
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF) umeitambua Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuwa kinara wa vyombo vya habari nchini kwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wake kwa wakati kila mwezi.
Tuzo hiyo ya heshima imetolewa leo Jumanne Oktoba mosi, 2024 jijini Dar es Salam na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba katika kikao kazi baina ya NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kupokewa na Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo wa MCL, Rashid Kejo.
MCL ni wazalishaji wa maudhui ya Mwananchi, MwanaSpoti, The Citizen, Mwananchi Digital na wasafirishaji wa mizigo maeneo mbalimbali Tanzania.
Mbali na MCL, kampuni nyingine zilizotambuliwa kwa uchangiaji wa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ni IPP Media, Azam Media na Jamhuri Media.
Akizungumza baada ya tuzo hizo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema vyombo vya habari vilivyotambuliwa kwa kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati, sio kwamba vina fedha nyingi, bali ni kuheshimu taratibu za fedha za nchi.
“Michango hii haitafikia mahala kuwa mzigo mkubwa kama ikilipwa kila mwezi, hii michango inalipika,” amesema Balile ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri.
Amesema kuna kampuni zinalipa mishahara karibu Sh20 milioni ya wafanyakazi wake kwa mwezi, lakini zinashindwa kulipa angalau Sh1 milioni ya michango hiyo ya NSSF kwa correspondents.
Hata hivyo, Balile ametoa rai kwa wahariri wa vyombo vya habari akisema, “tujipange na tuwalipe correspondents kwa wakati na tuchangie michango hii kwa wakati, taasisi yoyote inaweza kulipa mafao ikiamua.”
Awali, Mshomba alisema wanaboresha mifumo ya Teknolojia na Habari na Mawasiliano (Tehama), ili shughuli zote zifanyike katika mfumo huo.
“Kwa sasa tunafanya shughuli zetu kwa mfumo wa Tehama kwa asilimia 82, tunataka mpaka itakapofika mwisho wa mwaka huu wa fedha, shughuli zote zifanyike katika mtandao.
“Tunataka kuwafikia waajiri na wanachama wetu kwa urahisi zaidi na wachangie moja kwa moja kupitia mfumo. Pia, hadi mwishoni mwa mwaka huu wa fedha tunataka wanachama wawasilishe madai ya mafao yao kwa mtandao,” alisema.
Akitoa wasilisho kuhusu utoaji huduma kwa watu waliopo sekta isiyo rasmi, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omari Msiya amesema wamejumuishwa ili waongeze wigo wa wananchi kwa kutoa fursa ya hifadhi ya jamii kwa makundi ambayo hayanufaiki na huduma hizo, ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa nchi.
Amesema mwanachama anayetaka kujiandikisha anatakiwa kuwa na namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) iwapo hana kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpigakura au leseni ya udereva pamoja na picha moja.
Mziya amesema wakishajiunga na kuchangia Sh30,000 kila mwezi watanuifaika pia na fao la ziada la matibabu na ikiwa atachangia Sh52,200 kwa mwezi atanufaika na fao hilo la matibabu pamoja na mke/mume pamoja na watoto wao.
Shuhuda anavyonufaika na mafao
Flora Wingi, mhariri mstaafu amesema sasa anafurahia mafao yake baada ya utumishi wake na kuchangia katika mfuko huo kwa miaka 41.
“Nilianza kazi mwaka 1978 kampuni ya Uhuru na Mzalendo, nilifanya kwa miaka 18 na wakati huo nilikuwa nikichangia mfuko wa hifadhi ya jamii ukiitwa NPF, mwaka 1996 nilihamia Gazeti la Nipashe, lakini sikuchua pesa zangu niliendelea kuchangia mpaka mwaka 2019 nilipostaafu.
“Aprili 2019 nilipostaafu nilianza kufuatilia mafao yangu na baada ya miezi minne nilipata. Septemba mwaka huo huo nikaanza kupokea mafao yangu ya kila mwezi mpaka sasa,” amesema Wingi ambaye alipata tuzo ya kutochukua mchango hadi anastaafu.
Wanahabari wengine wastaafu waliopata tuzo hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu, Jesse Kwayu, Absalom Kibanda, Betrice Bandawe na Mbaraka Islam.