Staa wa Mchezo” Mbagala Zakhem, Dar es Salaam.
Anasema Mfuko unaendelea na maboresho ya Skimu ya uchangiaji wa hiari kwa wananchi waliojiajiri (Hifadhi Scheme) ambapo kupitia mpango huo wananchi waliojiajiri katika shughuli mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sekta ya usafirishaji (boda boda, bajaji) mama na baba lishe pamoja wajasiriamali wengine wote wataweza kupata huduma za hifadhi ya jamii kama wanavyonufaika wanachama walioajiriwa katika sekta binafsi.
Anasema hadi kufikia mwezi Februari 2025, wanachama 437,319 wamejiunga kwenye skimu hiyo na wanaendelea kunufaika na mafao kama pensheni ya uzeeni, urithi, uzazi, matibabu, ulemavu na mafao ya kujitoa. Skimu ya Hifadhi (Hifadhi Scheme) inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi Aprili, 2025.
Mshomba anasema tayari Mfuko umezindua kampeni ya “NSSF Staa wa Mchezo” ambapo ujio wa “Hifadhi Scheme” unatoa nafasi kwa NSSF kushika usukani na kuwa staa wa mchezo katika maisha ya uzeeni au pindi majanga yanapotokea kwa wananchi waliojiajiri. Kujiunga na kuchangia ni rahisi tu kwa kubofya *152*00# ambapo mwanachama anaweza kuchangia shilingi 30,000 au zaidi kwa kutoa kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi au msimu kulingana na kipato chake na kunufaika na mafao yote yanayotolewa na NSSF yakiwemo ya matibabu.
Matarajio ya Mfuko kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu
Bw. Mshomba anaeleza kwamba matarajio ya Mfuko ni pamoja na;
• Kuendelea kutekeleza mikakati ya ukuaji wa Mfuko ili kuhakikisha kwamba thamani ya Mfuko inafikia zaidi ya shilingi trilioni 11 mwezi Juni 2026, ikiwa ni mara mbili ya thamani ya shilingi trilioni 5.078 iliyofikiwa mwezi Juni 2021.
• Kuendelea kubaini fursa za uwekezaji katika maeneo mapya yenye faida zaidi na salama ikijumuisha masoko ya hisa na mitaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC ili kuweza kuwa na mtawanyo mzuri wa vitega uchumi.
• Kuimarisha mifumo na matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi, kupunguza malalamiko kwa wateja na kutoa huduma bora kwa wanachama wake.
• Kuendelea kutekeleza Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi waliojiajiri yaani “Hifadhi Scheme” ili kuvutia wananchi waliojiajiri kujiunga na huduma za Hifadhi ya Jamii ambapo watanufaika na huduma mbalimbali zinatotolewa ikiwa ni pamoja na mafao ya matibabu.
Mshomba anahitimisha kwa kutambua mchango na ushirikiano ambao Mfuko umepata kutoka kwa waajiri na wanachama wetu kote nchini kama sehemu ya mafanikio anayoyaeleza.
“Niishukuru tena Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi hiki cha miaka minne (4) kwa kuweka mazingira mazuri na wezeshi ya uwekezaji na hivyo kuruhusu wawekezaji wengi nchini waliochangia kukuza ajira na kuongeza idadi ya wanachama kwa Mfuko”. Anaeleza Mshomba.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu anaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wadau wa Utatu (ATE, TUCTA, Serikali) Msajili wa Hazina, Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi thabiti wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini.
“Nitoe rai kwa waajiri wote nchini kuzingatia sheria za kazi na kutekeleza jukumu la kuwasilisha michango ya watumishi wao kwa mujibu wa sheria ili kuwezesha jukumu la ulipaji wa mafao kufanyika kwa haraka,” amesema. Mshomba.